Mpendwa msomaji ni karibu wiki mbili sasa sijaandika safu hii. Nimepata simu, ujumbe mfupi (sms) za kutosha – wengi wakiuliza kulikoni mbona siandiki. Niwaondoe hofu, kuwa kila kitu ni salama tu, isipokuwa mitanziko ya hapa na pale.
Niwashukuru pia wote walionipigia simu au kuwasiliana nami kwa njia mbalimbali, kwa nia ya kunipa pole kutokana na majambazi walionipora laptop nikiwa wilayani Songea kikazi. Nasema asanteni sana.
Kwa karibu mwezi sasa nchi yetu imegubikwa na mambo makuu mawili; uchaguzi wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na harakati za ndugu zetu na Watanzania wenzetu, Waislamu. Wameandamana, wamekamatwa, wengine wamefikishwa mahakamani na wengine wametuhumiana kulipuana kwa mabomu!
Napata wakati mgumu kujadili mada hizi mbili kwani tayari zimejadiliwa kwa kina, hasa katika mitandao ya kijamii ambako watu wanajimwaga kwa uhuru wa kutosha. Jingine linalonipa shida kujadili mada hizi ni munkari na upupu unaosambazwa na walio na nia zao kuhusiana na mada hizi mbili.
Hata hivyo, kuandika ni jukumu langu la msingi na kwa mantiki hiyo yanipasa kuzijadili bila kutia chumvi wala kuliita beleshi kijiko kikubwa, bali beleshi.
Sitanii, naanza na hili la uchaguzi ndani ya CCM. Nimefuatilia kwa karibu mno malalamiko ya kuwapo kwa rushwa katika uchaguzi huo unaoendelea kwa ngazi mbalimbali, ambayo ni mengi kwa kiwango cha kutisha.
Napata shida zaidi juu ya tuhuma hizi inapobainika kuwa ndani ya CCM kila mtu sasa analalamika. Kila mtu analia na kupaza dua la kuku lisilompata mwewe. Mwenyekiti wa CCM, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, naye amepanda basi la malalamiko.
Wote wanazungumza kwa mafumbo. Wamenikumbusha maneno ya Mwalimu Julius Nyerere katika kitabu chake cha “Tanzania na Hatima ya Uongozi Wetu.” Mwalimu anasema kama taifa tutakuwa tunafanya kosa kubwa kufikiri kuwa miongoni mwa panya atapatikana mmoja mwenye ujasiri wa kumfunga paka kengele, iwasaidie kutambua alipo kila wakati.
Mwalimu alikwenda mbali zaidi akasema tutakuwa watu wa ajabu kabisa kudhani kuwa miongoni mwa paka atajitokeza mmoja mwenye kuwahurumia panya, ajifunge kengele mwenyewe kuwasaidia kujitambulisha kwao kila mara anapowakaribia kwa kengele aliyojifunga shingoni kujipiga. Sisemi CCM wako hivyo, ila kama ipo tufauti unahitaji kuwasha tochi mchana wakati wa jua kali kuweza kuibaini!
Sitanii, ukiacha hilo kwamba ndani ya CCM wote falsafa yao moja, malengo hayatofautiani na wachache mno wasiojaa kwenye kiganja, bado wana uwezo wa kufanya uamuzi, napenda kuamini kwa CCM ya sasa anayeshindwa katika uchaguzi wowote basi hakuna kingine bali ameangushwa na rushwa.
Tena kibaya zaidi, kila anayeshindwa au kundi linaloshindwa wanaona njia pekee ya kupata huruma ya jamii ni kusema “Edward Lowassa ametoa rushwa mtu au kundi lao lishindwe”. Nasema huu ni ujinga mpya katika taifa letu.
CCM wanataka kutuaminisha sasa kuwa Lowassa alichangia ushindi wa Mbowe, Zitto, Nassari, Mdee, Mchungaji Mdelwa, Dk. Mbasha na majimbo yote ya Pemba ambako CUF waliifagia CCM bila huruma!
Sitanii, mchezo huu wa kila anayeshindwa kuegemeza kushindwa kwake kwa Lowassa kutatufikisha pabaya kama taifa. Kelele wanazopiga sasa viongozi ndani ya CCM dhidi ya Lowassa zinathibitisha maneno ya Mzee Yusuf Makamba, kwamba mti wenye matunda ndiyo unaorushiwa mawe. Nani ahangaike na michongoma?
Kuna watu wanafanya mchezo katika siasa. Mtu anasimama anawatangazia wafuasi wake kuwa ameacha siasa na hatashiriki tena milele, kisha anarudi kuwaomba kura. Anabwagwa na mwanamama mahiri, analia eti Lowassa kammwagia upupu. Kuna akili hapo kama si kuthibitisha uziro?
Kinachonishangaza katika mchakato huu sijasikia hata mtu mmoja aliyeshinda akilia rushwa imetumika hata kama Lowassa anamsikia redioni tu. Lakini pia wingi wa kelele dhidi ya Lowassa na muungano wa wanasiasa na makundi ndani ya CCM dhidi ya Lowassa, unapaswa kuwafanya wenye akili wajiulize kwa nini Lowassa.
Ni wazi ingawa inawakera baadhi ya watu, Lowassa anao uwezo wa kusimamia mambo na kuamua, hata kama kwa kufanya hivyo atafanya makosa machache.
Nchi hii inahitaji kiongozi wa kufanya maamuzi 100 kwa wakati hata kama atakosea matano kati ya idadi hiyo. Umbea unaosambazwa sasa na wanasiasa ndani ya CCM kufunga ndoa bandia ni hatari kwa mustakabali wa taifa hili.
Sitanii, ikiwa rushwa inasambazwa wahusika wakamatwe. Nasema santuri ya kauli za rushwa ndani ya CCM imechuja, yawapasa wahusika kuchagua wimbo mpya. Ikibidi watueleze ukweli iwapo msemo wa “Asiyekubali kushindwa si mshindani” umepoteza maana pia. Nilisema nitajielekeza kwenye mada mbili, safu hii inazidi kupungua ila yanipasa japo kwa ufupi kuzungumzia vurugu za kidini zinazoendelea hapa nchini.
Sitanii, Watanzania tunakaribisha hatari kubwa. Tunakaribisha mgawanyiko na vita isiyo na tija kwa ustawi wa taifa letu. Tumeanzisha vita ya udini ambayo ni hatari kuliko vita ya kisiasa inayoendelea kama niliyoitaja hapo juu ndani ya CCM.
Mchezo wa makanisa kuchomwa moto, Waislamu kuandamana na baadhi ya watu kuanza kuua askari polisi huku wengine wakilipuana kwa mabomu, tuuache ni wa hatari.
Mataifa mengi watu wanapambana kupata amani, sisi inaelekea tumeichoka. Tunafanya kila mbinu ipotee. Kumbuka habari kwamba ukifa duniani thawabu unapata mbinguni haijapata kutibitika.
Sitanii, katika hili nasema hapana. Polisi dhibitini mihadhara na makanisa yanayofanya uchochezi kwa kuwasha vipaza sauti usiku wa manane. Tukiruhusu udini ukatugawa, tutajuta sisi na vizazi vyetu. Nasema yote yanayoendelea ni siasa uchwara na baadhi ya watu kufilisika kisera, kwani wakifilisika wanaamua kutumia udini, rushwa, ukabila na umajimbo kujihalalisha.
Sitanii, tukatae vilio visivyo na majibu, atakayetuhumu rushwa asonge mbele na kwenda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwataja watuhumiwa, kisha atoe ushahidi wahusika wafungwe badala ya tuhuma za jumla. Mungu ibariki Tanzania.