Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema anakerwa na baadhi ya wanasiasa wanaoeneza maneno ya chuki, kupalilia uhasama na kumtupia lawama zisizomhusu Rais Samia Suluhu Hassan.
Kutokana na mwenendo huo, amewataka wajue kuwa wanashiriki kutenda dhambi huku wakimkosea heshima kwa kuwa hawapaswi na wala hawalazimiki kumbebesha shutuma za aina yoyote.
Msimamo huo ameutoa wiki iliyopita katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika ofisini kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam.
“Rais wetu Mama Samia amefanikiwa kulirejesha taifa letu katika reli yake ya asili iliyopitwa na watangulizi wake. Nina hakika amelipatia taifa heshima ya juu na kuibakisha nchi yetu katika ramani ya dunia ya mapatano, utangamano, ushirikiano na maelewano thabiti,” anasema Lowassa.
Katika hatua nyingine, Lowassa, amempongeza na kumshukuru Rais Samia kwa kujiandaa kwake vema kifikra, kivitendo na kimkakati kuliongoza taifa kuchapa kazi na kujiamini.
Anasema Rais Samia amemudu kutandika zulia kwa mapatano ya ndani, kikanda na kimataifa, hivyo hapaswi kutiliwa shaka na yeyote ili kuviza dhamira ya kuliongoza taifa na kulijenga kiuchumi.
Pia anasema katika kipindi kifupi alichoshika madaraka, Rais Samia amefanikiwa kujijengea imani katika taasisi, mashirika, jumuiya za kimataifa na nchi washirika wa maendeleo, huku akiishirikisha vema sekta binafsi kuelekea ujenzi wa uchumi imara, hivyo watu wote hawana budi kumuunga mkono na kumsaidia kwa nguvu zote, kufa na kupona.
“Uongozi mpya wa Rais Samia ni mithili ya nyota ya jaha. Uongozi wake umepambwa kwa nuru njema na mwanga unaotoa matumaini ya kufikia kilele cha maendeleo ya kweli. Wenzake waliopita wamekwisha kutimiza wajibu wao na yeye aachwe atekeleze mikakati ya kisera katika serikali yake,” anasema.
Lowassa anasema hatua ya Rais Samia kukutana na wakuu wa nchi, viongozi na watendaji wakuu wa mashrika ya kimataifa na wafanya biashara ni dhahiri ameshika turufu katikati ya jozi ya karata za kiutawala, amekubalika na kuwavutia wawekezaji.
Anasema ahadi zake mbele ya Baraza Kuu la 76 la Umoja wa Mataifa (UNGA) za kuendelea kulinda amani, usalama wa ndani, kikanda kwa kushirikiana na mataifa yote ulimwenguni ni matamshi yaliyosababisha msisimko na kuwa gumzo ulimwenguni kote.
“Rais Samia amekutana na baadhi ya marais wa nchi mbalimbali, wakuu na watendaji wa mashrika na taasisi za kimataifa likiwamo Shirika la Fedha Duniani (IMF), Shirika la Biashara Duniani (WTO), wakuu wa Umoja wa Ulaya (EU). Si vikao mzaha. Rais amejipanga kuliongoza taifa kwa maendeleo ya kweli,” anasema.
Lowassa anasema ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania si kisiwa, hivyo inabidi ishiriki katika majadiliano na kuendeleza ushirikiano ili kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa kushughulikia masuala mtambuka yanayoambatana na uchumi na kijamii, ikiwamo kujadili ajenda za mlipuko wa virusi vya Uviko-19, mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya kidijitali, sayansi na teknolojia.
Pia anasema Rais Samia amethibitisha bila shaka yoyote kuwa Tanzania imepata nyota ya uongozi, kwa kuwa na mkuu wa dola mwanamke, hodari na shupavu, ambaye leo hii kuna kila sababu ya kujivunia na kumuunga mkono.