Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ameweka kando majibu ya tafiti zote na badala yake, ameelekeza masikio yake Oktoba 25, mwaka huu.
Katika kusisitiza hilo, Lowassa ameonya mizengwe inayoripotiwa kufanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kile kinachoelezwa kuwa kutengeneza mazingira ya kukipa ushindi.
“Majibu ya utafiti na matokeo pekee yatapatikana Oktoba 25, mwaka huu. Na katika hili Watanzania wasiwe na wasiwasi, nakwenda kuwatumikia tu basi,” anasema Lowassa alipohojiwa na JAMHURI mwishoni mwa wiki iliyopita.
Lowassa amesema kwamba asingependa kuegemea zaidi kwenye takwimu hizo, badala yake ametaka NEC kutofanya kazi kwa kusukumwa na takwimu hizo.
Takwimu zilizoripotiwa hadi mwishoni mwa wiki iliyopita ni za Taasisi ya Twaweza, Kampuni ya Ipsos, Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC pamoja na Tadip.
Twaweza na Ipsos zimempa nafasi ya pili Lowassa nyuma ya Dk. John Magufuli wa CCM wakati nyingine zimeonesha atashinda uchaguzi huo wa awamu ya tano tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi Tanzania.
Anasema: “Kwa Umoja huu… mimi si mtu wa kushindwa na sitakubali kushindwa urais hadi itakapooneka wazi kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Anasema kwamba haoni sababu ya mambo kutokwenda sawa katika uchaguzi huu na kwa namna ya mwamko wa Watanzania ulivyo, “Kwani wengi wana elimu ya uraia.”
“Tutadhibiti wizi wa kura. Na hili likifanikiwa tutasubiri matokeo ya ridhaa ya Watanzania. Wasianze kuwatisha Watanzania sasa kwa kuwapa matokeo ambayo hayapo na wala si ya kweli. Watanzania wasubiri tarehe 25 Oktoba, wakapige kura na ndipo watapata majibu.”
Lowassa anasema ana ndoto nyingi za kuifanyia Tanzania na kwake ingekuwa rahisi kutekeleza hata kama angebaki CCM, lakini “Sasa Mungu ameandika nifanye mabadiliko nikiwa Ukawa.”
Mara kwa mara Lowassa amekuwa akiituhumu CCM kuwa ni hodari wa kuiba kura hivyo anawataka wananchi wajitokeze kumpigia kura kwa wingi ili hata kama kura zikiibwa, ashinde kwa kishindo.
Anasema hata kama angebaki CCM, angekikosoa chama hicho, akisema, “Kuna mambo ambayo ni lazima ningeyazungumza ambayo ningeyasafisha, lakini CCM haisafishiki tena.”
Anasema japo CCM imejitahidi kufanya mambo yake katika utawala wake, lakini kuna mengi ambayo yanatakiwa kufanywa kukuza uchumi kwa kutumia vizuri rasilimali zilizopo kuleta maendeleo.
Lowassa alihamia Chadema Julai 28 mwaka huu, akitokea CCM baada ya jitihada zake za kugombea urais katika chama hicho kinachoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, kugonga mwamba baada ya jina na lake kuenguliwa mapema kabla ya tano bora ambayo huchujwa na Kamati Kuu (CC).
Kuhamia kwake Chadema kumeleta upinzani mkali katika uchaguzi wa mwaka huu hasa baada ya kuteuliwa kuwa mgombea urais.
Kilio cha Lowassa ni kwamba hali ya uchumi kwa sasa ni mbaya na iwapo Mungu atamjalia atawaongoza Watanzania katika mustakabali mwema.
Lowassa amekuwa akiitikisa kambi ya chama tawala CCM kutokana na kuvuta hisia kubwa kwa Watanzania hasa baada ya kujiunga na Chadema kwani hatua ya kutangazwa kwake kugombea urais kupitia Chadema imewafanya CCM kuwa na wakati mgumu.
Lowassa anawania nafasi hiyo kwa mwamvuli wa vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambayo ni National League for Democracy (NLD), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na Chadema kilichompa tiketi.
Shutuma dhidi ya CCM zimemwibua mmoja wa wapiga kampeni wa Dk. Magufuli akidai Chadema imeandaa mikakati kamambe ya vurugu ikiwa Lowassa atatangazwa kushindwa Uchaguzi Mkuu.
Anadai kwamba mgombea urais wa chama hicho anaandaa pia mkakati wa kumshawishi Maalim Seif Sharrif Hamad anayewania urais wa Zanzibar kupitia CUF, ayakatae matokeo ya urais upande wa Zanzibar iwapo atatangazwa ameshindwa na baada ya hapo waanzishe vurugu Zanzibar wakati vurugu nyingine zikiendelea upande wa Tanzania Bara.
Kada huyo ambaye kwa sasa ameomba jina lake lisitajwe anasema mkakati huo umepangwa kufanywa na Lowassa akiwatumia walinzi zaidi ya 10,000 wa Red Brigade ambao wanadaiwa kuwepo kila mkoa ambao wanatokana na Chadema.
Katika kusuka mikakati hiyo kwa nyakati tofauti kuanzia Julai, mwaka huu Lowassa anadaiwa kuitisha kikao na viongozi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema kilichofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Chadema yaliyopo Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
“Wakati wa kikao hicho Lowassa alitaka kujua idadi ya walinzi wa Red Brigade nchini na ujuzi na utaalamu wao,” imeeleza sehemu ya taarifa ambayo JAMHURI ina nakala yake.
