Nayaandika haya nikisukumwa na kauli ya Rais John Magufuli, ya “msema kweli ni mpenzi wa Mungu.”
Ili mambo yaweze kwenda mbele hatuna budi kuwa na ujasiri wa kuyasema mambo kwa uwazi ili kuondoa vikwazo vinavyoashiria mkwamo. Kuusema ukweli utawafanya viongozi wetu wakuu wasiendelee kulaghaiwa. Dhamira yao ni nzuri kwa hiyo kinachotakiwa ni sisi tulio pembeni kuacha woga ili tuyaseme mambo kwa lengo la kuwasaidia viongozi wetu.
Bila kumung’unya maneno ni kuwa endapo Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro ataendelea kuwa Mfaume Taka; na Mkuu wa Mkoa wa Arusha akawa ni huyu huyu Mrisho Gambo, tujiandae kuzika Pori Tengefu Loliondo na Hifadhi ya Taifa Serengeti. Huu ndio ukweli.
Unaweza kusema kuwa Taka na Gambo wana serikali yao ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali yao ni mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) na kampuni za wawekezaji zinazoendesha shughuli zake Loliondo. Wawili hawa wanaongezwa nguvu kutoka kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, William ole Nasha na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer.
Ukweli unaposemwa, wanachokilimbilia ni kuandaa taarifa za uongo na upotoshaji kuwa wanaowasema wamehongwa. Nipo hapa Loliondo na kuna kundi la wanahabari walioletwa kuandika uongo ili kuaminisha umma kuwa wanaowakosoa Taka, Gambo na viongozi wengine, wamehongwa. Makala hizo zitaanza kuonekana wiki hii.
Narejea kusema kuwa NGOs chochezi na chonganishi pamoja na wanasiasa wanaoishi kwa kutegemea migogoro ya ardhi Loliondo na Ngorongoro, wakiachwa hivi hivi hakuna suluhu itakayopatikana. Hata kama mgogoro huu utakwisha kesho, bado genge hili litaibua mgogoro mwingine alimradi tu liwe na chanzo cha fedha kutoka kwa wafadhili.
Taka na Gambo ndio wanaohamasisha wananchi waandamane kupinga mpango wowote wa Serikali wa kuilinda Loliondo. Hawa ndio wanaoeneza sumu ya uongo ya kwamba Wamaasai wanaondolewa katika ardhi yao. Hii ni ajabu kabisa.
Wiki iliyopita kuliandaliwa maandamano ya ‘wanawake’ yenye maudhui ya kuzuia utengwaji wa eneo la uhifadhi Loliondo. Napenda kuwahakikishia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Rais John Magufuli, kuwa maandamano hayo, na mengine yaliyokwishafanyika na yanayopangwa kuendelea, yanaratibiwa na Tika na Gambo. Huo ndio ukweli wenyewe.
Makala hii inalenga kuwaambia ukweli viongozi wakuu ili watambue kuwa wanaoikwamisha Serikali ni genge la viongozi wa Serikali waliokwekwa mfukoni na NGOs. Huo ndio ukweli wenyewe.
Yaliyojiri Loliondo na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuanzia Machi 6 hadi Machi 18, 2017 ni jazba, mori, chuki, fujo na kuasi meza ya mazungumzo na maridhiano.
Vurugu zimepangwa ili kupotosha mchakato wote kwa kusema ardhi ya Wamaasai inaporwa, na inauzwa na serikali kwa Mwaarabu wa OBC; na kwamba Wamaasai wananyanyaswa na wananyimwa na serikali kuchunga mifugo yao katika Pori Tengefu la Loloindo, Crater ya Embakai, Masek, Olduvai Goarge, NCAA na katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Baadhi ya watumishi wa serikali, viongozi wa serikali, viongozi wa CCM (wachache), Wazungu wachochezi kutoka nje ya nchi na baadhi ya watu wa jamii ya Kimaasai waliorubuniwa na NGOs; badala ya kuendelea na mchakato wa mazungumzo ya kumaliza mgogoro wa ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo, wao wanaendelea kutafuta namna na mbinu za kuvuruga mpango wa Serikali kama ulivyoelezwa na Waziri Mkuu Majaliwa.
NGOs zinazoishi kwa migogoro ya ardhi Loliondo na Ngorongoro (kwa kufanya biashara kwa kutumia migogoro ya ardhi Loliondo wanayoanzisha wao), zinahangaioka usiku na mchana kuona Loliondo haitulii. Kwa mtu mwenye akili timamu ataweza kujiuliza maswali kadha wa kadha kuwa je, NGOs zinataka kufanya mapinduzi? Nasema hivyo kwa sababu Wamaasai wanahamasishwa na NGOs, wanawezeshwa na NGOs, na wanatumiwa na NGOs kupinga mipango ya serikali na kuwapiga vita wawekezaji.
NGOs hizi zinapewa miongozo na ushauri na jasusi Susanna Nordlung kutoka Sweden na wanasiasa Matthew ole Timan na Tina Timan na hasa namna ya kukabiliana na migogoro ya ardhi Loliondo.
