Historia ya Ligi Kuu Uingereza (EPL) inaonyesha kuwa kwa kawaida timu ambayo inakuwa imeshika nafasi ya juu inapofika katikati ya msimu, aghalabu huwa kipindi cha Krismasi na Mwaka Mpya, hiyo ndiyo huwa bingwa mwisho wa msimu.

Unaposoma hapa, Liverpool, ambayo haijawahi kuchukua ubingwa wa Uingereza kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, inajidai katika kilele cha ligi hiyo ikiongoza kwa zaidi ya tofauti ya pointi kumi.

Hali hiyo imewafanya baadhi ya wachambuzi wa soka barani Ulaya kuanza kujiuliza iwapo Liverpool ipewe tu Kombe la EPL kwa sababu kwa jinsi hali ilivyo haionekani ni timu gani ina ubavu wa kuifikia na kuipiku katika mbio za kuwania ubingwa.

Mechi yao dhidi ya Leicester wiki iliyopita ilidhaniwa kuwa ingeweza kuisogeza timu hiyo ya pili karibu na Liverpool lakini mabingwa hao wa Kombe la Klabu Bingwa Duniani waliishushia timu hiyo kipigo cha 4-0. 

Wakati timu inayokamata nafasi ya tatu, Manchester City ilipopigwa na Wolves magoli 3-2, ndipo matarajio ya baadhi ya wachambuzi kuwa timu hiyo inayotetea ubingwa wake inaweza kufanya hivyo yakaanza kutoweka.

Akiuzungumzia ushindi wa 4-0 dhidi ya Leicester, mchambuzi wa soka, Phil Thomson, aliiambia SkySport kuwa: “Ule ulikuwa ni ushindi mkubwa ugenini kwa Liverpool. Katika muongo mmoja sijapata kuiona Liverpool bora kama ile. Jinsi walivyocheza ni hatari sana. Mwisho wa mechi walipata pointi tatu tu kama kawaida, lakini ukiangalia jinsi zilivyopatikana unaiona Liverpool ya kipekee kabisa.”

Anaongeza: “ Lolote linaweza kutokea katika soka, lakini Liverpool imethibitisha kuwa timu bora msimu huu. Inastahili kuchukua ubingwa. Hata hivyo, tusubiri kwanza, maana mambo bado sana.”

Kweli mambo bado, maana Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, anasema timu yake isiondolewe katika mbio za ubingwa msimu huu. Anasema licha ya kuwa nyuma ya Liverpool kwa pointi 14, yupo tayari kuweka rehani Kombe la FA na Kombe la Ligi ili kuweka mikakati ya kunyakua Kombe la EPL. Aliyasema haya baada ya kichapo nyumbani kwa Wolves.

Anasema: “Tumezoea kuwa juu katika msimamo wa ligi lakini sasa tupo mbali, kwa hiyo tunapaswa kutuliza akili. Nimeshasema mara nyingi kuwa hatupaswi kuifikiria Liverpool tu. Hivi sasa akili yetu inapaswa kujikita jinsi ya kushika nafasi ya pili. Tulikuwa na nafasi ya kuishika nafasi hiyo lakini tumeteleza.”

Anasema sasa hivi timu yake inapaswa kuhakikisha kuwa inapata nafasi ya kushiriki michuano ya Ulaya mwakani.

“Hatuwezi kuwa na kipaumbele kwenye mataji mengine, la sivyo msimu ujao tunaweza kujikuta nje ya michuano ya Ulaya,” anasema Guardiola.

Histori ya EPL inaonyesha kuwa ni katika msimu mmoja tu timu iliyo kileleni iliwahi kuongoza kwa tofauti ya pointi 13 katika kipindi kama hiki. Manchester United ilikuwa na pointi kama hizo Desemba 1993 na ikafanikiwa kushinda taji ikimaliza ligi ikiwa na tofauti ya pointi nane baada ya kuifunga Blackburn iliyokuwa inafundishwa na Kenny Dalglish katika mechi ya mwisho.

Klopp alonga

Hata hivyo, Meneja wa Liverpool, Jurgen Klopp, anajiepusha kuzungumzia ubingwa, akijikita kila mara kuzungumzia mechi inayofuata.

“Kitu pekee kinachobadilika ni kuwa namba ni tofauti. Ilikuwa 10, ikaja 11 na sasa ni pointi 13. Hatujihisi hicho, hatufikirii hicho (ubingwa). Hatujawahi kusema hicho mwisho wa mechi. Hakivutii,” anasema na kuongeza:

“Hata mimi ninaweza kutabiri. Haijawahi kutokea katika ligi ya Uingereza timu ilikuwa inaongoza kwa tofauti ya pointi nyingi (kipindi kama hiki) na ikashindwa kuchukua ubingwa. Hilo linaonekana kuwa hasi kwangu na sisi tumejikita kuangalia mechi inayofuata.”

“Sasa tunaangalia jinsi tutakavyokabiliana na Wolves (Jumapili iliyopita), Sheffield United, Everton, Tottenham na hatimaye Manchester United. Mechi hizo zote hatujui matokeo yake. Tunajitahidi kujiandaa. Namba si muhimu wakati huu,” anasema.

Wakati Klopp akijiepusha kuzungumzia ubingwa, Leicester yenyewe inapambana kuhakikisha kuwa haipotezi mchezo wowote ili kujiweka vizuri katika mbio za kuwania ubingwa. Hata hivyo, timu hiyo inajilaumu kwa kupoteza michezo miwili ya karibuni, jambo ambalo limepanua pengo la pointi kati yake na Liverpool, ingawa kufungwa kwa Man City kumeendelea kuihakikishia nafasi ya pili.

Kwa mujibu wa mchambuzi mwingine, Clinton Morrison, matokeo ya Leicester yanaonyesha tofauti ya viwango baina yake na Liverpool, jambo ambalo ndilo limeiweka Liverpool ilipo leo.

Anasema: “Hali si ya kutisha sana lakini Manchester City na Liverpool wako katika viwango tofauti ukilinganisha na Leicester. Wamekuwa na msimu mzuri, lakini bado mapambano yanaendelea.”

“Lakini unapaswa kumpa sifa Brendan Rodgers (Kocha wa Leicester), nadhani amefanya kazi kubwa. Kuna wachezaji wenye vipaji pale Leicester, lakini ukiangalia mechi zao mbili walizofungwa, wanaonekana dhahiri walizidiwa,” anasema.

Liverpool inakumbuka

Ingawa sasa hivi Liverpool iko mbele ya Man City kwa tofauti ya pointi 14, (wikiendi iliyopita) huku ikiwa nyuma kwa idadi ya michezo pia, lakini bado kuna matumaini kwa timu zinazoifukuza.

Msimu uliopita Liverpool iliukosa ubingwa huku kila mmoja akiamini kuwa walikuwa na nafasi kubwa ya kuipiku Man City. Je, hayo yanaweza kutokea tena msimu huu au Liverpool wapewe tu kombe lao?