Hatuhitaji ushahidi mwingine wa kutusaidia kutambua kuwa viongozi wetu ni kama wameshindwa kuliongoza Taifa letu. Rushwa na vurugu za kidini katika nchi yetu zilianza kama cheche za moto. Watawala (si viongozi) wakazipuuza. Wakaziacha, na sasa tunayaona matunda yake.

Viongozi wetu wasivyo na aibu, haitashangaza kuona bado wakisimama majukwaani na kwenye mikutano ya kimataifa na kujinasibu kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani. Tulijidanganya, tumejidanganya na tunataka tuendelee kuwadanganya walimwengu. Ule umoja tulioufaidi kwa kila mmoja wetu kumwona mwenzake ni ndugu, haupo tena.


Wakati mwingine ni vigumu kuamini kama kweli Tanzania ina viongozi wakuu. Matukio ya karibuni ya kuchomwa kwa makanisa na maandamano ya waumini wa Kiislamu pamoja na chokochoko nyingi zinazoendelea nchini, yasingeweza kuwa makubwa kama kweli tungekuwa na viongozi makini na wenye maono.


Fikiria, nchi inakumbwa na zahama, kiongozi mkuu yupo ziarani nje ya nchi. Hili ni jambo linalohitaji mjadala. Katika historia ya Tanzania huru hakujawahi kutokea vurugu kubwa za kuchomwa kwa nyumba za ibada kama tulivyoshuhudia Mbagala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.


Kwa kuwa ni tukio kubwa, la kwanza na la kusikitisha, tulitarajia viongozi wakuu, ikiwezekana, wakatize ziara zao ili warejee kutuliza hali ya mambo. Hilo halikufanyika.


Rais yupo nje ya nchi. Waziri Mkuu yuko ziarani ughaibuni. Makamu wa Rais hajulikani aliko! Spika wa Bunge anafanyiwa ukaguzi wa afya na kisha kuendelea na mikutano ya kimataifa!

 

Wakati Rais anarejea nchini na kupokewa kwa mabomu ya machozi na wanajeshi wenye silaha mitaani, alipaswa kuliona jambo hili kuwa ni zito, na pengine hata kingeitwa kikao cha Baraza la Mawaziri cha dharura. Alipaswa akiingia Ikulu awakute mawaziri wapo ukumbini. Wakutane, wajadili hali hii. Hilo hatukulisikia, na hata lile Baraza/Kamati ya Usalama wa Taifa sidhani kama ilipata muda wa kuketi kujadili hali hii.


Rais Kikwete alipozuru Mbagala alipokewa na waamini waliokuwa wakitokwa na machozi na kupaza sauti. Kilio kile si kwamba kilitokana na kuchomwa kwa makanisa au kuharibiwa kwa mali, la hasha! Kwa mtazamo wangu, kilio kile kilikuwa kama cha kusema, “Baba upo wapi, wakati sisi wanao tunauana?” Kilikuwa kilio kilichoelekezwa kwa baba anayeonekana kutowajibika.


Ndugu zangu, sikutarajia kuiona Tanzania ikibadilika ghafla na kuwa Taifa la aina hii katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Kibaya zaidi, tukio hili limekuja ndani ya wiki ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ambaye kwa hakika amani, upendo na utulivu vilikuwa vitu alivyoviweka mbele.


Matatizo mengi katika nchi hii yanasababishwa na viongozi wetu. Wanachukua muda mrefu sana kushughulikia chokochoko, matokeo yake wanagutuka wakati mambo yakiwa yameshaharibika.  Haya mambo si kwenye vurugu za kidini pekee. Sote ni mashahidi. Juzi tumemsikia Rais Kikwete, akimsukumia Mungu zigo la rushwa ndani ya jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Sijui, lakini inawezekana Rais wetu ana staili ya kuongoza ambayo ni ya kipekee kabisa duniani. Huyu ni Rais na ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CCM. Huyu ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama. Ana nguvu zote za kikatiba. Ameunda vyombo vya kikatiba vya kupambana na rushwa. Mwenyewe anakiri kabisa kuwa rushwa ndani ya jumuiya hizi ni kubwa.

 

Badala ya kuchukua hatua, yeye anabaki kutoa wosia, tena wa kusema, “Kama ni rushwa chukueni, lakini kura muwanyime”. Huyu huyu anatambua kuwa mtoa na mpokea rushwa wote ni wakosaji. Pamoja na kutambua ukweli huo, bado anabariki upokeaji. Wanachama wa CCM walimsikia na kumpuuza vizuri sana! Safari hii rushwa ikawa katika dola za Marekani. Walipokea, lakini je, tuna hakika kuwa waliwanyima kura watoa rushwa hao?

 

Kiongozi wa Taifa ambaye ana vyombo vyote vya intelejensia alipaswa kuwatambua watoa rushwa ni nani, na angeandaa utaratibu wa kuwashughulikia. Kwa mfano, kama alikuwa na hakika kwamba ndani ya UWT fedha zimemwagwa kupindukia, kwanini hakutumia mamlaka ya kikatiba ya kichama, na hata kiserikali, kuufuta uchaguzi huo?


Kama hilo lingekuwa gumu, kwanini hakuwafuta watoa rushwa? Je, tuamini kuwa na yeye alizungumza kutokana na maneno ya “kusikia”, na si kwa hakika na alichokuwa akikitambua? Je, ni haki Rais kutoa kauli za kihisia? Kama si za kihisia, anashindwa nini kuchukua hatua stahiki? Nani mwenye akili timamu anayeweza tena kuogopa karipio lake juu ya rushwa?


Matukio kama haya ya kuviona vitendo vya rushwa na kuvitolea kauli laini namna hii, yanajenga hisia miongoni mwa wananchi kuwa huenda Mwenyekiti ndiye mwenye matatizo zaidi kuliko hata hao wanachama na wawania madaraka, maana haiwezekani kiongozi abaki kukemea rushwa tu kwa maneno bila kuchukua hatua. Sasa tunasubiri sinema nyingine kuanzia leo bungeni Dodoma.

 

Eti taarifa za awali zinasema wale wabunge waliomwaga rushwa nje nje, Kamati ya Ngwilizi haijabaini kama kweli walifanya vitendo hivyo viovu wakati wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini! Nasema haya nayo ni maajabu mengine katika mlolongo wa maajabu ya uongozi katika Tanzania yetu.


Kama kweli Kamati itasema haikubaini vitendo vya rushwa, na kama kweli hiyo ndiyo itakuwa ripoti ya Ngwilizi, ofisa wa cheo cha juu kabisa katika Jeshi lililojipatia sifa ya uadilifu, basi Rais Kikwete ana haki ya kusema tumwachie Mungu!


Nihitimishe kusema kuwa tatizo la uongozi katika Taifa letu sasa chanzo chake ni viongozi legelege tulionao. Vurugu za kidini na kushamiri kwa rushwa ni matokeo ya aina ya viongozi tulio nao.


Napata shida kuamini kuwa kwa uongozi huu huu, na kwa mwenendo huu huu, Watanzania wote – bila kujali tofauti zetu za kiimani – tunapaswa kushiriki kwa pamoja kusali na kuliombea Taifa letu.


Uongozi wa juu katika nchi yetu hauoneshi dalili za kukabiliana na maovu yanayotuvuruga. Maovu makubwa kabisa ninayoyaona ni rushwa na udini.


Pengine Katiba ijayo iwe na kipengele cha kutuwezesha kuwashitaki hawa wanaoliacha Taifa letu litumbukie kwenye shimo la rushwa na udini. Hilo linaweza kuwa funzo kwa wajao baada ya 2015.