NGOs zinazoivuruga Loliondo:
Hapa ni vema Mheshimiwa Waziri Mkuu atambue NGOs ambazo ni kikwazo cha amani na chanzo kikuu cha vurugu zinazoendelea Loliondo.
i)Ndorobo Safaris: Meneja Mkuu ni David Peterson – anaishi Olasiti, Arusha na ni mratibu mkuu wa PWC & UCRT) mwenye ushirikiano wa karibu sana na wafadhili wa kimataifa kutoka Ulaya na Marekani. Anafadhili NGO ya Ujamaa Community Resource Team– UCRT ambayo Mkurugenzi wake ni Sinandei Makko – anayeishi Olasiti, Arusha na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ajira ya Wilaya ya Ngorongoro.
Ndorobo wanafadhili pia Pastoral Women Council (PWC) ambayo Mkurugenzi wake ni Maanda Ngoitiko – anayeishi Olasiti, Arusha. Huyu ni Diwani wa Viti Maalum- Chadema.
(iii) Pastoralists Indigenous NGO for Hunters and Gatherers – PINGOs FORUM. Mkurugenzi wake ni Edward Thomas Porokwa – anaishi Kwa Iddi Arusha.
Ngorongoro NGOs Network – NGONET. Hiii Mkurugenzi wake ni Samwel Nang’iria ambaye anaishi Kata ya Engusero-Sambu, Loliondo.
(iv) PALISEP Organization – Mkurugenzi wake ni Robert Kamakia anayeishi Kata ya Engusero-Sambu Loliondo.
(v) Tanzania Pastoralist Community Forum (TPCF) – Mkurugenzi wake ni Joseph Parsambei anayeishi Kaloleni Arusha.
(vi) IRK Ramat Organization – Mkurugenzi wake ni Yaniki Idoinyo – anayeishi Kijiji cha Ololosokwan na ni Diwani wa kuchaguliwa wa Kata ya Ololosokwan.
(vii) Legal Human Rights Coalition (LHRC) Mkurugenzi wake ni Onesmo ole Ngurumwa –ofisi yake ipo Magogoni na anaishi zaidi Dar es Salaam.
(vii) Frankfrurt Zoological Society& GIZ-Loliondo (FZS & GIZ-Loliondo) – Mratibu wa shughuli za maendeleo za FZS & GIZ-Loliondo kwa upande wa Loliondo ni Dk. Karaine Kuneei. Kinachofanywa na asasi hii ni ajili ya uhifadhi na kwa ajili ya maslahi ya biashara zao binafsi kadiri ya mabwana wakubwa kutoka Ujerumani wanavyotaka kwa eneo la Loliondo na kwa SENAPA pia.
Frankfrurt Zoological Society imekuwa na kivuli chake cha kufadhili miradi ya TAWIRI na TANAPA ndani ya SENAPA. Kwa kuwa na ofisi ndani ya eneo la Serikali, uamuzi wake umekuwa ukichukuliwa na wengi kama ndio msimamo wa Serikali, jambo ambalo si la kweli. Dk. Kuneei anaishi Wasso, Loliondo. Huyu amekuwa akieneza ‘sumu’ ambayo ni msimamo wa FZS kufanya yafuatayo:
(i) Kukubali kuanzishwa kwa WMA na kupinga utengaji wa kilometa za mraba 1500 kwa ajili ya Pori Tengefu. Amekuwa akiwahamsisha na hata kuwashinikiza madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji, malaigwanani, NGOs na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro wakubali WMA badala ya Pori Tengefu Loliondo.
(ii) Frankfrurt Zoological Society & GIZ-Loliondo chini ya mwongozo wa Dk. Kunnei wameanzisha vikundi vya COCOBA (Community Conservation Bank) katika baadhi ya vijiji katika Tarafa ya Loliondo kama vile vijiji vya Tinaga, Mageri, Eyasi-Mdito, Oldonyo-Was, Magaiduru, Oloirien, Engusero-Sambu, Ng’arwa, Orkiu, Ololosokwan, Kirtalo na Oloipiri. Mpango huu wa Dk. Kuneei kama kiongozi mwakilishi wa FZS& GIZ-Loliondo kwa vikundi vya COCOBA kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira na misitu kwa wanajamii wenyewe ni mpango na mfumo mzuri, lakini umeleta na unaendelea kuleta athari na migogoro ifuatayo kwa ardhi katika Tarafa ya Loliondo na vijiji tajwa na hata kwa wawekezaji wakubwa:
(a) Frankfrurt Zoological Society& GIZ-Loliondo haipaswi kuanzisha mfumo huu wa uhifadhi wa mazingira na misitu katika vijiji vya Loliondo kwa sababu mpaka sasa bado hakuna mpango rasmi wa matumizi bora ya ardhi kwa wilaya nzima ya Ngorongoro, kwa kata na kwa vijiji husika kwa ajili ya maeneo ya makazi, maeneo ya kilimo na maeneo ya nyanda za malisho kwa kila kijiji hivyo. Hali inazua vurugu na kwa sasa tayari kuna vurugu na fujo wa kuanzishwa kwa mfumo huu wa uhifadhi wa mazingira vijijini.
