Mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) anayewakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa, sasa ameamua kutumia helikopta tano katika kampeni zake.
Uamuzi huo unalenga kuimarisha kampeni zake ikiwa ni takribani mwezi mmoja kabla ya siku ya upigaji kura za Uchaguzi Mkuu ifikapo Oktoba 25.
Matumizi ya helikopta hizo yatakayoanza Oktoba Mosi, yameelezwa kwamba yamelenga kumwezesha Lowassa, mgombea mwenza, Juma Duni Haji, na makada wengine kuweza kufanya mikutano mingi kabla ya siku ya mwisho ya kampeni ambayo ni Oktoba 24.
Wakati Ukawa wakijiandaa hivyo, upande wa Chama Cha Mapinduzin (CCM), mgombea wake amekuwa akitumia magari, akisema hiyo ndiyo mbinu nzuri ya kuwafikia wananchi na kuyaona matatizo yanayowakabili ili ajiandae kuyaondoa.
Kwa siku za karibuni, kumekuwapo picha kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha helikopta inayonakishiwa picha za mgombea urais kupitia CCM, Dk. Magufuli, ikiwa ni maandalizi ya kuanza kutumiwa naye katika mikutano mbalimbali.
Habari kutoka ndani hya UKAWA zimesema kambi hiyo itagawanyika katika vikosi-kazi vitano kwa ajili ya “kushambulia” kanda za Kusini, Kati, Kaskazini, Magharibi na Mashariki.
Kanda ya Kusini ina mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Songwe na Mbeya. Kanda ya Kati ina Dodoma, Singida, Tabora na Simiyu.
Kanda ya Magharibi ina mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Kagera, Geita, Kigoma, Katavi na Rukwa.
Kanda ya Kaskazini inajumuisha mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro; wakati Kanda ya Mashariki ina Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na Zanzibar.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema: “Itakuwa ni kama tunaanza kampeni. Lowassa alikuwa hajaanza kampeni, alikuwa anatambulishwa tu kwa wananchi, hivyo sasa ndiyo anataka kuanza kampeni ambazo zitakuwa ni kampeni za historia, tumejipanga ipasavyo.”
Mbowe ameongeza: “Tupo vitani. Tupo katika vita ya kumkomboa mwananchi na ukandamizaji uliofanywa na Chama Cha Mapinduzi, sasa kwangu ni vigumu kuelezea mikakati yetu yote ya kivita kwa wakati huu.”
Mbowe anasema kuwa kwa wakati huu kila upande una mbinu zake za ushindi, na Ukawa wamejipanga kuhakikisha wanashinda Uchaguzi Mkuu, lakini hawezi kutoa siri ya mikakati hiyo hadharani.
“Mbinu za ushindi hazitolewi hadharani, huo ni mkakati wa kivita hauwezi kuuelezea maana mshindani wako anaweza kupata faida ya kubainishwa kwake, wewe subiri utaona mambo yatakavyokuwa,” amesema Mbowe.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, anasema mbinu za kuendesha kampeni zinabadilika kutokana na wakati.
Anasema kuwa kadiri siku zinavyozidi kusonga na uchaguzi kukaribia, Ukawa wamejipanga kubadili mbinu, na kwamba suala la kuongeza helikopta ni moja ya mikakati ya ushindi.
Wakati Ukawa wakijipanga kubadilisha mbinu za kampeni, JAMHURI limedokezwa kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa anatarajiwa kurudi nchini wiki ijayo na kufanya mkutano na waandishi wa habari.
Taarifa zinasema Dk. Slaa atatolea ufafanuzi baadhi ya mambo. Kuna habari kwamba huenda akarejea kwenye siasa kwa kumnadi mmoja wa wagombea urais.
Kwa upande wake, Mbowe anasema kuwa suala la Dk. Slaa kumfanyia Dk. Magufuli kampeni ni la binafsi na wala haliwezi kuiathiri Ukawa maana si mwanachama wa Chadema.
Anasema ana uhuru wa kufanya chochote akitakacho maana alishajiondoa Chadema kwa utaratibu alioutaka yeye.
Wakati huo huo, Mwandishi Clement Magembe, anaripoti kuwa Lowassa kwa mara nyingine amezungumza hadharani kuhusu kashfa ya zabuni ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, akisema: “Sina muda tena kuwajibu.”
