NGORONGORO
Na Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema mvutano uliopo Pori Tengefu la Loliondo mkoani Arusha kati ya serikali na baadhi ya wananchi wanaoungwa mkono na asasi zisizo za kiraia, una vimelea vya uchochezi kutoka kwa raia wa kigeni.
Amewataka raia hao wa kigeni wanaokuja nchini kuishi wafuate na kuheshimu sheria za nchi.
Ingawa hakutaja uraia wao, lakini kwa muda mrefu Wakenya wamekuwa wakitajwa na vyombo vya habari kwamba wako mbele katika mgogoro huo.
Katika Kijiji cha Kirtalo, tayari kumebainika kuwapo kwa boma la mwanasiasa mmoja wa Kenya ambaye amekuwa mstari wa mbele kuishambulia Serikali ya Tanzania kwa hatua zake za kuinusuru ikolojia ya Serengeti ambayo kitovu chake kipo Loliondo.
Sambamba na hao, kuna wanasiasa Watanzania wanaohaha huku na kule kupinga uamuzi wa serikali. Miongoni mwao ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, mbunge mstaafu wa moja ya majimbo mkoani Arusha, na asasi za kiraia.
Wanataka eneo la kilomita za mraba 1,500 zilizotengwa liwe chini ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMA) ili wawe na fursa ya kufaidika moja kwa moja, badala ya sasa ambako fedha nyingi zinakwenda Serikali Kuu.
Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza Pori Tengefu la Pololeti (kilomita za mraba 1,500) ambalo ni sehemu iliyotengwa kutoka Pori Tengefu la Loliondo (kilomita za mraba 4,000) lipewe ulinzi muda wote ili kuhakikisha rasilimali zilizomo zinalindwa kwa manufaa mapana ya nchi.
“Vigingi tumekamilisha, lakini kazi nyingine bado zinaendelea. Juni 22, 2022 Amiri Jeshi Mkuu baada ya kuwasilisha taarifa ya kazi hii na kwamba uwekaji wa vigingi umekamilika.
“Lakini pengine bado vibichi na vinahitaji kulindwa pia, alitamka pale hadharani kwamba ulinzi kwenye eneo hili utaendelea, yaani si kwamba mtakapoondoka patabaki wazi, hapana. Lazima wajue eneo hili linalindwa vilevile,”
amesema.
Majaliwa ametangaza msimamo huo alipozuru eneo la uwekaji vigingi unaofanywa chini ya uangalizi na uratibu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana, amemweleza Majaliwa: “Tulikuwa tunatakiwa kujenga beacons (vigingi) 424. Kazi mliyotutuma chini ya uongozi wako na uratibu wa ofisi yako imekamilika. Tunashukuru vikosi vyote
ambavyo vilikuwa hapa – mmefanya kazi usiku na mchana kwa ‘kujitoa’. Tumeshuhudia uzalendo wa hali ya juu.
“Sisi Wizara ya Maliasili na Utalii tunasema hizi maliasili tumerithishwa na sisi lazima tuwarithishe wengine. Eneo hili ni la vyanzo vya maji, ni eneo muhimu la mazalia ya nyumbu na wanyama wengine. Hili eneo ni kiini na ni wajibu wetu
kulilinda.”
Kuhusu utunzaji wa eneo hilo, Dk. Chana, amesema: “Tumeshapitisha GN (Tangazo la Serikali) sasa litaitwa Pori Tengefu la Pololeti – lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500. Tunazilinda hizi kwa kuweka beacons; na zile 2,500 zimeachwa kwa wananchi. Hizi zimelindwa kwa faida ya Watanzania wote. Vyanzo vya maji haya vinasaidia maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na Hifadhi ya Serengeti na tunafahamu Serengeti imepewa tuzo miaka mitatu mfululizo – hiyo yote ni kutokana na vyanzo vya maji vinavyotoka huku.”