(b) Tayari athari zimejitokeza na kesi ipo mahakamani ya Frankfrurt Zoological Society & GIZ-Loliondo kuanzisha vikundi vya COCOBA katika vijiji vya kata husika kukizana na kusababisha migongano ya kimaslahi na mifumo mingine ya wadau wengine vijijini kimakazi, kwa kilimo na kwa ufugaji.
Na hasa migogoro ya ardhi inajitokeza pale panapokuwa na mwingiliano wa maeneo ya uhifadhi wa mazingira, misitu, ulinzi wa wanyamapori, maeneo ya kilimo, maeneo ya makazi, maeneo ya kulishia mifugo, vyanzo vya maji vijijini na kadhalika na kwa mahitaji kuwa kila mdau anagombania na kudai kwamba eneo hili ni lake.
(c) Frankfrurt Zoological Society & GIZ-Loliondo chini ya uongozi wa Dk. Kuneei tayari imekuwa ni chanzo cha migogoro ya ardhi Loliondo ndani ya vijiji, kata na tarafa ya Loliondo kwa kuanzisha rasmi mpango na mfumo mpya wa uhifadhi wa mazingira vijijini bila kuwapo matumizi bora ya ardhi ya wilaya na uanzishwaji wa vikundi vya COCOBA vijijini inayosababisha migogoro ya ardhi na kesi nyingi kufunguliwa.
Anashawishi halmashauri na wenyeviti wa vijiji kufanya kampeni ya kuanzishwa kwa WMA katika ardhi ya vijiji vya kata saba na kupinga uwepo wa Pori Tengefu Loliondo la kilometa za mraba 1,500.
(d) Frankfrurt Zoological Society & GIZ–Loliondo vile vile imefadhili uwekwaji wa mipaka kati ya mkoa wa Arusha na Mara ambayo pia ni mipaka baina ya wilaya za Ngorongoro na Serengeti; na pia ni mpaka kati ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori Tengefu Loliondo la kilomita za mraba 1,500 ambayo wadau wengine wanasema ‘beacons; zimeingia zaidi ndani ya mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro na kumega sehemu ya Pori Tengefu Loliondo.
Nini kifanyike?
Serikali iwaondoe Frankfrurt Zoological Society & GIZ-Loliondo wasiishi tena ndani ya SENAPA na wala kwenye Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Waishi nje ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na waishi pia nje ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ili kukwepa uchochezi.
Wenye NGOs ni akina nani?
Upo ugumu wa kupata mwafaka kuhusu maridhiano ya Pori Tengefu Loliondo kuweka matumizi bora ya ardhi endapo NGOs zitakuwa kwenye Kamati ya Maridhiano. Hapa swali la msingi la kujiuliza ni kwamba je, hawa watu wa NGOs ni akina nani?
Watu wenye NGOs ni watu waliojiwekea mipango na mikakati za kile wanachodai kuwa ni ‘kuikomboa’ ardhi ya Wamaasai wanaodai kuwa imeporwa na serikali na wawekezaji. Tabia hii ikiachwa iendelee, ina maana maeneo mengine kama ya Mtwara, Mara, Mererani na kwingineko nchini wananchi watadai ardhi kuwa ni mali yao, na si mali ya Taifa zima.
NGOs za Loliondo zimejipanga namna hii:
(a) Kama ‘watetezi wa ardhi ya Wamaasai’ ni lazima wawe kwenye NGOs na washike nyadhifa na madaraka ya juu kama wakurugenzi kwenye NGOs.
(b) Ni lazima wawe viongozi wa serikali kwa kushika Uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
(c) Ni lazima wawe watumishi wa serikali kwa kushika ubunge wa Wilaya ya Ngorongoro.
(d) Lazima wawe wafanyakazi wa Serikali.
(e) Ni lazima wawe wafanyakazi wa NGOs na wa Serikali pia.
(f) Wafuasi wa vyama vya siasa vya upinzani na wa chama tawala ni watu wa NGOs na ni wanaharakati.
(g) Madiwani wa Chadema na wa CCM wa kuchaguliwa na wa Viti Maalumu ni watu wa NGOs.
1. Maanda Ngoitiko (PWC)
Kwa malengo ya ushawishi yupo kotekote: Kwenye NGO, serikalini na Chadema. Amejitwalia ekari 3,000 katika eneo la Irmasilig Mundorosi. Ana kesi ya ujasusi na uchochezi/uchonganishi mahakamani dhidi ya wawekezaji, serikali na wananchi. Wafadhili wake ni African Initiatives, Comic Relief, Global Partners for Development, Minority Rights Group International, Oxfam, Segal Family Foundation, Sylvia Adams Trust, The Waterloo Foundation, Trias & UN WOMEN.
