Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chama cha Mpira wa Wavu nchini (TAVA) limetangaza rasmi kurejea kwa mzunguko wa pili wa Ligi ya Mpira wa Wavu nchini.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Septemba 25 Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi ya Mpira wa Wavu Tanzania, Riziki Godwin amezungumzia kuhusu urejeo wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo mpaka hatua ya fainali.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa mzunguko wa pili unarejea kufuatia mapumziko ya muda mfupi mara baada ya msimu wa kwanza wa ligi hiyo ambao ulianza rasmi mwezi julai mwaka huu.

“Ligi yetu tulianza rasmi mwezi wa saba ambapo pazia la ligi yetu lilifunguliwa rasmi kisha tukapumzika na sasa tunaenda kwenye mzunguko wa pili ambapo katika mzunguko wa pili utatupa timu ambazo zitafuzu kucheza hatua ya robo fainali na nusu fainali pamoja na timu ambazo zitakuwa zimeondolewa katika mashindano.

Huu mzunguko wa pili tunatarajia uanze siku ya Ijumaa ya Septemba 27 na utatamatika oktoba 4, mwaka huu” alisema mwenyekiti Riziki.

Aidha mwenyekiti huyo wa bodi ya ligi ameongeza kwa kusema kuwa wanatarajia katika mzunguko wa pili wa ligi kutakuwa na ushindani wa hali ya juu kwani ndiyo muda wa vilabu kuonyesha ubora wao ili kujihakikishia kubaki katika ligi na mwishoni kushinda ubingwa huo.

Katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo pia mwenyekiti huyo amebainisha kupatikana kwa wadhamini ambao watashirikiana nao katika kuendesha ligi hiyo kwa mzunguko huo wa pili.

Miongoni mwa wadhamini ambao wametajwa na mwenyekiti huyo ni vodacom Tanzania, natkens company ltd ,damens engineering pamoja nao kampuni ya mshati sports.

Mbali na wadhamini hao pia mwenyekiti Riziki ameutaarifu umma kuwa wanatarajia kupata ugeni katika hatua ya fainali ya ligi hiyo ambapo amethibitisha ujio wa rais wa shirikisho la mchezo wa wavu Afrika Bouchla Hajih ambae atakuwa mgeni rasmi katika fainali ya ligi hiyo ya kitaifa.

Mzunguko wa pili wa ligi hiyo utaanza rasmi ijumaa hii ambapo itashuhuduwa baadhi ya michezo kuendelea katika viwanja vya mwembeyanga , dar es salaam na ligi hiyo kuhitimika rasmi oktoba 4 mwaka huu.