Waandishi wa habari wa Gazeti la JAMHURI wamefika eneo hilo na kujionea kazi kubwa iliyofanywa na vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na taasisi nyingine za ulinzi na usalama. Tayari barabara yenye urefu wa kilomita 108 imelimwa kando ya vigingi hivyo – ikitenganisha eneo hilo na lile lilioachwa kwa wananchi.
“Na sasa tunaweka njia ili wajue vizuri, kwa sababu vigingi hivi tumeweka umbali wa mita 250 hadi 300, kwa hiyo ukikaribia kigingi barabara hii itakuonyesha,” amesema Majaliwa.
Askari Polisi Garlius Mwita, aliyeuawa kwa mshale wakati wa maandalizi ya uwekaji vigingi, atajengewa mnara kwenye kigingi namba moja kama ishara ya kumkumbuka.
JAMHURI kimeshuhudia baadhi ya maboma yakiwa hayana wafugaji; hali inayoelezwa kuwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo walikuwa ni raia kutoka nchi jirani, ambao wamerejea kwao baada ya dhamira ya serikali ya kulihifadhi eneo hilo.
Kwa miaka mingi gazeti hili limekuwa likichapisha taarifa na orodha ya majina ya watu wasio raia waliojipenyeza Loliondo na kuwa chachu ya migogoro ya mara kwa mara.
Kwa kawaida maelfu ya mifugo huonekana malishoni katika Kijiji cha Ololosokwan, na kando ya Mto Pololeti, lakini sasa uwanda huo umepambwa na makundi makubwa ya wanyamapori.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Majaliwa, amelaani upotoshaji wa kwamba serikali inawaondoa wananchi wa Loliondo katika ardhi yao.
“Tarafa ya Loliondo kuna vijiji 14, vinaanzia huko mbele (mashariki), hapa tulipo ni msituni, na mimi nimepita kwa helikopta, marubani wamenisaidia sana kuona jiografia. Wamepita kijiji cha mwisho na tukaanza kuingia huku porini – kutoka huko hadi hapa ni kilomita 12 hadi 15 na ndiyo maana tumeshindwa kuwapata wenyeji, maana hauwezi kutembea kutoka kule hadi hapa.
“Ni mbali. Hapa ni kati ya kilomita nne hadi tano kutoka kwenye mpaka wa majirani zetu (Kenya), eneo hili lina umuhimu mkubwa kwetu Watanzania. Umuhimu wa hapa si Tanzania tu, bali ni pamoja na nchi jirani ya Kenya. Umuhimu wa eneo hili ni kutokana na hii tunu tuliyopewa na Mungu ya kuwa na wanyama wa aina mbalimbali ambao wamekuwa kivutio duniani, na wanapenda kuja huku kuona wanyama, na wanyama hao wamejitengenezea mzunguko muhimu sana kwa shughuli zetu za utalii.
“Mzunguko huu unaanzia eneo hili – eneo hili ndiko wanyama hawa wanakuja wanazalia, wanaongezeka halafu wanaanza mzunguko wanaingia Serengeti, wanakwenda hadi Mara – wilaya za Serengeti, Bunda wanazunguka wanapandisha nchi jirani, wanakaa eneo linaitwa Masai Mara, wanazunguka wanapita hapa. Eneo hili (umuhimu wake) si kwa Tanzania tu, hata nchi jirani ya Kenya ni muhimu,” amesema.
Ifuatayo ni sehemu ya hotuba ya Majaliwa neon kwa neno: Tunapoanza mkakati wa kulihifadhi tunatarajia pia na wenzetu (majirani) watakuwa wanatuunga mkono. Wasipotuunga mkono eneo hili likifa hakuna utalii hata huko, kwa sababu hawa wanyama hawatazunguka kwenda huko. Na kama mkakati huu ni wa pamoja, tutaendelea kulilinda eneo hili kwa pamoja na kwa sababu sisi ni nchi jirani, nchi marafiki, nchi ambazo tunaishi kama ndugu – kaka na dada – naamini wataendelea
kutuunga mkono katika hili.
