Polisi wa eneo la Merseyside, Uingereza wamesema wanafahamu kuhusu vitisho vya maisha ambavyo vimetolewa dhidi ya mlinda lango wa Liverpool Loris Karius baada ya kuchezwa kwa fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Jumamosi.

Maafisa wamesema vitisho vyovyote vinavyotolewa kupitia mitandao ya kijamii vinafaa kuchunguzwa.

Karius, 24, na familia yake wamekuwa wakipokea vitisho baada ya makosa mawili kutoka kwake kuwasaidia Real Madrid kupata ushindi wa 3-1.

“Tunachukulia ujumbe huu wa vitisho kwenye mitandao ya kijamii kwa uzito sana. Visa hivi vitachunguzwa,” polisi wamesema.

“Maafisa wa polisi wanafahamu kuhusu ujumbe kadha na vitisho vilivyotolewa kupitia mitandao ya kijamii.

“Polisi wa Merseyside wangependa kuwakumbusha wanaotumia mitandao ya kijamii kwamba makosa yooyte yakiwemo kutoa mawasiliano yenye hila na kutumia vitisho, haya yote yatachunguzwa.”

Mjerumani huyo alimpa mshambuliaji wa Real Madrid Karim Benzema bao rahisi la kwanza mjini Kiev.

Baadaye, alimruhusu Gareth Bale kufunga bao la tatu la Real kutoka mbali alipojaribu kuzuia kombora lake lakini likapita mikono yake na kutumbukia wavuni.

Hilo liliwawezesha Real kushinda taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya tatu mtawalia.

Baada ya kipenda cha mwisho kupulizwa, mlinda lango huyo alionekana kusikitika na kutokwa na machozi.

Baadaye, aliwaomba radhi mashabiki wa klabu hiyo ya Anfield.