*Wasema nchi imemshinda, watapika nyongo
*Wasema Serikali inaandaa taifa la wajinga

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Freeman Mbowe, Mbunge wa  Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Tanzania Labor Party (TLP), Agustino Mrema, wametoa tuhuma nzito kuwa nchi imemshinda Rais Jakaya Kikwete.

Viongozi hao wametaka Serikali ikiri wazi kushindwa kuongoza nchi, na wengine wameishinikiza itangaze haraka mfumo mpya wa elimu wenye ubora wa kimataifa.

Wabunge waliozungumza na JAMHURI wameahidi kupambana kwa nguvu kubwa bungeni kuhakikisha elimu inapewa kipaumbele cha kwanza kwa kutengewa bajeti kubwa mwaka 2013/2014.

Kilio cha ubora wa elimu, kimekuja baada ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia kuibua hoja kuwa Tanzania haina mtaala wa elimu. Ukiacha hilo, matokeo ya kidato cha nne ambapo wanafunzi zaidi ya asilimia 60 wameshindwa mitihani yameibua hasira za viongozi.

Baadhi ya wadau wanaitaka Serikali ifanye uamuzi thabiti kuhusu ufumbuzi wa anguko la elimu kwa kurudisha mitaala ya Uingereza (Cambridge) katika sekta ya elimu nchini.

Matokeo yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawamba wiki iliyopita, yanaonesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 walipata sifuri, huku 23,520 wakifaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi la tatu na 103,327 wakaambulia daraja la nne.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), ameliambia JAMHURI kuwa anguko la watahiniwa wa kidato cha nne ni matokeo ya Serikali kutoweka kipaumbele cha kuwekeza zaidi katika elimu.

“Serikali inaweka kipaumbele kwenye mambo yasiyo ya msingi. Inaingia mikataba na wageni isiyo na tija nchini, imesahau elimu na afya,” amesema Lissu ambaye ni Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya upinzani bungnie akiisimamia Wizara ya Katiba na Sheria.

Anaitazama Serikali kama chombo kilichoshindwa kuwatumikia wananchi kwa uzito unaostahili, na hivyo anataka yafanyike mabadiliko ya mfumo mzima wa utawala na uchumi.

Lissu ameelezea kushangazwa kwake na watu wanaoshangazwa na matokeo mabaya ya wahitimu wa kidato cha nne mwaka jana, wakati hali hiyo imeendelea kutokea mfululizo kwa miaka kadhaa sasa.

“Watu wanashangaa matokeo ya mwaka huu, lakini ya miaka ya nyuma yalikuwa mazuri kiasi gani? Ya mwaka jana yalikuwa mazuri kiasi gani?” amehoji na kuendelea:

“Elimu yetu imeporomoka kwa kiasi kikubwa kwa miaka mingi sasa, kwa hiyo kuyaangalia haya [matokeo ya kidato cha nne 2012] ni kukosea sana. Yaangalie kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita utagundua kwamba elimu imeporomoka sana, na inaelekea hali itakuwa mbaya zaidi.”

Lissu atofautiana na Mbowe

Kwa upande mwingine, Lissu ametofautiana kidogo na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuhusu hoja ya kujiuzulu kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.

“Nakubali waziri ajiuzulu, lakini matatizo ya elimu ni makubwa zaidi kuliko waziri mmoja na wizara moja. Matatizo ya elimu yanahusu mfumo mzima wa kiutawala. Waziri mmoja hana uwezo wowote wa kufanya lolote, ni responsibility (uwajibikaji) ya Serikali nzima,” amesema Lissu.

Akihutubia mkutano wa hadhara jijini Mwanza hivi karibuni, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alitoa siku 14 kwa Dk. Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo, kujiuzulu kwa kile alichodai kuwa wameshindwa kuongoza wizara hiyo ndio maana watahiniwa wameishia kuandika matusi na kupata sifuri katika mtihani huo wa kidato cha nne.

Hata hivyo, viongozi hao wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hawajaonesha nia ya kujiuzulu.

Alipoulizwa ni kwa namna gani CHADEMA inavyoshiriki kukabili matatizo yanayoiandama chini, Lissu amesema jukumu kubwa la chama hicho ni kupiga kelele kwa vile hakina fedha wala Serikali.