Washirika wa PWC:
CASEC – Community Aid and Small Enterprises, International Institute for Enviroment and Development, Legal and Human Rights Centre, Longido Community Development Organization, Maasai Women’s Development Organization, Maliasili Initiatives, Pastoral Council of NCA, PINGOs FORUM – Pastoralists Indigenous NGO’s Forum, TNRF – Tanzania Natural Resource Forum & UCRT – Ujamaa Community Resource Team.
NGO ya PWC ni ya ukoo wa Purko. Mwanzilishi ni Ndorobo Safaris ili kulinda maslahi yake Loliondo. Taasisi ina mabilioni ya fedha kwa ajili ya utetezi wa ardhi Loliondo. Inapokea wastani wa Sh bilioni 2.5 kwa mwaka kutoka kwa wafadhili wake.
PWC inapata fedha kwa njia ya migogoro ya LGCA na Thomson Safaris. Aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Jowiko Kasunga aliwafukuza PWC Loliondo kwa migogoro ya ardhi na wakakimbilia wilaya za Monduli, Longido na Tarafa ya Ngorongoro. Mkurugenzi wa PWC ni rafiki na mdau wa Ndorobo Safaris. Migogoro ya ardhi Loliondo baina ya vijiji na vijiji ina mkono mrefu kabisa wa PWC.
Mwanaharakati wa karibu na Maanda ni Diwani Tina Timan. Tina ni Mkenya aliyeolewa na Matthew Timan. Ng’ombe wa Kenya amewajaza katika Pori Tengefu la Loliondo. Tina ni Diwani Viti Maalum Chadema. Ni mfuasi, mtetezi na mshauri mkuu wa PWC.
Tina ni mpinzani mkubwa wa OBC na Thomson na anawaita wawekezaji waporaji wa ardhi ya Wamaasai. Kuna madai kuwa kwa vile ni Mkenya, huenda analenga kuwafukuza wawekezaji Tanzania ili waende Kenya kuwekeza.
Tina na mume wake Matthew Timan wamejitwalia ardhi ekari 2000 eneo la Endingting Ololosokwan; wamechukua ekari 100 eneo la Wasso na wamei9ngia katika eneo la Shule ya Sekondari ya Loliondo na kujenga nyumba ya kisasa. Tunapozungumza kupungua kwa eneo la malisho, mbona watu wa aina hii hawaguswi? Je, Waziri Mkuu anayajua haya?
Rafiki mwingine wa Maanda ni Mheshimiwa Pirias Maingo Killel. Pirias anafanyakazi PWC kama Ofisa Maendeleo wa Wanawake. Huyu ni Diwani Viti Maalum (Chadema). Ni mpinzani namba moja wa wawekezaji na mchochezi wa migogoroya ardhi Loliondo.
Mashirika ya Kimataifa yanayofanya kazi Loliondo kwenye koo mbili tu za Kimaasai ya Purko na Loita ambao wanaishi Kenya na Tanzania; na wanawafanya koo hizi mbili ziwe na mitizamo hasi juu ya wawekezaji (hasa OBC na Thomson) nao ni: UNESCO inayofanya kazi Ololosokwan kupitia NGO ya RAMAT ya Diwani Yaniki Idoinyo wa Ololosokwan (CCM).
Shirika la Oxfam linashirikiana na NGOs ya PALISEP ambayo ni ya Robert Kamakia katika eneo la EnguseroSambu kwa ukoo wa Loita.
Shirika la ACCORD lipo Wasso na wafanyakazi wake wote (asilimia 99.9) ni ukoo wa Loita. Hata walinzi ni Loita.
Kuna miradi ‘danganya toto’ ya PWC Longido kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Laizer na pia ipo Kata ya Engaresero kwa Diwani Ibrahimu Sakai ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya Ngorongoro. Wanamlinda Maanda kwa nguvu zote!
Sinandei Makko (UCRT)
Huyu ni mume wa Maanda Ngoitiko. Kwa nia ya ushawishi yupo upande wa NGO na serikalini.
Wafadhili wa UCRT ni Ndorobo Funds for Tanzania, Flora Family Foundation, Friends of Serengeti Switzerland FSS, IFAD- Indigenous Peoples Assistance Facility, International Land Coalition, International Work Group for Indigenous Affairs, Maliasili Initiatives, Oxfam, The Nature Conservancy, The Womadix Fund, Trias, United States Agency for International Development, Veterinaires Sans Frontieres Bbelgium & Wildlife Conservation Society.
Mwanzilishi wa hii NGO ni Ndorobo Safaris ili kulinda maslahi yake Loliondo na hivyo ni mdau mkubwa wa Ndorobo Safaris. Wanapata wastani wa Sh bilioni 1.5 kwa mwaka. NGO hii ni ya ukoo wa Purko. Migogoro ya ardhi kati ya vijiji na vijiji vinasababishwa na UCRT wanapopima vijiji hivyo kwani wanapendelea vijiji vya koo zao za Loita na Purko. DC Kasunga aliwafukuza UCRT Loliondo kwa migogoro ya ardhi wakakimbilia wilaya za Simanjiro, Longido, Monduli na Hanang.
