Isri Mohamed
MAKAMU mwenyekiti Chama Cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu amesema ipo haja ya vyombo vya usalama vya kimataifa kuja kuvichunguza vyombo vya usalama vya hapa nchini ili kubaini chanzo cha matukio ya utekaji na mauaji yanayotokea nchini.
Lissu ameyasema hayo akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwallimu Nyerere Julius ikiwa ni siku chache tangu aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya CHADEMA, Ali Mohamed Kibao kutekwa na kuuawa kikatili.
“Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa ambayo sasa anaiongoza mwenyewe (Rais Samia), hivyo ndio Watuhumiwa wa kwanza, watajichunguzaje?, lini Jeshi na Polisi na Usalama wa Taifa waliwahi kuchunguza chochote cha mambo haya!?, kwa hiyo kutuambia vyombo vya usalama vichunguze, haviwezi vikajichunguza vyenyewe.
“Vyombo vya usalama vinahitaji kuchunguzwa, kusafishwa kuhakikisha kwamba kuna vyombo vya usalama kweli, na hakuna majambazi na vibaraka wanaovaa sare na kulipwa mishahara.
“Lilipoungua jengo la Benki Kuu mwaka fulani walileta wapelelezi kutoka nje, kwa hiyo kwenye hili ambalo vyombo vya ulinzi na usalama ndio watuhumiwa wa kwanza inabidi wachunguzwe na vyombo vinavyoaminika na sio wajichunguze wenyewe huko tutakuwa tunadanganyana” amesema.
Aidha Lissu amezungumza uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu bado kuna vipengele vinahitaji kufanyiwa marekebisho.
“Suala la kwamba tunakwenda kwenye uchaguzi mwezi wa kumi na moja linasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu, tunaweza tusiende kwa sababu walioiba uchaguzi 2019, asilimia mia moja ya wenyeviti wa mitaa na vijiji ni wa CCM, na sio kwa sababu kulikuwa na uchaguzi, ni kwa sababu walifuta uchaguzi” amesema.