Eneo hili liko mbali sana na makazi ya Watanzania. Tuna vijiji 14, lakini viko mbali mno – makamanda walio hapa kazi yao ilikuwa kuja kujenga tu na kusimamia usalama wa wanaojenga. Hawakuja hapa kuwafukuza Watanzania. Tuwashukuru kazi hii ya kuweka vigingi 424 imekamilika.
Watu wanachanganya haya matukio mawili ya hapa Loliondo na kule Ngorongoro. Wanayachanganya. Hapa tulipo ni eneo la mazalia ya wanyama lililopo Loliondo na kazi ya hapa ni kuweka vigingi tu ili ikitokea yeyote – Mtanzania au jirani huku ajue eneo hili halipaswi kufanya haya…kwa sababu bado kuna maeneo mengi ya kutosha ya kufanya shughuli hizo.
Hayo yanayozungumzwa ndani na nje ya nchi Watanzania wanapima na sasa wanaanza kutambua ukweli. Kwenye kundi la watu 1,000 huwezi kukosa watu watano wanaobisha tu, hata ukiwa na yai ukaliweka hapo ukasema hili ni yai watasema hili si yai, basi atasema si yai, lakini ni yai. Hao wapo. Endeleeni kuwasikiliza, lakini msitilie maanani wanayozungumza kwa sababu wanapotosha, wanadanganya.
Tanzania tuna sheria, ni nchi huru, inajiwekea taratibu zake. Tuna sheria zetu na tamaduni zetu na watu wetu, na ndivyo tunavyoishi. Nawasihi Watanzania wenzangu tuzingatie sheria zetu tulizoziweka wenyewe.
Kila nchi ina utamaduni wake. Hata kama wewe unatamani kwenda nchi hiyo, basi utalazimika kwenda kufuata sheria za nchi hiyo. Usiende na sheria zako huko.
Hata Watanzania mkitamani kwenda kwenye nchi zilizopakana na sisi – sisi tumepakana na nchi saba – naomba niwasihi unapotamani kwenda nchi yoyote, basi uwe tayari kwenda kufuata sheria za nchi hiyo.
Uzuri majirani zetu tumeunda ile Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki – tumepunguza punguza masharti kadhaa, basi ni muhimu ukayajua masharti hayo yaliyopunguzwa ili uyafuate hayo.
Kwa kufanya hilo ndiyo maana Tanzania leo tunaendelea kubaki salama, na Tanzania imekuwa kimbilio la waliopoteza amani kwenye maeneo yao kwa sababu tunazingatia sheria. Tuendelee kuzingatia sheria zetu.
Tanzania tuna marafiki wengi, basi mnapokuja Tanzania muendelee kufuata sheria za nchi kama ambavyo Watanzania wanavyoishi kwa kufuata sheria za nchi.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa (John Mongella) pongezi kwa kazi nzuri uliyoifanya ya kuratibu ‘zoezi’ hili chini ya usimamizi wako na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huu na hii ya Wilaya wenyeji Ngorongoro.
Kwa kweli niwapongeze sana. Mmeratibu kwa weledi mkubwa bila athari yoyote, ukiondoa athari iliyojitokeza ambayo wasiopenda maendeleo ya nchi yetu wamesababisha kifo cha kamanda wetu, lakini vinginevyo katika utekelezaji wa ‘zoezi’ la Loliondo limekwenda vizuri sana. Hongera sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa.
Wanahabari tunawapongeza sana. Mmejitahidi sana kueleza nini kinachoendelea Loliondo, nia ya serikali ninyi mmeieleza vizuri sana na mnaendelea kuieleza. Endeleeni kuieleza.
Endeleeni kuelimisha watu, na wala hatuhitaji kurudiarudia kutamka ukabila. Sisi wote ni Watanzania, nani anakaa wapi, anahamia wapi, ni kitu cha kawaida kwa Watanzania.