Huyu ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ajira ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Sinandei anafanyaje kazi hii wakati anakaa ofisi ya UCRT iliyopo Olasiti, Arusha kwa jamaa zake Ndorobo Safaris na pia bado yupo Hanang. Nyumbani ni Arash, Loliondo.
Washirika wa UCRT ni African Initiatives, Carbon Tanzania, Community Reseach and Development Services, Hadzabe Survival Council, Honeyguide, KINNAPA, Kivulini Trust, Longido Community Development Organization, Mama Ardhi Alliance, MVIWATA Arusha, NGONET-Ngorongoro NGO Network, Northern Tanzania Rangelands Initiative, Oikos East Africa, Pastoral Women Council, Pastoralist Indigenous NGO’s Forum, Pastoralists Katiba Initiative (KAI), Pathfinder International, Tanzania Land Alliance & Tanzania Natural Resource Forum.
Pia ni wadau wa PINGOs Forum na maswaiba wa wanasiasa wakuu wa Chadema, Laizer (CCM), Sakai (CCM) na Nasha. Ni washirika wa jasusi Susanna Nordlung kutoka Sweden kupinga LGCA na kutaka WMA ili kumwondoa OBC na vijiji kumiliki eneo la Pori Tengefu Loliondo. Wanataka WMA ili jamii isimamie yenyewe kimkataba na kibiashara.
Samwel Nang’iria (NGONET)
Ana uhusiano na mitandao ngazi ya Mkoa wa Arusha (PINGOs Forum – ya Edward Thomas Porokwa), ngazi ya kitaifa (Tanzania Human Rights Defenders Coalition – ya Onesmo Ngurumwa). Kwenye ngazi ya kimataifa yuko karibu sana na Susanna.
NGONET ni Ngorongoro NGOs Network. Ni mtandao wa mashirika ngazi ya Wilaya ya Ngorongoro. NGO hii ni ya ukoo wa Loita.
Mfadhili wake ni Oxfam Ireland. Samwel ni Mkurugenzi wa NGONET. NGOs zote Ngorongoro zipo chini yake, kwa mfano PWC, UCRT PALISEP, LADO, Embudeo na kadhalika. Mke wake ni mfanyakazi kwenye Idara ya Maendeleo ya Jamii, ofisi sekta ya NGOs wilayani. Rafiki wa Samwel Nang’iria ni Diwani wa Kata ya EnguseroSambu, Osoitai Parmiria.
Anafanya kazi NGONET kama Afisa Mipango na Miradi wa NGONET. Ng’ombe wote wa kata yake ya EnguseroSambu wamejazana kwenye Pori Tengefu Loliondo. Ni wadau wa PINGOs Forum na maswaiba wa wanasiasa.
Joseph Parsambei (TPCF)
Tanzania Pastoralist Community Forum (TPCF) hii ni NGO ya ukoo wa Loita. Pasrambei ni Mkurugenzi wa TPCF. Rafiki yake Matthew ole Siloma ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Siloma ni mfanyakazi na ni mtumishi wa TPCF. Ndiye Mdhibiti wa Fedha wa TPCF. Siloma ni Diwani wa Kata ya Arash ambayo ni wang’ang’anizi wa Pori Tengefu na Hifadhi ya Taifa Serengeti katika uingizwaji wa mifugo huko.
Parsambei alikuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM mwaka 2015. Amekuwa haungiu mkono msimamo wa serikali wa kuihifadhi Loliondo na amekuwa mwiba kwa wawekezaji. Hataki maridhiano na LGCA, bali anataka WMA ili wananchi wawe na mamlaka kamili badala ya serikali na wawekezaji.
Hataki maridhiano ya Pori Tengefu kwa matumizi ya ardhi mseto. Anataka WMA tu.
Robert Kamakia (PALISEP)
Kamakia ni Mkurugenzi wa PALISEP. Huyu ni rafiki wa Susanna Nordlung na wanasiasa wa Kenya. PALISEP ni NGO ya ukoo wa Loita. Anaungana NGOs za NGONET, PWC, UCRT, TPCF, LADO n.k ili ng’ombe wa Kenya, kata za EnguseroSambu na Orgosorok wachungwe katika Pori Tengefu. Kamakia anashirikiana na wanasiasa kama Diwani William Parmiria na mbunge ili mifugo yao ya EnguseroSambu ipate malisho kwenye Pori Tengefu Loliondo.
Yaniki Idoinyo
Huyu ni Diwani wa Ololosokwan (CCM). Anatetea mkataba ambao Kijiji cha Ololosokwan kimeingia na wawekezaji wa Andbeyond (Clein’s Camp). Anatetea mwekezaji aliyepewa hekta 25,000 jambo ambalo ni kinyume cha sheria za ardhi Tanzania. Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro haina lolote inaloambulia kwenye mkataba huo.
