Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia Arusha

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu leo imetoa hukumu ya mashauri saba yaliyowasilishwa mahakamani hapo kwa nyakati tofauti mojawapo likiwa shauri kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na mashirika mengine ya kutetea haki za binadamu dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika maombi hayo namba 019/2018 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Kituo cha Haki za Binadamu (CHR) pamoja na Taasisi ya Haki za Kibinadamu na Maendeleo katika Afrika (IHRDA) wamedai ukiukwaji wa haki kadhaa za watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) zinazolindwa chini ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Stela Anukam ameiambia Mahakama hiyo kuwa katika shauri hilo mjibu maombi (Jamhuri) aliwasilisha mapingamizi mawili dhidi ya mleta maombi ikieleza kuwa mwaka 2000 ambao unatajwa kufanyika kwa matukio yanayodaiwa ni ukiukwaji wa haki za watu wenye ulemavu wa ngozi nchi ya Tanzania ilikuwa haijawa mwanachama wa Itifaki.

Mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo na kueleza kuwa madai ya ukiukwaji huo yalitokea kati ya mwaka 2000 na 2016 ndani ya muda ambao mjibu maombi alikuwa ni mwanachama wa Itifaki na kwamba Mahakama ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza maombi hayo.

Pingamizi la pili wajibu maombi waliitaka mahakama kutupilia mbali shauri hilo kwa kuwa waleta maombi hawakupitia ngazi za chini za mahakama za ndani na badala yake walipeleka shauri hilo moja kwa moja mahakamani hapo.

Kwa upande wa pingamizi hilo mahakama imeeleza kuwa imepitia Sheria na kugundua kuwa imekataza mashirika binafsi kupeleka shauri mahakamani yenye maslahi ya umma hivyo mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo na kutangaza kuwa maombi hayo yamezingatia Kanuni ya 50(2)(e) ya Kanuni hizo.

Mahakama imeeleza kuwa waombaji walikuwa na madai ya ukiukaji wa Vifungu 2, 4, 5 na 7 vya Mkataba, Kifungu cha 7 cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) na Kifungu cha 16 na 29 cha Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto.

Baada ya Mahakama kusikiliza pande zote ilijiridhisha kuwa mjibu maombi alikiuka haki za watu wenye ualbino chini ya Vifungu 2, 4 5, 7 vya Mkataba na Vifungu 16 na 29 vya Mkataba wa Watoto.

Mahakama pia imebainisha kuwa hata kama mjibu maombi amefanya baadhi ya hatua za kukabiliana na ubaguzi unaofanywa dhidi ya watu wenye ualbino lakini juhudi hizo zimeshindwa kufikia viwango vya sheria za kimataifa za haki za binadamu kwa hiyo mjibu maombi amepatikana na hatia ya ukiukwaji wa haki za watu wenye ualbino.

Mahakama imebainisha kuwa pamoja na kwamba mjibu maombi alichukua baadhi ya hatua za kukabiliana na mauaji hayo kwa kuunda kikosi maalum cha kuchunguza na kuendesha kesi zinazohusu mauaji hayo lakini haikuonyesha ufanisi wa kazi hiyo maalum.

Zaidi ya hayo, Mahakama imeeleza kuwa mjibu maombi ameshindwa kuchunguza, kuwashtaki na kuwaadhibu wahusika wa mauaji ya watu wenye ualbino hivyo amekiuka haki ya kuishi ya watu hao.

Mahakama pia imegundua kuwa mfumo wa elimu unaotolewa haukidhi haki za watu wenye ulemavu wa ngozi kwa mfano watoto wenye ualbino hawakupewa vifaa saidizi kama vile miwani hivyo mahakama imebaini ukiukwaji wa haki ya elimu.

Mahakama pia imebainisha kuwa haki ya afya inapaswa kupatikana, kukubalika na kwa ubora unaokubalika. Katika suala hilo Mahakama imegundua kuwa huduma ya afya ya msingi haikupatikana, kufikiwa au kukubalika kwa watu wenye ulemavu wa ngozi hasa kwa sababu ya mitazamo ya kibaguzi ambayo inaendelea na hivyo kubaini ukiukwaji.

Hivyo Mahakama imemuamuru mjibu maombi kuanzisha mfuko wa fidia kiasi cha Shilingi Milioni Kumi za Kitanzania (TZS 10,000,000) kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa fidia.

Kuhusu fidia zisizo za kifedha Mahakama imemuamuru mjibu maombi kurekebisha sheria zilizopo ili kuharamisha na kuadhibu vitendo vya unyanyasaji ambavyo vinalenga watu wenye ulemavu wa ngozi.

Mahakama pia imemuamuru mjibu maombi kufanya marekebisho ya Sheria ya Uchawi ya mwaka 1928, Sura ya 18 ya Sheria za Tanzania, ili kuweka wazi utata unaohusiana na uchawi na tiba asili.

Aidha mjibu maombi ameamriwa kuchapisha hukumu hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu tarehe ya kutangazwa kwa hukumu hiyo kwenye tovuti za Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mahakama na Wizara ya Katiba na Sheria ili kuhakikisha kuwa andiko la Hukumu hiyo linaendelea kupatikana kwa angalau mwaka mmoja baada ya kutangazwa.

Mjibu maombi pia ameamriwa kuwasilisha ndani ya miaka miwili taarifa ya hali ya utekelezaji wa uamuzi huo na endapo hukumu hiyo haitatekelezwa kikamilifu ndani ya miaka mitatu Mahakama itafanya usikilizwaji wa utekelezaji.

Upande wa waleta maombi uliwakilishwa na Mawakili Fulgence Massawe, Chipo Rushiwaya na Michael Nyarko huku upande wa wajibu maombi ukiwakilishwa na Mawakili wa serikali Hangi Chang’a, Narindwa Sekimanga, Vivian Method na Daniel Nyakiha.

Hukumu nyingine sita zilizosomwa Mahakama hapo ni pamoja na hukumu mbili zinazotokana na mashauri yaliyofunguliwa na wananchi dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hukumu mbili kati ya wananchi dhidi ya nchi ya Cote d’lvoire (Ivory Coast), hukumu moja kati ya mwananchi dhidi ya nchi ya Benin na hukumu nyingine moja kati ya mwananchi dhidi ya nchi ya Tunisia.

Mashauri hayo yalikuwa chini ya majaji kumi na moja ambao Imani Daud Aboud ambaye ni Rais wa Mahakama hiyo, Modibo Sacko Makamu wa Rais, Jaji Ben Kioko, Jaji RafaĆ¢ Ben Achour, Jaji Suzanne Mengue, Jaji Tujilane R. Chizumila, Jaji Chafika Bensaoula, Jaji Blaise Tchikaya, Jaji Stella I. Anukam, Jaji Dumisa B. Ntsebeza, Jaji Dennis D. Adjei pamoja pamoja na Msajili wa mahakama hiyo Dkt Robert Eno.