Lowassa copy.

Machinga wamkabidhi Sh milioni 1, zana za kazi
.Wakulima wa Tanga
nao wamwagia Sh. 200,000
.Madiwani Bariadi wafunga safari kwenda Monduli
.Mwenyewe azungumza mazito kwenye waraka

 
Wakati makada sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiendelea kufungwa kwenye adhabu ya kuchunguzwa, Edward Lowassa amebanwa na mashabiki wake wanaomtaka atangaze haraka nia ya kuwania urais.
Wanachama hao wanamtaka amalizie kazi ya kutangaza nia, lakini yeye ameshikilia msimamo wake wa kutofanya hivyo akitoa sababu mbili; mosi ni kiapo cha uongozi; na pili ni kuheshimu maagizo ya chama.
Makundi ya wafuasi wake kutoka sehemu mbalimbali nchini yamemfuata na kumkabidhi Lowassa fedha wakisema wanataka muda wa kuchukua fomu ukiwadia, asikwame wala kusita kufanya hivyo.
Wafuasi wake wamekuwa wakimiminika nyumbani kwake Monduli, na Dar es Salaam kumkabidhi fedha hizo.
Aboubakary Liongo – Msemaji wa Lowassa, amethibitishia kumiminika kwa michango hiyo na kwamba imekuwa vigumu kwa wasaidizi wa Waziri Mkuu huyo wa zamani kuzuia watu kufanya kile walichodhamiria.
Liongo anasema kwamba Jumamosi iliyopita waliibuka viongozi wa Serikali, Chama Cha Mapinduzi na jamii ya wafugaji kutoka Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga ambako pamoja na mambo mengine, walimkabidhi Lowassa Sh 200,000.
“Ni kweli viongozi hao walikuja nyumbani kwa Mheshimiwa Lowassa, Monduli kumshawishi kuwania urais kupitia CCM,” anasema Liongo katika mahojiano na Gazeti la JAMHURI.
Anataja kundi jingine kuwa ni la Umoja wa Wamachinga Tanzania (SHIUMA) waliomkabidhi Lowassa mchango wao wa Sh. milioni moja ili azitumie kuchukua fomu.
Viongozi wa SHIUMA, pamoja na viongozi wa UVCCM kata za Jiji la Mwanza walikwenda nyumbani kwa Lowassa; Ngarash, Monduli mwishoni mwa wiki, kumshawishi agombee urais.
Kwa mujibu wa Liongo, Lowassa alikabidhiwa ngao na mkuki avitumie kwenye safari yake ya matumaini. Aliyekabidhi vifaa hivyo ni Mwenyekiti wa SHIUMA, Matondo Masanja.
Mbali ya ya viongozi hao, kuna kuna baadhi ya wabunge ambao tayari wameshajitokeza kumshinikiza Lowassa atangaze nia ya kuwania urais. Wiki kadhaa zilizopita, wabunge hao walikutana na kutangaza hadharani kumuunga mkono.
Kundi jingine lililojitokeza kumtaka atangaze nia ni la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu ambao wametangaza wazi kwamba wanamuunga mkono kwa maelezo kwamba ni mchapakazi asiyebembeleza watumishi wasiowajibika.
Madiwani hao walijitokeza wakati wa kikao cha Baraza la Halmashauri hiyo kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini Bariadi.
Wakasema wanatamani Lowassa angerudi kuongoza nchi kwa sababu alipokuwa Waziri Mkuu aliwawajibisha watumishi wazembe.
Diwani wa Kata ya Guduwi, Yohana Muyumba anasema kwamba hakuna kiongozi aliyekuwa anachukua uamuzi wa papo kwa papo kwa kuwawajibisha wanaofuja mali za umma, hasa watumishi wanaokwenda kinyume cha taratibu za kazi.
“Natamani Lowassa angerudi katika kuongoza nchi hii kwani kipindi cha uwaziri mkuu wake nchi hii aliinyoosha; hasa katika upande wa watumishi alikuwa akiwawajibisha lakini kwa sasa tunawalea,” anasema.