Indoinyo ni Mkurugenzi wa Shirika la IRK-RAMAT. NGO hii ni ya ukoo wa Purko.
Ni mjumbe wa Kamati ya Ardhi na Mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Kijiji chake cha Ololosokwan kinamiliki cheti batili cha usajili wa kijiji. Hataki maridhiano na LGCA, bali anataka WMA ili wananchi wawe na mamlaka kamili badala ya serikali na mwekezaji.
Metui Tipap (LADO)
Metui Tipap ni Mkurugenzi wa LADO. Ni Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Ni Diwani wa Kata ya Oloirien (Chadema). Hataki maridhiano na LGCA, bali anataka WMA akiamini kwenye WMA mapato makubwa yaishia kwa baadhi ya viongozi na wananchi kwenye ngazi ya kijiji.
Edward Thomas Porokwa (PINGOs Forum)
PINGO Forum ni mtandao wa mashirika ngazi ya mikoa ya Arusha na Manyara. Porokwa ni Mratibu wa PINGOs Forum. Anatumia mbinu ya lobbying & advocacy kuwashawishi viongozi wa serikali. Ni mpinzani wa wawekezaji anaowaita waporaji wa ardhi ya Wamaasai.
Gabriel Olle Killel (KIDUPO)
Shirika la KIDUPO liliombwa na kata tatu za Oloipiri, Oloirien na Maaloni kuwezesha mazungumzo ya mezani baina ya wawekezaji na vijiji kuhusu mpango wa matumizi bora ya ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo, lakini yaliishia kuvurugwa na NGOs, wanaharakati na wasiasa.
Gabriel ni Mkurugenzi wa KIDUPO na swahiba na rafiki mkuu wa serikali, wawekezaji na wananchi katika masuala yahusuyo ardhi, hasa ya Pori Tengefu Loliondo. Gabriel ni mfuasi wa CCM. Anataka kilometa za mraba 1,500 za Pori Tengefu Loliondo zikatwe ili kuwepo na uhifadhi na utalii endelevu Loliondo.
Anataka pia kuwapo matumizi ya ardhi mseto kwa malengo ya kudhibiti uingizwaji wa ngo’mbe kutoka Kenya, kata na vijiji vingine tarafani Loliondo. Anataka LGCA. Hapendi WMA.
William Nasha (RAMAT-Law)
RAMAT-LAW ipo eneo la Azimio katika jengo la Mollel jijini Arusha. Nasha ni Mkurugenzi wa RAMAT-Law. Ni wakili na mwanasheria. Anafanya kazi ya kibiashara ya kisheria na asasi yake ya RAMAT-Law. Pia ni mwanasiasa, Mbunge wa na Naibu Waziri Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Ni mfuasi wa NGOs na anawaona wawekezaji kama ni wapora ardhi ya Wamaasai. Anataka WMA badala ya LGCA ili wananchi wa jimbo lake la uchaguzi, Tarafa ya Loliondo wawe na mamlaka na ardhi ya Pori Tengefu Loliondo. Hataki kilometa za mraba 1,500 za Pori Tengefu zikatwe. Anataka WMA ili ardhi yote ya pori tengefu imilikiwe na vijiji na wawekezaji wawe chini ya vijiji!
Natang’aduaki Mollel (NEPT)
Natang’aduaki Mollel ni Mkurugenzi wa Ngorongoro Education Project Tanzania (NEPT) iliyopo Ngorongoro.
Ni Ofisa Elimu Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido. Kahamia Longido kikazi kwa sasa. Aliwahi kupeleka timu ya viongozi wa Halmashauri akiwepo Tina Timan na Susanna Nordlung katika Kijiji cha Karkamoru kuwaonesha sehemu ya kujenga shule ya msingi akijua ni ndani ya Pori Tengefu Loliondo.
Susanna Nordlung
Huyu ni jasusi wa kimataifa kutoka Sweden mwenye maslahi mengi katika mgogoro wa ardhi Loliondo ana tovuti kwa ajili ya uchochezi na uchonganishi ili aweze kuendelea kuishi kwa migogoro ya ardhi Loliondo. Amekuwa akikusanya mabilioni ya fedha kwa mgongo wa ‘uetetezi’ wa wananchi wa Loliondo. Fedha nyingi zinatoka Ulaya na Marekani na kwa wafadhili binafsi kupitia taarifa za uongo na za upotoshaji juu ya masuala ya ardhi. Taarifa nyingi anaandaliwa na mamluki wake Watanzania na Wakenya walioko Loliondo.
Mzungu huyu mwanamke anatumiwa na NGOs za Loliondo za PWC, UCRT, TPCF, PALISEP, IRK RAMAT, LADDO, NGONET, PINGOs Forum na taasisi zinazoratibiwa na kusimamiwa na Onesmo ole Ngurumwa za Tanzania Human Rights Defenders Coalition na Legal Human Rights Coalition (THRDC/LHRC). Huyu ameshafukuzwa hapa nchini kwa PI mara kadhaa, lakini akawa anaingia kinyemela kwa msaada wa mamluki Watanzania.
