*Taarifa za awali zahusisha kutekwa na urais 2015

*Risasi aliyopigwa ilifumua jicho, ikatokea kisogoni

Tukio la Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, kutekwa, kupigwa, kung’olewa meno, kukatwa kidole na kung’olewa kucha limeanza kuhusishwa na mlengo wa kisiasa.

Taarifa kutoka sehemu mbalimbali zinahusisha tukio hilo na msimamo wa mwanahabari huyo katika siasa za kitaifa.

 

Kibanda anahusishwa moja kwa moja kwenye mtandao wa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kuwa watakiwakilisha kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

 

Wanaofuatilia siasa za kitaifa wanasema kwamba uamuzi wa Kibanda wa kuhama kutoka Kampuni ya Free Media, inayomilikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kwenda New Habari (2006) Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara Rostam Aziz, umelenga kwenda kuimarisha nguvu za Lowassa.

 

Kwa miaka mingi, Lowassa anatajwa kuwa na urafiki wa karibu mno na Rostam. Wawili hao ndiyo waliokuwa vinara wa mtandao uliomwingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005.


Kwa upande wake, JAMHURI imezungumza na Lowassa kuhusu ukaribu wake na Kibanda, na kama kweli hiyo ndiyo sababu ya mwanahabari huyo kujeruhiwa.


Lowassa amesema kwa kifupi, “Jamani, tuna ushahidi gani? Haya ni maisha ya mtu, hata wakubwa tusiwatuhumu hivyo, tuwe na ushahidi tukitaka kutoa tuhuma nzito kama hizi.”

 

Gazeti la Tanzania Daima Jumamosi lilikanusha vikali habari za utekaji wa Kibanda kuhusishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe. Jumamosi hiyo hiyo, zikatokea taarifa zikivishutumu vyombo vya dola kuwa vinahusika na utekaji wa Kibanda. Taarifa hizo zinasema vyombo vya dola viliamua kumshughulikia Kibanda kutokana na msimamo wake juu ya makundi ya urais wakati huu wa kuelekea mwaka 2015.


“Kibanda wanamhusisha na kundi la [Edward] Lowassa. Wanaona Kibanda analipa nguvu kundi hilo kwa kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri na baadhi ya watu ndani ya vyombo hivi wanadhani kuwa Kibanda ana-set (anatengeneza) mazingira ya Lowassa kuwa rais. Hii inawaogofya wenye nia mbaya,” kilisema chanzo chetu.


Mara kadhaa Kibanda ameweka wazi msimamo wake wa kumuunga mkono Lowassa, akisema anastahili kuwa rais wa Tanzania baada ya Kikwete.


Taarifa za madaktari kutoka Afrika Kusini zinasema jicho la kushoto la mwanahabari huyo limeharibiwa kabisa na haliwezi kurejea kwenye hali yake ya kawaida.

 

“Madaktari wamebaini kuwa hakupigwa kwa nondo, bali risasi. Alipigwa risasi usoni, ikatoboa jicho, ikatokea pembeni mwa kichwa. Kitaalamu imeonekana risasi haikulenga nyuzi 180, badala yake ilikwenda nyuzi 45. Ana bahati haikupita katikati ya kichwa,” kilisema chanzo chetu.


Baadhi ya wananchi waliozungumza na JAMHURI wameonyesha hofu ya kutajwa majina gazetini wakihofia maisha yao, lakini wakaomba Serikali ifanye uchunguzi wa kina kubaini iwapo madai kuwa vyombo vyake vinahusika yana ukweli wowote.

Usiku wa kuamkia Machi 6, Kibanda alitekwa akiwa nje ya nyumbani kwake, Mbezi jijini Dar es Salaam.


Mwajiri wake, New Habari (2006) Ltd alimlipia gharama za safari na matibabu katika Hospitali ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

 

Mwishoni mwa wiki alifanyiwa upasuaji wa kurejesha sura katika hali yake, na alikuwa akihudumiwa na madaktari bingwa sita walioanza na kichwa kwanza kabla ya jicho. Kulikuwa na habari kwamba miongoni mwa kazi za madaktari hao ni kuondoa damu iliyovilia katika ubongo. Hali ya Kibanda imeelezwa kuwa inahitaji uangalizi wa karibu.


Katika hatua nyingine, TEF imeunda jopo la waandishi wa habari kwa ajili ya kuchunguza tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Kibanda.


Mashirika, asasi, vyama vya siasa, wadau, wananchi na nchi kadhaa zimejitokeza kulaani tukio hilo. Serikali ya Marekani kupitia kwa Balozi anayeiwakilisha nchi hiyo hapa nchini, Alfonso Lenhardt, imeitaka Serikali ya Tanzania kuhakikisha wote waliohusika kwenye tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

 

Viongozi mbalimbali, wakiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi; Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, ni miongoni mwa viongozi wengi waliokwenda kumjulia hali Kibanda wakati alipolazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI). Rais Kikwete alimjulia hali hospitalini Afrika Kusini.

Maendeleo ya afya ya Kibanda

Taarifa ya karibuni iliyotolewa na Katibu wa TEF, Neville Meena kwa vyombo vya habari inasema, “Nimepokea taarifa kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe kwamba tayari Mwenyekiti wetu, Kibanda ametoka ‘theater’ alikokuwa akifanyiwa upasuaji. Hata hivyo taarifa mbaya ni kwamba madaktari wameshindwa kuokoa jicho lake la kushoto hivyo wameling’oa.


“Wamechukua hatua hiyo ya kitatibu baada ya kuwa tayari jicho hilo lilikuwa limepondeka kwa ndani hivyo lisingeweza tena kuona. Atawekewa jicho la bandia la plastiki ambalo hata hivyo halitakuwa na uwezo wa kuona.


“Jambo la kumshuruku Mungu ni kwamba kwa jumla upasuaji huo uliochukua saa 5 na dakika 30 umefanyika kwa ufanisi mkubwa na ulikuwa ukiongozwa na madaktari bingwa watatu. Wawili kati yao ni wataalamu wa kichwa na mmoja ni mtaalamu wa macho.

“Katika upasuaji huo, hakukuwa na madhara ya ndani katika kichwa chake, hivyo kichwa kiko salama. Sura yake imejengwa upya kutokana na majeraha.


“Changamoto kubwa waliyokutana nayo madaktari waliomfanyia upasuaji ni kurejesha katika sehemu yake baadhi mifumo midogo inayozunguka jicho, pia kurejesha taya la kushoto ambalo lilikuwa limeathiriwa na tukio la kupigwa kwake. Hata hivyo hatimaye walifanikiwa.”


Ripoti kamili kuhusu upasuaji huo inatarajiwa kutolewa Jumapili na madaktari hao.