.Wasaidizi wake wasema “Mzee sasa ana amani”
NA WAANDISHI WETU
Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, kwa mara ya kwanza amemtaja Rais Jakaya Kikwete ndiye anayefahamu kwa kina mkataba wa Kampuni ya Richmond uliosababisha nchi kupata hasara ya mamilioni.
Lowassa anasema, “mamlaka ya juu” ukiachilia mbali yeye aliyekuwa waziri mkuu wakati huo mkataba ukisainiwa ilikuwa inajua kila hatua na kwamba ndiye alikuwa akimaanisha Rais ambaye kwa sasa ni Jakaya Mrisho Kikwete.
Anayetafsiri mamlaka ya juu ni Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Antipas Lissu, aliyezungumza na JAMHURI mambo mbalimbali hasa linalohusiana na nyadhifa na kuhamia kwa Lowassa Chadema.
Akizungumza kwa utaratibu na kupangilia maneno na sentensi, Lissu anasema kwamba ni ngumu kwa mkataba ule wa Richmond uliogharimu uwaziri mkuu wa Lowassa kushirikisha kiongozi mmoja tu katika mfumo wa uongozi.
“Kashfa ile kubwa haiwezekani kumhusisha Lowassa peke yake,” anasema Lissu na kuongeza: “Lowassa ametoa majibu, amesema kilipoanza kunuka aliwaambia makatibu wakuu…jamani eeeh tuvunje huu mkataba.
“Sasa Philip Luhanjo ambaye ni Katibu Mkuu kiongozi wakati huo akawaambia kwamba amezungumza na Rais (Jakaya Kikwete), Rais amekataa. Tuendelee. Wakati huo Rais Kikwete alikuwa safari.
“Si Luhanjo pekee. Hata Gray Mgonja wakati ule akiwa Katibu Mkuu wa wizara ya Fedha, alimwamba, mkataba uendelee maana mamlaka ya juu imeamua hivyo,” anasema.
“Aliporudi Rais Kikwete nchini. Maana hakuwako. Mheshimiwa Lowassa alimfuata akamwambia kimenuka, tuvunje huu mkataba…Rais akasema nimeshauriwa na makatibu wakuu wangu, tusivunje huu mkataba. Tuendelee nao. Sasa Lowassa akawajibika kisiasa.”
Lowassa anamtaja Rais Kikwete hivi karibuni wakati anakaribishwa Chadema ambako yeye na mkewe, Regina Lowassa walipewa kadi mpya za kutambulika kuwa wanachama halali wa chama hicho.
Lowassa alisema hayo baada ya kuhojiwa na mmoja wa waandishi ambako katika majibu ya kukana kuhusika kwake, alikwenda mbali akisema, anayedhani kwamba ana ushahidi, apeleke mahakamani.
“Nipende tu kusema mimi kama waziri mkuu. Kwa kawaida ya sheria huwa ninaletewa mkataba muda wa mwisho kuupitia na kuupitisha… huwa sihusiki na kuandaa mikataba…
“…Mwenye mamlaka ni waziri husika, hivyo baada ya kuletewa mkataba husika wa Richmond niliupitia na kiukweli niliuwekea shaka kwa sababu nilishawahi kuwa waziri wizara ya maji nina uzoefu na kuandaa mikataba.
“Nilishauri mkataba huo uvunjwe lakini, waziri wa nishati na akawasiliana na ngazi ya juu na kulazimishwa kuupitisha mkataba huo,” anasema Lowassa.
Baada ya kugundua mkataba huo kuwa na upungufu mwingi, anasema: “Nilichukua maamuzi magumu (uamuzi mgumu) na kubeba mzigo wote ndio maana hadi leo wanasema mimi ni fisadi wa Richmond.
“Nipende kumaliza kwa kusema kwamba mwenye ushahidi wa Richmond aende Mahakamani. Vinginevyo watu wafunge midomo yao na kukaa kimya,” anasema.
Hii si mara ya kwanza kwa Lowassa kuzungumzia kashfa hiyo kwani Mei, mwaka huu wakati anatoa taarifa kuwa ana safari ya kwenda Arusha, kutangaza nia ya kuwania urais, Lowassa alizungumzia hilo akiwa Dodoma.
Huko Lowassa alisema kwamba chuki na roho mbaya dhidi yake hasa katika nafasi ya uwaziri mkuu ilikuwa ajenda iliyosababisha kujiuzulu kutoka kwenye wadhifa huo miaka saba iliyopita.
Kadhalika, Lowassa alipata kulisema hilo kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Novemba, mwaka 2011 baada ya kushutumiwa na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM kuwa ni fisadi.