Maazimio ya wanasiasa na NGOs
Maazimio ya wanasiasa na NGOs katika harakati zao za kupinga rasmi mipango ya Serikali kuhusu uwekezaji na matumizi bora ya ardhi kwenye tarafa za Loliondo, Sale na Ngorongoro yamefikiwa.
Mbinu inayotumiwa ni pamoja na kuhamasisha migogoro, maandamano, kilimo sehemu za uhifadhi na kuingiza mifugo kwa wingi kutoka Kenya.
NGOs zilizotajwa hapo juu na wanasiasa wanairubuni jamii ya Kimaasai ili kuhujumu mchakato wa majadiliano na maridhiano kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu Majaliwa.
Wakitambua kuwa hoja za uhifadhi zinazidi kwa mbali sana hoja zao za ubinafsi na chuki wa wawekezaji, Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wameamua, ama kwa ushawishi wa fedha, au kwa hadaa, kuandaa hujuma dhidi ya Serikali kwa kuandaa maandamano ili kuwadanganya viongozi wakuu kuwa wananchi wa Loliondo hawataki kutengwa kwa Pori Tengefu.
Juma lililopita kwenye NCAA bado NGOs hizo hizo na wanasiasa waliwahamasisha Wamaasai kufanya maandamano na kuandika mabango kwa lengo la kuendelea kuwaweka ng’ombe kienyeji na kiholela katika bonde la Ngorongoro kinyume cha maagizo ya Waziri Mkuu Majaliwa.
Wanaopotosha kutowekwa kwa matumizi bora ya ardhi kwa kutenga kilometa za mraba 2500 kwa ajili ya makazi ya vijiji; na kilometa za mraba 1500 kwa ajili ya uhifadhi ni hawa wafuatao:
(1) PWC – Mkurugenzi ni Maanda Ngoitiko na ni Diwani Viti Maalum (Chadema) wilayani Ngorongoro. Ni mke wa Sinandei Makko. Mwanzilishi wa NGO hii ni Ndorobo Safaris kwa ajili ya kulinda maslahi yao Loliondo.
(2) UCRT – Mkurugenzi ni Sinandei Makko na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ajira Wilaya ya Ngorongoro. Ni mume wa Maanda Ngoitiko. Mwanzilishi wa NGO hii ni Ndorobo Safaris kwa ajili ya kulinda maslahi yao Loliondo.
(3) NGONET – Mkurugenzi ni Samwel Nang’iria na huyu anawasiliana na mitandao ya kimataifa kama vile Avaaz na jasusi Susanna Nordlung na kutoa ripoti mbalimbali za migogoro ya ardhi kwa Loliondo. (NGONET ni Mtandao wa NGOs zote ngazi ya Wilaya ya Ngorongoro.
(4) TPCF – Mkurugenzi ni Joseph Parsambei. Mdhibiti Fedha wa NGO hii ya TPCF ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Matthew ole Siloma. NGO hii imepokea fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha WMA inaanzishwa Loliondo.
(5) PALISEP NGO – Mkurugenzi ni Robert Kamakia. Huyu anawasiliana na jasusi Susanna Nordlung kwa kuratibu migogoro ya ardhi Loliondo.
(6) IRK RAMAT NGO – Mkurugenzi ni Yaniki Idoinyo ambaye ni Diwani wa Ololosokwan na kijiji chake cha Ololosokwan kimeingia mikataba feki ya kilomita 25,000 ya ardhi ya kijiji na Kampuni ya Andbeyond/Cleins’ Camp ya Afrika Kusini bila ridhaa ya halmashauri na wala ya Wizara ya Maliasili na Utalii/Mamlaka ya Idara ya Wanyamapori na eneo husika bado ni kitalu cha uwindaji cha kampuni ya OBC kwa mujibu wa sheria.
(7) LADDO NGO – Mkurugenzi ni Metui Tipap na ni Diwani wa Oloirien-Magaiduru. Yeye ni mfuasi wa WMA na hapendi Pori Tengefu Loliondo.
(8) PINGOs Forum – Mkurugenzi ni Edward Thomas Porokwa. PINGOs Forum ni mwavuli wa NGOs/mtandao wa NGOs ngazi ya Mkoa wa Arusha na hasa kwa mashirika ya Wilaya ya Ngorongoro. PINGOs Forum inatumiwa na jasusi Susanna kupata fedha kutoka Ulaya na Marekani ili kuwezesha NGOs kupambana na serikali.
(9) Legal Human Rights Coalition & Tanzania Human Rights Defenders Coalition – zinazosemewa na Onesmo Ngurumwa na ambaye pia ni mkurugenzi wa LHRC. Taasisi hizi ngazi ya kitaifa zinatumiwa sana na jasusi Susanna kwa shughuli za uchochezi na uchonganishi kwa kumtumia kiongozi wake ambaye ni Mkikuyu kutoka Kenya, lakini akiwa anajifanya Mtanzania.