Ngorongoro kwa bahati nzuri watu wameelewa, wenyewe wameelewa. Wanajitokeza wenyewe, wanajiandikisha na sasa wameshafikia 1,497 na bado wanaendelea kujiandikisha, na nina shaka serikali tutakuja kuzidiwa. Leo nimeaga Ngorongoro kaya 27 zenye watu 117 tayari wameondoka na mimi nimewaaga wanakwenda Msomera.
Tumebeba mizigo yao kwenye malori maalumu, wenyewe wameingia kwenye magari maalumu ya abiria, mifugo kwenye malori maalumu na anayetaka kuondoka na vifaa vyake kwenye nyumba yake ya zamani tunambembea, kwa sababu kwenye ekari tatu unaweza kujenga chochote unachotaka – huru.
Nani anahamishwa kwa nguvu? Hapa Loliondo nani anahamishwa kwa nguvu? Hakuna. Wanasema wananyang’anywa ardhi yao! Tanzania hatunyang’anyi ardhi ya mtu, huwa tunaelekeza tu hapa kunafaa kujenga soko, hapa shule. Si hapa
wala Ngorongoro – hakuna anayehamishwa kwa nguvu.
Hao wanaohama kwa hiari tunawafanyia mambo makubwa haijawahi kutokea. Nilishasema na naomba nirudie, yanayofanywa kwa wananchi wale wa Ngorongoro ni kwa ajili ya Ngorongoro tu – haitafanyika mahali pengine. Naomba nirudie hili: Haya tunayoyafanya Ngorongoro ya kumlipa, kumsafirisha, kumhudumia, tunawapa magunia mawili ya mahindi, tunawapa chakula cha leo anaposafiri na kesho ili waanze (maisha) vizuri, tumewapa na fedha ya motisha – haya yote ni kwa ajili ya Ngorongoro tu. Kwa nini? Kwa sababu wamejitokeza wenyewe kwa hiari kwa eneo hili muhimu.
Mheshimiwa Rais alisema hebu tufanye hilo kwa sababu umuhimu ule (kuilinda Ngorongoro) na hawa kujitokeza kwao…kwa kweli wamefurahi.
Ukitoka nje ya lango la Ngorongoro ndiyo unayasikia maneno mengi yanazungumzwa. Sikilizeni serikali inachosema, tuache kuwasikiliza wapotoshaji wengine. Kama unataka kujua Ngorongoro na Loliondo kuna nini sikiliza maelezo ya serikali. Hakuna mahali popote – si Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, Waziri Mkuu alipotamka kwamba tunakuja kuwahamisha Loliondo, kwamba tunakuja kuwaondoa kwa nguvu Ngorongoro.
Hakuna.
Eneo hili litalindwa wakati wote, eneo hili litalindwa wakati wote, eneo hili litalindwa wakati wote…tukielekea huko, Waziri wa Mifugo, eneo hili lina mambo mengi, lina mikanganyiko mingi.
Ni muhimu sasa fika Ololosokwan kujua pale kuna wafugaji wangapi, wana ng’ombe wangapi – weka alama zao – alama ya kuvika pete, hatutaki tena mtu achome ngozi ili ngozi ipate thamani.
Baada ya sensa hiyo kwa vijiji vyote 14 ambayo pia tutakuwa tunaratibu na wao kwa ajili ya kuokoa mifugo yetu kipindi cha ukame sana tujue tuna ng’ombe wangapi?
Nataka niwaambie hili: Kama tungekuwa tunanywesha ng’ombe wa Tanzania tu wala tusingepata shida hii. Kama ingekuwa tu mifugo ya Watanzania, hiyo ambayo tumeiona hapo wala kusingekuwa na shida.
Mkiruhusu kuingiza mifugo kutoka mahali kwingine popote ya kuja hapa kulisha na kutoka, mmeongeza idadi, mwisho mnasababisha serikali iendelee kuzuia mifugo mingi isiendelee kuongezeka. Hilo tutashirikiana na wananchi kuhakikisha kwamba hatuongezi mifugo ili hii iliyopo tuiratibu vizuri…mnajua kuna msimu hakuna malisho, ukiwa na ng’ombe
1,000 utawalisha wapi? Ni muhimu unapofuga kuku ujue una mahindi ya kuwalisha, usifuge kuku utegemee nyumba ya jirani.