Kwenye kikao hicho, Lowassa alipopewa nafasi ya kusema, alinukuliwa na baadhi ya wajumbe akisema, “Mwenyekiti (akiwa na maana Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete) utakumbuka kwamba mimi nilishaamua kuvunja mkataba wa Richmond mapema…
“…Lakini baada ya kukupigia simu ukiwa katika safari nje ya nchi ulisema tusubiri kwani ulikuwa umepata ushauri wa makatibu wakuu wa wizara, sasa leo (siku hiyo ya kikao) hii ninahukumiwa na kuitwa fisadi kwanini?”.
“Nilijiuzulu kuwajibika kwa ajili ya kuilinda Serikali yangu na kwa heshima ya chama changu, sasa kwanini leo (siku hiyo ya kikao) nahukumiwa kwa jambo hili, tena natukanwa na wanaCCM wenzangu na siyo wapinzani nchi nzima kwamba mimi eti fisadi?
Taarifa zinasema hoja ya Lowassa ilizimwa mara moja baada ya kutoa kauli ifuatavyo, “Mwenyekiti nikukumbushe mwaka 1997 kule Zanzibar, kina Mzee Daudi Mwakawago walikuja na mafaili yakiwa na tuhuma dhidi ya mtizamo hasi wa jamii dhidi yako, kwa hiyo wakati ule kama si busara za kina Mzee Mkapa (Benjamin) leo usingekuwa hapo ulipo.”
Akizungumza namna ambavyo Chadema wamempokea Lowassa, Lissu anasema kwamba mapendekezo ya chama chao ilikuwa ni kushawishi hatua za kisheria, kitu ambacho hakikufanywa na Serikali ingawa mwanasiasa huyo mkongwe aliwajibika kisiasa.
“Hatujawahi kusema kwamba wasipowajibishwa, basi hatutawapokea. Tunataka watoke kwenye CCM, ili tuiwajibishe CCM na tujenge nchi upya kwa misingi ya isiyokuwa ya ki-CCM,” anasema Lissu.
Anasema kwamba katika hali ya kawaida na mazingira ya sasa ya siasa inayohitaji mabadiliko ni ngumu kumkwepa Lowassa kwa sababu ana nguvu ndani na nje ya CCM pamoja na kwenye mfumo unaotawala.
Anasema kwamba Chadema wamefanya utafiti wa kutosha na kupata majibu ya utafiti wa kampuni kadhaa zinazopata nafasi za usimamizi huru, wamewaambia kwamba wakipata mtu mwenye nguvu kama za Lowassa, watashinda uchaguzi.
Anakiri kwamba kuna wanachama wenye hofu ndani ya Chadema ambako Lissu anatumia nafasi hii kuwatoa hofu akisema, “Kamati Kuu ya chama ina watu wenye maarifa sana. Ina watu wenye kufanya uamuzi mzito baada ya kupokea ushahidi na kuujadili kwa kina. Haikufanya uamuzi rahisi.
“Uamuzi mgumu umefanyika baada ya mjadala mkali na wa muda mrefu. Hakuna kiongozi wa juu wa chama ambaye hakushiriki kwenye process (mchakato huu) hii,. Mwenyekiti na makamu wake wa bara na visiwani, katibu wa chama na wasaidizi wake na wajumbe wa Kamati Kuu. Tumefanya uamuzi si wa kushitukiza.
“Tumefanyia kazi sana kwa siku nyingi. Tulianza siku nyingi. Tulianza kufikiria hiki kinachotokea kwenye CCM maana yake nini? Hizi alama za nyakati zinatuambia nini? Na tujipangaje, kwa hiyo tulifanya tafakuri ya kina,” anasema.
Chadema kwa sasa wako kwenye vikao vya kupitisha jina la Lowassa ambako juzi Jumapili kiliketi kikao cha Kamati Kuu, Baraza Kuu pia liliketi na na leo wanatarajiwa kuendelea na mkutano mkuu.
Lowassa anatarajiwa kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambako Mwenyekiti Mwenza wa umoja huo, James Mbatia, amebainisha kwamba Lowassa akipewa majukumu ataweza.
Kadhalika Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anasema kumekuwepo na propaganda nyingi zikidai kuwa Chadema tunapokea mafisadi, lakini chama hicho kimeangalia mahitaji ya sasa ili kuleta mageuzi ya kweli nchini.
Naye, Profesa Lipumba anasema kwamba anampongeza Lowassa na kwamba anamuunga mkono kwa sababu uzoefu wake tangu aanze kuwania urais 1995, CCM imekuwa “Ikitupindua, lakini mwaka huu kazi imekwisha.”
Aidha wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, wamesifu hatua ya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuamua kuachana na chama chake tawala na kuamua kujiunga na upinzani wakisema ni hatua kubwa na inaonyesha namna siasa za Tanzania zinavyozidi kukua.