“Nguvu pekee ya chama cha upinzani ni kauli, kupiga kelele, hatuna hela, hatuna serikali. Wajibu wetu ni kuzungumza tu Serikali ione na kusikia, kama haioni wajibu wetu ni kuwambia wananchi kwamba angalieni hawaoni hawa,” amesema na kuendelea:

“CHADEMA tuna matumaini ya kushika dola, CCM (Chama Cha Mapinduzi) hawawezi tena kwa kila jambo. Kwenye afya, elimu, kilimo hawawezi kila mahala.”

Mrema aiponda CCM, Serikali

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, ameiponda CCM na Serikali kwamba ndio wachawi wa maendeleo ya Watanzania.

Akizungumza na JAMHURI, Mrema ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa, amewataka viongozi wa CCM na Serikali wasione aibu kukiri hadharani kwamba wameshindwa kuongoza nchi.

“Tunawambia wananchi kuwa nchi inapelekwa kusiko hawasikii. Serikali ya CCM ya miaka 50 na uhuru ndiyo hiyo. Hili anguko la elimu halijawahi kutokea katika Afrika. Naona kama hii nchi imewashinda hao jamaa… sasa ushahidi ni upi kuliko huu?

“Inakuaje aslimia 60 ya vijana wanaanguka [wanashindwa mtihani]? Utapata wapi vijana wa kwenda form five? Utapata wapi vijna wa kwenda vyuo vikuu? Madaktari utapata wap? Ni pigo kubwa,” amesema Mrema.

Mrema anataka matokeo hayo ya mtihani wa kidato cha nne yatazamwe kama janga la kitaifa, na hatua za makusudi zichukuliwe haraka kutafuta ufumbuzi thabiti.

“Tufumbie macho sekta nyingine kwanza tufufue hiyo ya elimu. Hali ni mbaya, nchi inakufa. Tunaona kwenye elimu hakuna vifaa, walimu hawatoshi, madarasa hayana madawati ya kutosha, yaani ni msururu wa matatizo. Serikali imeshindwa kutambua kwamba sekta ya elimu ndiyo kiongozi wa sekta nyingine zote.

“Serikali inasema kilimo kwanza, kilimo kwanza bila elimu enhee? Atakayekwenda kufundisha kilimo sasa ni nani? Ni hao waliopata mayai [sifuri]?

“Lakini pia, hawa vijana waliopata sifuri ni vigumu kupata ajira hata kwa watu binafsi. Unajua vijana wanataka kula, wanataka kulala, wanataka kuvaa, wakikosa njia halali ya kutafuta mahitaji yao watajiingiza katika vitendo viovu,” anasema Mrema.

Hata hivyo, Mrema ameahidi kupigania elimu bungeni kuhakikisha bajeti kubwa inaelekezwa kwenye sekta hiyo. Ametishia kutopiga kura ya kuunga mkono bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014 ikiwa suala la elimu halitapewa kipaumbele cha kwanza.

Kwa upande wake, mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la M.A. Mwenda, anaitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kurejesha mitaala ya elimu iliyotumiwa na Waingereza nchini kunusuru anguko zaidi la elimu.

“Tukubali ukweli, turudie mfumo wa zamani kwani kubeza kuwa elimu ya Waingereza ni mfumo wa kikoloni si sahihi. Mahitaji ya binadamu wote ni sawa,” amesema Mwenda na kuongeza:

“Viongozi na wanataaluma wote waliobobea nchini ni matunda ya elimu tunayoiita sasa kuwa ni ya kikoloni. Turudishe mfumo wa elimu wa Uingereza toka darasa la kwanza mpaka chuo kikuu.

“Tuombe msaada kwa Waingereza watusaidie kuwaandaa upya walimu wetu wa ngazi mbalimbali tuondokane na aibu ya kupata wasomi feki.

“Ndugu zangu mema ya mnaowaita wakoloni, msiyakatae. Nchi inayumba kielimu, tuchukue hatua… turudi Cambridge.”

Mwishoni mwa wiki Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameunda Tume ya kuchunguza anguko la elimu, hali inayoelezwa kuwa ni upotezaji wa fedha kwani tatizo linafahamika. Shule hazina walimu na wala vifaa vya kufundishia ambapo masomo ya sayansi yaliyopaswa kufanywa kwa vitendo yanafanywa kinadharia.