Majina ya baadhi ya wahusika wakuu wa mgogoro ni:
(i) Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Michael Laizer. Yeye aliwakaribisha jimboni kwake Longido (akiwa mbunge) NGOs za PWC na UCRT. Laizer anazikingia kifua NGOs hizi kwa nguvu zote na kwa sasa anahaha kuhakikisha Maanda Ngoitiko apewe hati ya kusafiria ambayo ilizuiwa na Idara ya Uhamiaji.
(ii) Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Ibrahimu Sakai ambaye ni swahiba wa mashirika ya PWC & UCRT na yanafanya kazi katika kata ya Ngaresero.
(iii) Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Matthew Siloma.
(iv) Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha na ambaye pia ni Mbunge wa Ngorongoro. Huyu ni mtu wa NGOs tangu zamani. Ukiacha ubunge na uwaziri kuanzia mwaka 2015, hajawahi kufanya kazi mahali popote nje ya NGOs.
(v) Supuk Daniel ole Maoi ni mtumishi wa Serikali – Ni mwalimu wa Sekondari ya Loliondo iliyojengwa na kampuni ya OBC na anashirikiana na jasusi Susanna kwa kumpa taarifa zote za Loliondo na Tanzania.
(vi) Clinton Eng’es Kairung ni mtumishi wa Serikali – Ni mwalimu wa Sekondari ya Digodigo na anashirikiana na jasusi Susanna ili Wazungu wapate kuingia mikataba na Wamaasai wa vijiji vya kata saba pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Mikakati za NGOs
(1) NGOs kutayarishiwa mihutasari ya vijiji vyote vya kata saba isainiwe na mikutano mikuu ya vijiji ipigwe mihuri na kupelekwa kwa NGOs hasa za PWC, UCRT, PINGOs Forum, LHRC kwa ajili baadaye kupata ushahidi mahakamani.
(2) NGOs kuwatafuta mawakili ili baadaye wafungue kesi dhidi ya OBC na Serikali (Wizara ya Maliasili na Utalii)
(3) NGOs na jasusi Susanna wamepanga kufungua kesi katika nne:
(i) Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha
(ii) Mahakama Kuu ya Tanzania
(iii) Mahakama ya Afrika ya Mashiriki/Mahakama ya Afrika.
(iv) Mahakama iliyoko The Hague, Uholanzi
Mapendekezo na Ushauri kwa Serikali
(a) Eneo la Pori Tengefu la kilometa za mraba 1,500 likatwe na litangazwe rasmi kuwa ni Pori Tengefu la Loliondo kwa ajili ya uhifadhi.
(b) Mifugo ya Kenya irudishwe Kenya mara moja.
(c) Ng’ombe wa kata za Orgosorok, Engusero-Sambu na za kata nyingine warudishwe kwenye vijiji vyao na huko huko kwenye vijiji hivyo waweke Matumizi Bora ya Ardhi zao – yaani maeneo ya Makazi, Maeneo ya Kilimo na Maeneo ya Kufugia. Uhamaji wa kiholela kwenye maeneo ya kata na vijiji vingine vipigwe marufuku.
(d) NGOs chochezi na chonganishi zifutwe.
(e) Watumishi wa serikali wenye NGOs chochezi na chonganishi wafukuzwe kazi au wahamishwe.
(f) Wanaofadhili NGOs chochezi na chonganishi kama vile Ndorobo Safaris, Oxfam Tanzania, PINGOs Forum, Legal Human Rights Coalition na kadhalika wapigwe marufuku kutoa fedha zinazoendeleza migogoro ya ardhi Loliondo; na ikibidi zipigwe marufuku kufanya kazi Tanzania.
(g) Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, wawajibishwe kwa kuwa ni wapinzani wakuu wa maslahi ya Serikali. Wamekuwa wakipanga maandamano ya kuipinga Serikali waliyoapa kuitumikia. Wamekuwa na ushirika wa kutia shaka, tena wa wazi wazi na NGOs pamoja na kampuni kama AndBeyond huku wakisimama kupinga uhifadhi.
Asilimia 50 ya maji katika Hifadhi ya Taifa Serengeti vyanzo vyake viko Loliondo. Mazalia ya nyumbu yako Loliondo. Msafara wa wanyamapori kati ya Serengeti -Maasai Mara ndio pekee uliobaki katika sayari hii. Utalii ndio unaoongoza kwa kuliingizia Taifa letu fedha nyingi za kigeni. Urithi huu umelindwa na mababu, mabibi na waasisi wa Taifa letu. Je, ni busara urithi huu kuuawa ilhali tukiwa na viongozi makini wa kitaifa? Je, NGOs ni nani hata ziweje kuitisha Serikali?
Naamini vyombo vya ulinzi na usalama vina macho na masikio hivyo vitafanya kazi sahihi na kuziarifu mamlaka husika ukweli kuhusu kinachoendelea Loliondo. Kama wasaliti wanaondolewa CCM naamini hata ndani ya Serikali wanaweza kuondolewa. Taka na Gambo hawana tofauti na wasaliti wengine.
Nawasilisha