Miezi michache baada ya baadhi ya madaktari na wauguzi wa Hospitali Teule ya Bugando kumtimua mgonjwa aliyeoza makalio akiwa wodini, kijana mwingine aliyepooza mwili kuanzia kiunoni hadi miguuni naye ameondolewa.
Kijana aliyeondolewa hivi karibuni ni Deogratius Daud Mashauri, mwanafunzi aliyehitimu kidato cha nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari ya Kakora iliyopo Nyang’hwale mkoani hapa.
Mashauri alifikishwa kwenye Hospitali hiyo ya Bugando, Oktoba 10, mwaka huu akisumbuliwa na maradhi mbalimbali yakiwamo ya kupooza nusu mwili, kidonda mguuni pamoja na kukosa haja kubwa na ndogo.
Mashauri alifikishwa Bugando na wazazi wake akitokea katika Hospitali ya Masumbwe iliyopo mjini Ushirombo, alikopewa rufaa ya kwenda kutibiwa kwenye hospitali hiyo. Alipelekwa kwa gari la wagonjwa walilolikodi kwa Sh 200,000. Rufaa yake ilizingatia vipimo vilivyotakiwa hivyo akapelekwa Bugando ambako waliamini wanavyo vifaa vya kutosha kuchunguza afya za wagonjwa.
Katika mahojiano na mwandishi wa gazeti hili, Mashauri anasema kwamba ugonjwa ulianza Desemba, mwaka jana baada ya kuhitimu elimu ya sekondari Kakora ambako alianza kuhisi maumivu sehemu za kiunoni.
Kutokana na hali hiyo, alichukua jukumu la kwenda kuonana na daktari kwenye Zahanati ya Kakora na alipoeleza namna anavyojisikia, alishauriwa kutumia dawa kutuliza maumivu na baadaye hali hiyo ilitoweka baada ya kuzitumia.
Baadaye Februari, mwaka huu maumivu ya kiuno yalirudi tena na kutumia dawa mbalimbali za kutuliza maumivu kabla ya kwenda Maabara ya Four Ways ya mjini Geita.
“Majibu yalipotoka nilielezwa kuwa nasumbuliwa na magonjwa ya zinaa, wakaniandikia dozi ambayo niliitumia pasipo mafanikio huku maumivu yakizidi kutoka kiunoni hadi magotini,” anasema Mashauri.
Hata hivyo, baada ya kuona tiba za Kizungu hazimsaidii, alikimbilia kwa mganga wa tiba za asili (jadi) aliyepo katika Kijiji cha Nyamtukuza katika Kata ya Kharumwa, Nyang’hwale.
Anasema akiwa kwa mganga huyo wa jadi alipigiwa ramli na kuelezwa kuwa siku zijazo atapooza kama mgonjwa wa polio.
“Na kweli, siku moja baada ya kuelezwa hivyo na yule mganga wa jadi wakati natoka uani kuoga, ghafla miguu yangu iliishiwa na nguvu kuanzia kiunoni kushuka chini na sikuweza kusimama mwenyewe na kudondoka chini kifudifudi, sikuweza kukaa wala kusimama tena kama awali,” anasema Mashauri.
Anasema wakati hayo yakitokea alikuwa peke yake nyumbani kwa mganga huyo wa jadi na siku iliyofuata aliwatumia taarifa wazazi wake waliofika kumtizama na kumjulia hali.
Hata hivyo, anasema usiku wa siku hiyo alishindwa kujisaidia haja ndogo pamoja na kubwa, hali iliyomshtua mganga wake ambaye aliwataka wazazi wake wamkimbize hospitalini kucheki tatizo hilo.
Wazazi wake walikodi usafiri wa bodaboda kutoka hapo kwa mganga wa jadi hadi Nyang’hwale kwa ajili ya matibabu zaidi, lengo likiwa kuchunguzwa kibofu cha mkojo.
Wakati anashuka kwenye pikipiki hiyo hospitalini hapo, mguu wake wa kulia uligusa bomba la bodaboda na kumuunguza.
Baada ya vipimo, madaktari hawakuweza kubaini ugonjwa, hivyo kupewa rufaa ya kwenda katika hospitali ya misheni iliyopo Sengerema mkoani Mwanza, ambako pia hawakubaini ugonjwa unaomsumbua.
Baadaye alipata taarifa juu ya mganga wa jadi, Paul Chasama, wa Nyankumbu mkoani Geita aliyewahi kumtibu na kumponya mgonjwa mwenye matatizo kama yake na mikasa ya kufanana, lakini alipuuza.
Baadaye alipelekwa Hospitali ya Masumbwe iliyopo mjini Ushirombo, ambako hata hivyo, hakupata matibabu baada ya kuelezwa kwamba hakukuwa na akiba ya damu hospitalini hapo, hivyo kurudishwa Bugando.
Anasema akiwa hajapatiwa huduma yoyote kwa usiku huo, siku iliyofuata alifuatwa na daktari wodini na kumweleza azma yake ya kumkata mguu ili amwanzishie matibabu ya maradhi aliyokuwa nayo.
