Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amesema moja kati ya makosa mawili yaliyosababisha Tundu Lissu kufutwa ubunge ni kutojaza taarifa za mali na madeni.
Kosa hili kwa mujibu wa Ibara ya 67(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kosa la kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Ibara hiyo imeeleza kuwa mbunge yeyote anakosa sifa za kuendelea kuwa mbunge au kuchaguliwa kuwa mbunge ikiwa atakuwa amekiuka ama kuvunja Sheria hiyo ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Zaidi, ibara hiyo imeweka wazi kuwa mtu huyo ataendelea kukosa sifa ya kuwa mbunge au kutochaguliwa kuwa mbunge katika kipindi cha miaka mitano tangu siku alipovunja Sheria hiyo ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Maana yake ukiivunja Sheria hiyo ya Maadili ya Viongozi wa Umma leo, 2019, tunahesabu miaka mitano kuanzia leo mwaka 2019 ambayo itakuwa hadi mwaka 2024 ndipo unakuwa na sifa tena ya kuweza kugombea na kuchaguliwa kuwa mbunge. Kwa hiyo Lissu atakosa sifa hii ya kuwa au kugombea tena ubunge hadi mwaka 2024.
Kuhusu urais
Ibara ya 39 (1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imebainisha wazi kuwa moja ya sifa kuu ya kugombea kiti cha rais wa Jamhuri ya Muungano ni kuwa na sifa ya kuwa mbunge au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Maana yake, ili uweze kuwa na sifa ya kuwania kiti cha rais lazima kwanza uwe na sifa za kuwa mbunge au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na unapokosa sifa ya kuwa mbunge au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, basi unakosa pia sifa ya kuwania kiti cha rais.
Kwa hiyo kama Lissu amepoteza sifa ya kuwa mbunge hadi mwaka 2024, amepoteza pia sifa ya kuwania kiti cha rais hadi mwaka 2024 kadhalika.
Hivyo, Lissu hataweza kugombea ubunge hadi mwaka 2024, lakini pia hataweza kugombea urais hadi mwaka 2024.
Hizi ndizo hesabu za kisheria na hali halisi hadi itakapotamkwa vinginevyo na vyombo vyenye mamlaka.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.