Hadi hivi sasa tunaweza kusema timu ya Simba SC, Yanga SC, Azam, KMC, Lipuli na timu ya  Mtibwa Sugar zimefanikiwa kujitengenezea ‘dunia’ ya peke yao katika Ligi Kuu Tanzania Bara, licha ya ligi hiyo kubakiza mechi chache kabla ya kufikia tamati.

Hali hiyo inatokana na timu kadhaa zinazoshiriki ligi hiyo kutokuwa na uhakika wa kusalia katika ligi hiyo kuu katika msimu ujao wa 2019\2020 kutokana na kuhitaji pointi tatu katika kila mechi dhidi ya wapinzani wao. Timu zote zinataka kujinasua katika mtego wa kushuka daraja.

Licha ya kila timu kupigania nafasi yake, timu ya Mwadui ipo katika nafasi mbaya ikishika nafasi ya 19 katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo wanahitaji kucheza kufa au kupona ili wasalie katika ligi kuu msimu ujao huku wakiwa na alama 38 katika michezo 36 waliyokwisha kucheza.

Timu ya Biashara United kutoka Mara nayo inashika nafasi ya tatu kutoka mwisho, hadi sasa imekusanya pointi 40, na katika mechi zote tatu zilizosalia wanahitaji alama tatu kwa kila mechi dhidi ya wapinzani wao. Kikubwa zaidi Mei 25, mwaka huu timu ya Biashara itaumana na Simba SC, mtanange utakaokuwa wa aina yake kutokana na timu ya Simba kuhitaji ushindi katika mechi hiyo ili kubeba kwa mara nyingine ubingwa wa ligi kuu.

Kuelekea lala salama ya ligi kuu, hadi sasa hakuna uhakika timu itakayotwaa ubingwa huo watapewa kiasi gani cha fedha kutokana na ligi kukosa wadhamini kama ilivyokuwa katika misimu mingine iliyopita, ingawa vilevile ni dhahiri kwamba licha ya kutokuwa na mdhamini, ligi hii imeendea kuwa ya ushindani wa hali ya juu.

Timu zingine ambazo itabidi kila mchezo kwao uwe kama fainali ni JKT Tanzania, Kagera Sugar, Ruvu Shooting, Prisons, Mbao FC, Coastal Union, Alliance, Stand United, Singida United, Mbeya City na timu ya Ndanda.

Bado timu nyingi zimekuwa katika hali ya matumaini kuendelea kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara katika msimu ujao. Timu ya African Lyon, ya jijini Dar es Salaam imeshuka rasmi daraja hadi Ligi Daraja la Kwanza baada ya msimu huu kukamilika, kutokana na matokeo mabovu waliyoyapata.