Anasema kwamba daktari huyo aliyekuwa akiziba pua yake muda wote kutokana na harufu iliyokuwa ikitoka kwenye kidonda chake, hakutaka maelezo mengine huku akisisitiza lazima mguu ukatwe ndipo apatiwe matibabu.
”Huyu daktari kwanza alikuwa anaonekana mtu mwenye majivuno sana, muda wote ameziba pua kutokana na harufu ya kidonda changu mguuni, hakujali kama mimi kwa wakati huo sina damu mwilini wala kutaka kujua kama sipati haja kubwa, nikakataa kukatwa mguu,” anasema.
“Akawafuata wazazi wangu akiwataka wanishawishi nikubali kukatwa mguu, lakini nao waligoma kutokana na hali niliyokuwa nayo kwa wakati huo na huenda ningepoteza maisha kwani sikuwa na damu, nimepooza na hata mguu wangu haukuwa na hali ya kumshawishi mtu aukate. Wote walikataa. Nikaweka saini ya kukataa,” anasema.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, daktari alimfuata na kumtaka awaeleze wazazi wake wamtoe wodini hapo na kumpeleka wanakojua wao kwa madai ya kugoma kukatwa mguu. Aliondoka hospitalini hapo huku wakitozwa Sh 20,000 ya kitanda hadi wilayani Geita ambako walifikia katika moja ya nyumba za wazazi wake zilizopo Nyankumbu.
Baadaye alikwenda kwa Mganga wa jadi Chasama na kupatiwa dawa za mitishamba ya kuongeza damu sambamba na kusafishwa kidonda chake ambapo alianza kupata nguvu tofauti na awali.
“Baada ya wiki moja hali ilikuwa tofauti, damu iliongezeka mwilini na nilianza kupata haja kubwa na ndogo bila matatizo kutokana na dawa za asili nilizokuwa natumia na mpaka sasa hali yangu inaendelea vizuri na hata mguu wangu unaonesha matumaini ya kupona… kwa kweli namshukuru Mungu kwani ameniokoa kutoka kwenye kifo, ” anasema Mashauri.
Elizabeth Mahushi, mama mzazi wa Mashauri, mbali ya kusikitishwa na kitendo cha madaktari kuwatimua wodini bila mwanaye kupatiwa matibabu, aliiomba Serikali na taasisi zisizo za kiserikali kujenga utaratibu wa kukagua vyeti vya wafanyakazi wao ili kubaini walioajiriwa kwa kubebwa na wanaostahili kufanya kazi hizo.
Mama huyo anasema hakuona haja ya kuona uongozi wa hospitali kwa kuhofia mtoto wake angedhurika iwapo wangeng’ang’ania wodini kama walivyoamuriwa na daktari kuondoka eneo hilo.
Daud Mashauri, baba mzazi wa Mashauri, amemshukuru Mungu na kusema wameokolewa na Chasama.
Naye Chasama, mganga anayemtibu Mashauri, ameahidi katika kipindi cha miezi miwili ijayo mgonjwa huyo atakuwa amekwisharejea katika hali yake ya kawaida na kuendelea na shughuli zake za ujenzi wa Taifa kama ilivyokuwa hapo awali.
JAMHURI imebahatika kuona nyaraka mbalimbali zinazodhihirisha kwamba mgonjwa huyo amewahi kulazwa katika hospitali hiyo kabla ya kuagwa.
Tukio la Mashauri aliyeondolewa hospitali baada ya kukataa kukatwa mguu wake wa kulia, linafanana na la Joseph Luhogola (38), mkazi wa Kitongoji cha Nyabugera, Kijiji cha Mganza, Wilaya ya Chato mkoani Geita aliyeharibika makalio akiwa hospitali hapo kabla ya kuondolewa.
Jambo hilo lilitokea Mei 27, mwaka huu baada Hospitali hiyo ya Rufaa ya Bugando Mwanza kumtimua mgonjwa wa kupooza mwili, na baadaye kuoza makalio akiwa wodini hapo, hali iliyosababisha ndugu zake kumrudisha kwa Chasama anakotibiwa Mashauri.
Katika tukio ambalo lilihusishwa moja kwa moja na sakata hilo, Julai 10, 2014 Kanisa Katoliki lilimtimua aliyekuwa Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Teule ya Bugando, Profesa Charles Majinge.
Ajira ya mkurugenzi huyo ilisitishwa na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) Julai 10, mwaka huu, bila Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo ndiyo iliyokuwa ikisimamia ajira yake kupewa na taarifa.
Kabla ya kutimuliwa, mkurugenzi huyo alikuwa na mkataba alioingia na Serikali wa kuongoza hospitali hiyo kwa miaka mitatu kuanzia Julai 2013 hadi Julai 2016.
Taarifa za kutimuliwa kwa mkurugenzi huyo zilipokewa kwa shangwe na wagonja hao, wakidai kuwa Kanisa Katoliki limetenda haki kwa madai kuwa ameshindwa kusimamia wagonjwa.