Habari zinaeleza kwamba katika kikao hicho ambacho Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikuwepo alimweleza Lowassa kwamba wana kikosi kikubwa ambacho wengi wao wamewahi kupitia mgambo, Jeshi la Kujenga Taifa, na Askari Wastaafu na kwamba kila mkoa una walinzi wasiopungua 200.
Habari zinapasha kwamba Lowassa ameeleza kwamba hana mpango wa kushindwa urais na pia hatakubali matokeo iwapo atatangazwa kuwa ameshindwa hatakubali matokeo.
“Hivyo Lowassa alieleza kwamba mara baada ya uchaguzi mkuu walinzi hao wakusanywe katika miji minne ya Arusha, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza kwa ajili ya maandalizi ya kuanzisha vurugu kama atakuwa ameshindwa. Walinzi hao watalipwa vizuri ili watekeleze kazi hiyo vizuri,” imeeleza taarifa hiyo.
Habari zinaeleza kwamba katika mjadala huo lilitokea swali la namna Lowassa atakavyopata Urais, na katika kujibu ameeleza kuwa suala hilo aachiwe mwenyewe na marafiki zake huku akiushauri uongozi wa Chadema na Ukawa kwa ujumla washughulikie upatikanaji wa wabunge na madiwani.
“Vile vile Lowassa alisema atahakikisha Mhe. Rais Jakaya Kikwete anamkabidhi nchi hii ikiwa salama. Baada ya uchaguzi kumalizika Lowassa atawaomba rafiki zake msaada mbalimbali kwa ajili ya kuleta machafuko ikiwa atanyang’anywa ushindi ambao ana uhakika wa kushinda,” anasema.
Kwa mujibu wa habari, kusudi la mipango hiyo inayopangwa na mgombea huyo ili Jumuiya ya Kimataifa iingilie kati kwa kusema uchaguzi haukuwa huru na ikiwa jambo hilo litapigiwa kelele kwa kiasi kikubwa itakuwa vigumu kuendesha Serikali ijayo ya awamu ya tano.
Kusikia hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva aliyekuwako Arusha wiki iliyopita, mara moja ameliambia JAMHURI, “Tume haiangalii majibu ya takwimu hizo, badala yake inasimamia uchaguzi na kutoa matokeo sahihi.”
Akaongeza: “Kama nilivyopata kusema huko nyuma kwamba ni msimamo wa tume kwamba tutafanya kazi kwa weledi na zaidi ya yote kwa uwazi, sidhani kama hiyo mizengwe itakuwako.
“Nchi itabaki na amani, kwa sababu ya ukweli ambao sisi tutaufanya ndiyo maana tumeagiza kubandika matokeo yote kila kituo na msimamizi wa uchaguzi katika kata atakuwa na mamlaka ya kumtangaza mshindi wa udiwani pekee, ila matokeo yote atabandika ukutani.
“Kisha yule msimamizi ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa au Halmashauri atatangaza matokeo ya ubunge, na yale ya Rais atabandika tu na ile takwimu ataituma tume ambayo kisheria ndiyo itatangaza matokeo ya urais.
“Kwa weledi na uwazi na timu iliyoko Tume, kila kitu kitakuwa wazi. Hivyo nigependa kuwatoa hofu Watanzania kwamba kutakuwa na shida. Hapana, kila kitu kitakuwa wazi,” anasema Jaji Lubuva.
Wananchi kadhaa waliozungumza na JAMHURI, wanasema kuwa hawasadiki majibu ya tafiti hizo zilizotangazwa kwa siku tofauti wiki iliyopita.
Mkazi wa Dar es Salaam, aliyejitambulisha kwa jina la Ioche akitumia namba ya simu, 0655 364676 amsema: “Twaweza hawana jipya na tafiti zao hazina ukweli. Ni sawa na kuwapoza viongozi wa chama chao cha CCM.
Kadhalika, Mkazi wa Arusha aliyepiga simu ofisi za gazeti hili na kuridhia namba yake 0787 683360 itumike lakini si jina lake, anasema: “Hakuna shaka tafiti za uchaguzi mkuu zina dalili ya kupikwa kwa kuibeba CCM.
“Kauli za makada wa CCM kwamba watashinda kwa bao la mkono na liwalo na liwe CCM haitaachia Ikulu, ni ushahidi tosha na Tume ya Uchaguzi inayumbayumba.”
Kuhusu usalama wa nchi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe ambaye wizara yake ina dhamana ya usalama wa watu na mali zao, anasema hadi sasa mambo yanakwenda sawa kwa sababu nchi iko salama na hakuna matishio ya aina yoyote ya uvunjifu wa amani na wala hatarajii kuona uchaguzi huu unaingiza nchi katika machafuko ya aina yoyote.
Anaeleza kuwa Watanzania wanatakiwa kuwa waangalifu na kauli zao katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anakuwa mlinzi wa usalama.
Pia anasema kuwa wagombea wote nchini wanatakiwa kufuata sheria za uchaguzi kwa kufanya mikutano ya kampeni na kujihadhari kutoa kauli zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
“Wagombea lazima watambue kuwa majukwaa ya kampeni yasitumike kuchochea na kuvuruga amani ya nchi, wafuate sheria na taratibu za uchaguzi zilizowekwa na tume ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuwa walinzi wa amani ya nchi,” anasema Chikawe.
Waziri Chikawe anatoa angalizo kwa wale wote wenye nia ovu ya kusababisha vurugu za aina yoyote katika kipindi hiki cha uchaguzi kuwa jeshi la polisi halitosita kuwachukulia hatua za kisheria.