Itakumbukwa kwamba kwa Afrika Mashariki, Tanzania na Zimbabwe ndizo zilizokuwa hazijatikiswa kisiasa, lakini historia hiyo imejidhihirisha kwa Tanzania Julai 28, mwaka huu baada ya Lowassa kuandika historia hiyo.
Mchambuzi wa Masuala ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Kitila Mkumbo anasema Lowassa anapaswa kupongezwa kwa hatua aliyofikia kuamua kujiunga na upinzani.
“Kitendo cha waziri mkuu wa zamani na kada wa CCM ambaye kwa kweli hafahamu maisha mengine yeyote zaidi ya kufanya kazi CCM na serikali yake kukuamua kuingi upinzani ni jambo kubwa na kwa kweli haijawahi kutokea na kwa kitendo hiki ni wazi kwamba siasa za Tanzania zimebadilika kwa kiasi kikubwa.
Profesa Mkumbo anasema kwa muda mrefu hasa tangu katika mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1995 ikiwa mgombea atawania urais husubiri kuapishwa kuwa rais hivyo ikiwa atateuliwa kuwania urais kupitia upinzani ni wazi kwamba Dk. John Magufuli (mgombea urais wa CCM) ana kazi kubwa ya kufanya.
Hata hivyo upinzani (Ukawa) hasa Chadema wana kazi kubwa kwa sababu kabla hawajampokea Lowassa siku za nyuma walimchafua kwa kumtupia kashfa nyingi kwamba ni fisadi na hivi sasa wana kazi kubwa ya kuwaeleza wananchi vinginevyo kwamba waliyosema siku zilizopita kuhusu Lowassa hazikuwa za kweli na itategemea wananchi watalipokea vipi.
Profesa Mkumbo amesema pia katika hilo mshindi wa pili ni Chadema, kwa sababu katika hali ya kawaida ingekuwa linazungumzwa kuhusu usajili wa timu ni wazi kwamba hakuna kocha mwenye akili sawa sawa angekataa kumsajili Lowassa.
Pamoja na hilo, Profesa Mkumbo anasema katika hilo Chadema wamesajili mchezaji maarufu ambaye katika hali ya kawaida ingekuwa ngumu kwa kocha mahiri kukataa kumsajili.
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk. Onesmo Kyauke, amesema hatua hiyo imeonyesha namna demokrasia na mfumo wa vyama vingi unavyozidi kukua.
Amesema kwa kitendo cha Lowassa kuamua kujiunga na upinzani umezidi kuvipa nguvu vyama vya upinzani.
Mchambuzi mwingine wa masuala ya Kisiasa Julius Mtatiro amesema hatua ya Lowassa kujiunga na upinzani ni pigo kubwa kwa CCM kwani uondokaji wake umekiacha chama hicho kuwa na tumbo joto.
Kwa mujibu wa Mtatiro ikiwa Lowassa atateuliwa kugombea urais kupitia Ukawa; nchi itarajie kupata kampeni zenye ushindani mkubwa ikizingatiwa kwamba amekuwa na ushawishi mkubwa kwa wananchi.
Amesema pamoja na mambo ambayo Lowassa ametajwa nayo likiwemo la Richomond ambalo ameshalizungumzia hivi karibuni lazima nchi ikubali kwamba Lowassa ni mtu mwenye nguvu hivyo kwa hali hiyo amekiacha CCM katika hali ngumu.
Mtatiro ameongeza kwamba kwa siasa za Tanzania hali inayoonekana kwa sasa ni kwamba hilo ni hitimisho la mpasuko kwa CCM kwani chama hicho hakijaanza kukosolewa leo hivyo hatua ya Lowassa ambaye ni mwanasiasa mwenye nguvu kukihama chama chake ni kiashirikia kikubwa,
Kwa mujibu wa Mtatiro, Lowassa ana nguvu kubwa kwani karibu robo tatu ya wanachama wa CCM wanamuunga mkono.
Taarifa zinasema kwamba kwa sasa Lowassa ana amani moyoni tangu ahamie Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako anatarajiwa kupitishwa kuwania urais.
Watu wa karibu wa mwanasiasa huyo mkongwe, wameliambia JAMHURI kwamba “Hali ya woga na hofu na unyonge kwa Lowassa, imeondoka. Ana amani. Anacheka, anafurahi. Simu za ajabu ajabu na vitisho, hazimgusi tena.”
Mmoja wa wasaidizi hao aliyezungumza na JAMHURI, anasema kwamba mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz alimng’ang’ania Lowassa hadi sekunde ya mwisho kabla ya kwenda Hoteli ya Bahari Beach kutangazwa mwanachama mpya wa Chadema.
“Hadi asubuhi ya Jumanne Lowassa alikuwa na Rostam ambaye wakati wote alimsihi asiondoke CCM, lakini Lowassa alijipima kwa muda mrefu, na kufanya uamuzi alioufanya. Kuondoka CCM,” anasema.