Lowassa anasema anatambua matatizo ya Watanzania, hivyo anaona ni bora kwa muda huu mfupi wa kampeni anaowafikia wananchi akafafanua sera za Ukawa badala ya kujibizana kwa jambo ambalo amekwishalifafanua.
Lowassa anakwenda mbali akisema anayedhani kwamba ana ushahidi wa yeye kuhusika na Richmond, basi apeleke shauri hilo mahakamani ili mhimili huo utende haki.
Julai 28, mwaka huu alipotangaza kung’oka CCM na kujiunga Chadema, Lowassa aling’aka akiwaambia waandishi wa habari kwamba hahusiki na Richmond, ispokuwa mamlaka ya juu ndiyo ilihusika.
Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu ameshaseama mhusika wa kampuni hiyo ni Rais Jakaya Kikwete. Ikulu haijakanusha tuhuma hizo.
Lowassa anayetokana na Chadema, anagombea urais akiungwa mkono na Ukawa unaoundwa na vyama vya National League fore Democracy (NLD), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Lowassa alipata kulisema suala la Richmond kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichoketi Novemba, 2011 baada ya kushutumiwa na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM kuwa ni fisadi.
“Sitawajibu. Sina muda wa kuwajibu. Kama wanataka majibu wasubiri Oktoba 25.”
Waziri wa Afrika Mashariki anayewania ubunge Jimbo la Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, Agosti 29, mwaka huu alisema moto wa Richmond haujazimika, na kwamba Lowassa anaweza kufunguliwa kesi.
Dk. Mwakyembe aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata hilo alilieleza Bunge kuwa haikusoma taarifa kamili ya suala hilo kwa hofu kuwa Serikali nzima ingeanguka.
Rais Jakaya Kikwete ameshaeleza kushangazwa kwake na Lissu kumsakama kwenye majukwaa ya kisiasa kuhusu Richmond, na akamtaka amtaje mhusika wa Richmond ambaye alisema anatembea naye mikoani.
“Endapo Tundu Lissu atashindwa kumtaja mwenye Richmond, nitatoka hadharani na kumtaja mwenyewe,” amesema Rais Kikwete kwa kujiamini.
Kusikia hivyo, Lissu alijitokeza na kusisitiza kuwa mhusika mkuu wa Richmond ni Rais Kikwete.
Anasema baada ya Lowassa kujiuzulu mwaka 2008, mashine za kufua umeme zilishafika nchini na baada ya kujiuzulu haikufahamika zilikokwenda; na kwamba baadaye mkataba wa Richmond ukahamishiwa kwa kampuni ya Dowans ambayo iliendelea kulipwa mabilioni ya shilingi.
“Rais Kikwete awaambie Watanzania kwa nini Serikali yake iliendelea kuilipa Dowans mabilioni ambayo ilikuwa ya mfukoni na kama Lowassa alifanya makosa kwa nini hajapelekwa mahakamani kwa miaka minane tangu ajiuzulu?” Amehoji.
Katika mahojiano na gazeti hili, Lissu anasisitiza ugumu wa mkataba wa Richmond uliogharimu Uwaziri Mkuu wa Lowassa kushirikisha kiongozi mmoja tu katika mfumo wa uongozi.
“Kashfa ile kubwa haiwezekani kumhusisha Lowassa peke yake,” anasema Lissu na kuongeza: “Lowassa ametoa majibu, amesema kilipoanza kunuka aliwaambia makatibu wakuu…jamani eeeh tuvunje huu mkataba, lakini bwana mkubwa (Rais) akakataa.”
Akizungiumzia sakata hilo, Mbowe anasema kinachofanyika sasa ni kuendekeza makundi na vita vya kisiasa ndani ya CCM na Serikali yake na kuligharimu taifa hili Sh bilioni 120.
Mbowe anasema iwapo ukweli hautawekwa bayana, huko mbele jambo hilo litaligharimu Taifa mabilioni ya fedha ambayo yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki vingetawala katika mchakato mzima wa kashfa ya Richmond.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba amesema wakati ripoti ya Richmond ikisomwa, hakukuwa na hukumu na badala yake Waziri Mkuu wa kipindi hicho aliambiwa ajipime na kujitathimini, hivyo akajiuzulu.