Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu leo Desemba 17, 2024 amechukua fomu ya kugombea uenyekiti wa chama hicho, katika ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Baada ya katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika kumkabidhi fomu hiyo, Lissu ameweka wazi kuwa kijana Sativa ndiye aliyemlipia gharama za kuchukua fomu shilingi milioni moja na laki tano na anatarajia kuirudisha kesho.
Lissu amesema Sativa alimpigia simu jana kuomba kumlipia gharama hiyo ili kumuongezea nguvu akiamini endapo atashinda nafasi hiyo basi atashughulikia masuala ya watu kutekwa na wengine kuuawa kama alivyofanyiwa yeye.
Lissu amedhamiria kuchukua nafasi ya mwenyekiti aliyepo madarakani, Freeman Mbowe ambaye amehudumu katika nafasi hiyo tangu mwaka 2003, takribani miaka ishirini na moja.
Uchaguzi mkuu wa viongozi wa Chadema Unatarajiwa kufanyika Januari 21, 2025.