Na Isri Mohamed, JamhiriMedia, Dar es Salaam
Mratibu wa Kampeni wa Freeman Mbowe, anayegombea nafasi ya uenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Daniel Naftal amesikitishwa na tuhuma zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu zikimtaja kuwa alikamatwa akitoa rushwa katika uchaguzi wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) uliofanyika siku mbili zilizopita.
Naftal ameyasema hayo mapema leo akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, ambapo amesema Lissu ametoa taarifa za uongo na hata akipewa miaka 100 hawezi kuthibitisha tuhuma hizo.
“Mimi ndiye niliyekuwa mratibu wa kampeni wa Lissu alipogombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema akiwa nje ya nchi, mimi ndiye niliyemchukulia fomu na nikamfanyia kampeni, sasa leo kwa sababu sipo upande wake ndio maana ananituhumu”
Aidha ametolewa ufafanuzi suala la fedha kutumika katika kampeni, ambapo ameweka wazi kuwa hakuna mgombea ambaye hatumii fedha, kwani hata kitendo cha kusafiri tu kwenda kuomba kura kinatumia fedha kwa sababu ya nauli.
Katika hatua nyingine Naftal amewaomba upande wa Lissu kufanya kampeni kwa nidhamu na kuacha tabia ya kutuhumu watu wengine ambao hawapo upande wao.
Uchaguzi wa Chadema unatarajiwa kufanyika Januari 21, 2025 jijini Dar es salaam, ambapo tayari umeshatanguliwa na chaguzi ndogo za Bavicha na Bawacha.