Muyumba anasisitiza kwamba kungekuwa na viongozi kama Lowassa, suala la ufisadi mkubwa unaosikika sasa lisingekuwapo huku akieleza kuwa kiongozi huyo anaweza kusimamia miradi ya maendeleo nchini ikiwamo na kuwaajibisha wanaokwenda kinyume katika kutekeleza majukumu yao.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Robart Lweyo anasema kuwa viongozi wameshindwa kusimamia miradi ya maendeleo na ndio maana madiwani wamekumbuka Lowassa jinsi alivyosimamia watumishi katika idara zote.
“Wataalamu wetu wanashindwa kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali iliyopo katika Halmashauri yetu na ndio maana miradi mingi inaharibika kutokana na viongozi wetu kutokwenda kufuatilia miradi hiyo,” anasema.
Viongozi hao ni mweendelezo wa idadi ya watu wanaojitokeza kumtaka Lowassa awanie urais.
Wiki iliyopita, Lowassa aliandika waraka akimlilia Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, akisema amefariki kabla ya kumpa jibu kama atawania urais au la.
Viongozi wa kitaifa wa CCM wamekuwa wakitoa kauli zenye kuashiria kuwa hata adhabu ya kuchunguza makada wake ni geresha na hali ya kutuliza mambo ndani ya chama kwa sasa.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amemsifu Lowassa akisema ni mchapakazi na kiongozi shupavu. Kauli hiyo ya Kinana aliitoa muda mfupi baada ya kuwasili Monduli akiwa kwenye ziara ya kuimarisha chama.
Kinana anamsifu Lowassa kwa kutekeleza kwa ukamilifu ilani ya chama hicho wilayani Monduli; na kwamba anastaafu ubunge wake mwaka huu kwa heshima kubwa.
“Napenda kumpongeza Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu mstaafu ndugu yangu, Edward Lowassa kwa Kazi kubwa ya maendeleo aliyoifanya katika jimbo hili…maendeleo yote hapa hayakosi mkono wa Lowassa,” anasema Kinana wakati yeye na msafara wake alipopokewa  katika Kata ya Makuyuni mwanzoni mwa ziara yake ya siku tisa mkoani Arusha.
Akaongeza: “Ndugu Lowassa ameamua kustaafu ubunge, anaondoka kwa heshima kubwa… tunakushukuru sana ndugu Lowassa.”
Anasema kwamba kutokana na utekelezaji madhubuti wa Ilani ya uchaguzi ya CCM, Jimbo la Monduli ni ngome ya CCM. “Na ukitaka kujua ngome za CCM njoo hapa Monduli…ndugu yangu Lowassa amefanya kazi kubwa sana, mafanikio haya yote… hospitali ya kisasa, maji, umeme na shule ni juhudi za ndugu Lowassa," amesema Kinana.
Kwa upande wake, Lowassa anasema kama wabunge wote wa CCM wangetekeleza vyema ilani ya uchaguzi, chama hicho kingekuwa na kazi nyepesi ya kushinda uchaguzi wote.
“Ndugu katibu mkuu tunafurahi kuja Loksale na kutembelea wilaya yetu kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, Monduli tunaweza tukajivuna tukasema tumefanya vizuri sana… Nape hapa huna kazi, kazi tumeshamaliza…Hapa uchaguzi wa Serikali za Mitaa tumepata asilimia mia moja,” anatamba Lowassa.
Lowassa anasema alifundishwa mambo mawili na Kinana wakati walipokuwa mawaziri kwenye Serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Mambo hayo ni kutolitelekeza jimbo na kuweka alama nzuri ya kukumbukwa.
“Abdul (Kinana) unakumbuka tulipokuwa mawaziri chini ya Mzee Mwinyi? Uliwahi kuja Monduli na kuhutubia mkutano pale… ukasema rafiki yangu wakaanza kusema huonekani! Ujue ubunge umekwenda na maji,” akasema na kuwauliza wananchi  kama ameonekana au hakuonekana, na wananchi walipaza sauti kwa kusema: "umeonekana.”
Anasema jambo la pili alilofundishwa na Kinana ni kuacha kumbukumbu nzuri ‘legacy' na kusema hilo pia amelifanya kwa kuitekeleza kikamilifu Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo ni kuondoa kero na kuleta maendeleo.
