Binadamu tumeumbwa katika hali ya ajabu sana, ambayo kadiri mtu anavyokuwa katika nafasi fulani ya juu – iwe ni madaraka, elimu, siasa na wakati mwingine hata umri – ni nadra kusikiliza ushauri unaotolewa na mtu au kundi jingine ambalo liko tofauti au chini yake. Hii ni hulka pia ipo kwetu Watanzania
Asilimia kubwa ya viongozi walio juu katika nafasi fulani fulani za kisiasa, katika baadhi ya madhehebu ya dini, kifamilia na kadhalika, hujiona wao ni kila kitu na hujinyima nafasi ya kusikiliza ushauri wa wengine hata kama ni wa msingi.
Hali ya ujivuni wa namna hii inachangiwa pia na imani na mila potofu kuwa mkubwa hakosei!
Viongozi wengi wa kada mbalimbali huamini kuwa watu walio chini yao ni wajinga, hawana maono huku wao wakijiona kuwa ni werevu. Viongozi hawa kama wangethubutu kusikiliza maoni ya wengi wangeweza kugundua mambo mengi ya msingi yenye tija kwa wote.
Kila binadamu amepewa karama yake, wapo wenye kubwa na ndogo ndogo kwa ustawi wa maisha yao.
Mwanasiasa Edward Ngoyai Lowassa anatikisa miji, mikoa na nchi kwa ujumla. Lowassa anatikisa kila anapopita anaacha mtikisiko, kila Mtanzania sasa anazungumzia urais na Lowassa.
Tumeshuhudia chaguzi nyingi nchini lakini uchaguzi wa mwaka huu unakuwa kama ule unaotakiwa kutimiza maandiko – maandiko ya kuporomoka kwa chama tawala kilichoweka mizizi kwa nusu karne kikiporomoshwa na mtandao.
Lowassa alikatwa na CCM. Walimkata bila kujitafakari, walimkata wakambeza. Hawakufikiri nje ya boksi. Akajing’atua kutoka kwa wakataji wake, akajiunga na kile kinachoaminiwa kuwa ni nguvu ya umma. Kuondoka kwa Lowassa CCM ni pigo. Ni pigo la wazi wazi hata kama watakataa. Anakiumiza chama kutokana na kuondoka kwake kunakokibomoa kwa kukimong’onyoa.
CCM ilikosea, baada ya kukata jina lake iliendelea kumbeza, na kumzodoa kuwa imezuia mafuriko kwa kidole. Kitendo hiki ni sawa na kurusha mawe katika mzinga wa nyuki ulio jirani na makazi ya watu.
Sasa Lowassa hana tena yale mafuriko yaliyozuiwa kwa ncha ya kidole, ana vimbunga, tsunami na gharika zisizokoma kila anapokwenda.
Pamoja na kuwa CCM ni vigumu kuukubali ukweli, chama sasa kinaumia, kinaumbuka na kuzodolewa na wananchi. Wenyewe wanasema jiwe walilolikataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Viongozi wa CCM wanaonekana kukosa ubunifu wa kukibadilisha chama kiwe cha kisasa, ambacho kitakabiliana na changamoto za sasa na mchakamchaka wa vyama vingi.
Wanasema Lowassa ni msanii, anafanya sanaa. CCM wameshindwa kuenenda na sanaa za Lowassa na Ukawa kwa ujumla, wanalalamikia mafuriko na gharika.
Lowassa amekuwa rais kabla hata hajachaguliwa. Mvuto wa Lowassa umeongezeka, pamoja na kuwa wapo ambao hawakubali ukweli huu ila ndivyo ilivyo. Wote tumekuwa mashuhuda wa kile kinachoendelea nchini. Kampeni bado hazijaanza, lakini kile kinachoonekana kwa macho kila mmoja wetu anakiona.
Watanzania wanalalamika kutosikilizwa, wameamua kufanya uamuzi – uamuzi wa nje ya chama. Viongozi wa CCM wameamua kujiengua katika nyadhifa zao kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni ubabe, ubinafsi na kutosikilizwa ndani ya chama.
CCM inapoteza wanachama wake na wapiga kura wake, wameondoka na wanazidi kujiengua ndani ya chama na kumfuata Lowassa. CCM inapuuza na kuwabeza. Ama kweli sikio la kufa halisikii dawa.
Ni lazima CCM ijitafakari upya, kujua wapi imekosea na kujikosoa kabla wanachama wake wengi hawajaamua kukisusa chama na kujiunga na vyama vya upinzani.
Lowassa sasa ni lulu, ana mvuto wa ajabu. CCM imemfanya Lowassa kuwa rais kabla hata ya kuchaguliwa na wapiga kura. Viongozi wengine nchini hawasikiki tena, hawaonekani, wamepotea. Wamemezwa na Lowassa.
Napatwa na shaka na matamko ya CCM ya mara kwa mara, matamko ya kumfananisha yeye wanachama wanaojiengua ndani ya chama kuwa makapi huku chama kikizidi kumong’onyoka.
CCM wanalo la kujifunza kutoka kwa Lowassa. Wanaijua nguvu yake ndani ya chama na nje ya chama. Walianzisha mtandao, mtandao unaokiua chama na kumuweka Lowassa madarakani kabla hajachaguliwa.
Lowassa ana falsafa ya nguvu ya umma, anapendwa na vijana. Vijana wanadai mabadiliko ambayo katu hawawezi kuyapata ndani ya Chama Cha Mapinduzi. Lowassa ana nguvu ya umma.