Migogoro Loliondo
Taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2017 inasema wazi kuwa chanzo cha migogoro ya Loliondo ni kupingwa kwa upimaji wa mipaka ya vijiji na uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Baadhi ya vijiji vinapinga kutengwa kwa eneo la Pori Tengefu kwa madai kuwa eneo lililopendekezwa linatumika kwa malisho ya mifugo.
Utekelezaji wa mpango wa serikali ulishindikana kuanza kutokana na NGOs (zaidi ya 30 zilizopo Ngorongoro) kuchangia katika kuchochea migogoro ya Loliondo, kwa kuwa hutumia migogoro hiyo kupata fedha kutoka kwa
wafadhili.
“NGOs hizo haziafiki upimaji wa ardhi ya vijiji kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi kwa kuwa litawezesha kumalizika kwa migogoro, hivyo kuwakosesha fedha za wafadhili.
“Aidha, baadhi ya NGOs hizo zimeanzishwa na kampuni za utalii wa picha zinazofanya biashara hiyo ndani ya Pori
Tengefu la Loliondo kwa lengo la kulinda masilahi yao, ukizingatia kwamba wanafanya biashara katika eneo ambalo limekodishwa kwa kampuni ya uwindaji na kwamba wamenunua maeneo ndani ya Pori Tengefu kinyume cha sheria,” inasema taarifa ya Wizara ya Maliasili.
Miongoni mwa kampuni zilizojitwalia ardhi kinyemela ni AndBeyond ambayo licha ya sheria kuzuia, imeingia mkataba na Kijiji cha Ololosokwan wa kuhodhi hekta 51,230 ambazo ni sawa na ekari 126,592. Sheria inakipa kijiji kutoa ardhi kwa mwekezaji isiyozidi ukubwa wa ekari 50 pekee.
Aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangalla, kwenye andiko lake kuhusu Loliondo amesema: “Cha kusikitisha ni kwamba, wapiga propaganda za kuzuia kazi ya serikali kwenye eneo hili (uwekaji vigingi) wamekuwa,
toka mwaka 1992 wakidai kuwa Waarabu wameuziwa eneo hili na serikali (ukitaka kumuua paka anza kwanza kwa kumpa jina baya!)
“Yote hii ni kutafuta namna ya kupata utetezi wa Wazungu. Hata hivyo, eneo hili limekuwa na mashamba makubwa ya wawekezaji wa Kizungu tangu miaka ya 1980, na mengi yamegeuzwa kuwa lodge za kitalii, kama vile AndBeyond, Buffalo Luxury Tented Camp, Thomson’s Safaris na nyingine.
“Pengine mgogoro huu umepewa chachu na uwepo wa hawa wawekezaji wengine ambao wanaendesha utalii wa picha na wanalipa moja kwa moja kwenye serikali ya kijiji walipojenga na hawa wasingependa wanyama wawindwe kwa sababu wanakuwa na stress (msongo), hivyo kukwamisha utalii wa picha. Uwindaji wa kitalii haupeleki fedha katika serikali za vijiji, bali asilimia 75 ya mapato inakwenda serikali kuu, wakati asilimia 25 inakwenda halmashauri.
“Wapiga propaganda za wenyeji hawamtaki Mwarabu kwa kuwa hawalipi wao moja kwa moja, analipa huko juu tu, tofauti na hao wengine wa picha. Na hata kama anawajengea miradi mizuri ya maendeleo wao bado wangetaka awe chini yao tu, kwa sababu wangependa zaidi wapokee fedha kuliko miradi ya ujirani mwema (CSR) anayowapa!”
Katika matoleo yajayo JAMHURI litabainisha kwa uwazi kiini cha migogoro Loliondo, wanasiasa, NGOs na wote walio nyuma ya sakata hilo.