“Hilo pia alinifundisha Abdul, ni rafiki yangu sana, na kweli nimelifanya tumejenga barabara, miradi ya maji na hospitali, lakini namshukuru kwa namna ya kipekee kabisa Mwenyekiti wetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais Kikwete…Rais Jakaya Kikwete katika kila mradi tuliyoufanya Monduli ametusaidia sana,” anasema Lowassa.
Wiki iliyopita akiwa mkoani Dodoma, Kinana alisema kwamba chama hakitaingia kwenye mgogoro wa kukata majina ya makada wanaokubalika kuwania uongozi wa ngazi zote kuanzia udiwani, ubunge na urais.
Mbali ya Kinana, pia wamo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Hamisi ambaye katika vikao vya ndani vya Umoja huo, vikao vya chama na mikutano ya hadhara ikiwamo ile ya kuwakabidhi madaraka makamanda wa vijana, amekuwa akisisitiza kutokatwa jina la mwanachama katika vikao vya uteuzi vya chama.
Mathalani, katika mkutano wa kumweka madarakani Kamanda wa Vijana Mkoa wa Tanga, Sadifa alisisitiza: “Safari hii, hakatwi mtu. Hakuna jina la mtu litakalokatwa.”
Kauli hizi zimekuja huku kukiwa na tetesi za kukatwa kwa majina ya baadhi ya wanachama kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuanza kampeni mapema.
Mbali ya Lowassa, makada wengine wanaotumikia adhabu hiyo ni Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba; na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kwenye waraka wake, Lowassa anamlilia Komba aliyefariki dunia Februari 28, mwaka huu kwamba alikuwa ‘muumini asiyeyumba wa Safari ya Matumaini.’
Komba aliyezikwa kijijini kwao Lituhi Nyasa, Machi 3, mwaka huu alifikwa na mauti  akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam kutokana na kusumbuliwa na shinikizo la damu na kisukari
Katika waraka huo, Lowassa anasema: “Hivi ni kweli sitosikia tena sauti yako Kapteni Komba! Mbona umeondoka bila ya kuniaga ndugu yangu! Moyo wangu unabubujika machozi ya damu.
“Maneno yako kwa mmoja wa wasaidizi wangu siku tatu kabla ya umauti kukupata kwamba ‘Mwambie Edward akija aje kuniona, mimi sijisikii vizuri’ yanazunguka akilini mwangu.
“Kapteni Komba, mimi na wewe tumepigana vita nyingi kwa maslahi ya chama na nchi yetu…na tulishinda vita hivyo. Lakini bado tulikuwa tunaendelea na mapambano ya kumnasua Mtanzania katika umaskini.
“Komba ulikuwa muumini usiyeyumba wa ‘Safari ya Matumaini’. Ulikuwa mmoja wa makamanda wa kuongoza harakati za kunishawishi niwanie urais kupitia chama chetu.
“Ulipaza sauti bila woga kuelezea imani yako kwangu. Kapteni, naumia sana umeondoka bila ya kukupa jibu la kukubaliana na ushawishi wako au la.
“Kwa hakika chama kimepata pigo. Ni nani asiyejua mchango wako katika ushindi wa chama chetu katika ngazi zote. Nyimbo zako ndiyo adhana au kengele ya kuwakusanya waumini (wana CCM na wananchi) katika mikutano ya chama. Komba ulikuwa nembo ya chama chetu.
“Komba umeondoka, lakini umeacha alama katika ulimwengu wa siasa hususan katika chama chetu. Daima nitakukumbuka ndugu yangu, naamini kabisa yale mapambano utayaendeleza huko ulikoenda ambako sote tutakuja.
“Nakuahidi ndugu yangu, kama tulivyokuwa pamoja katika matatizo na furaha zetu, mimi na chama chetu tutaendeleza pale ulipoachia kutatua matatizo ya familia.
“Namuomba Mungu anipe nguvu na moyo wa kuyafanya hayo. Pumzika kwa amani rafiki yangu, ipo siku isiyo na jina tutaonana.”