MKURUGENZI wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga (Kulia)

 

MKURUGENZI wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga, amesema kuwa kituo hicho kimefuatilia kwa ukaribu uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 ulifanyika Novemba 26 mwaka huu, katika halmashauri 36 kwenye mikoa 19 nchini.

Katika uchaguzi huo tume ya haki za binadamu imebaini matukio mbalimbali ya uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, vikiwemo vitendo vya matumizi mabaya ya nguvu na vyombo vya dola, matukio ya watu kutekwa, kwa lengo la kuharibu uchaguzi na kuwatia hofu wapiga kura.

Vitendo hivi vimeripotiwa kufanywa na vyombo vya dola, watu wasiojulikana na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa vyama vya siasa, kikiwemo CCM, Chadema, na vyama vingine vya upinzani.

“Imeripotiwa kwamba kuna matukio ya watu kutekwa na kupigwa katika kata ya Kitwilu mkoani Iringa, na vijana wanaosadikika kuwa ni vijana wa kikosi cha ulinzi cha CCM. Waliwavamia na kuwateka wanachama wanaosemekana kuwa ni wa CHADEMA, ndugu Elizabeth Nyenza na Martha Francis ambao walifika kupiga kura na kuwanyang’anya simu na kuwatelekeza katika msitu wa Kilolo hadi walipopata msaada wa wapita njia.

“Hayo ni pamoja na kushambuliwa kwa gari la Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Dadi Igogo, huku jeshi la polisi likimkamata na kumshikilia Meya wa manispaa hiyo, Alex Kimbe.

Wakati huo huo mfuasi wa CCM katika jimbo la Kawe, alivamiwa na kujeruhiwa na watu wanaosadikika kuwa ni wafuasi wa Chadema, hatimaye kulazwa katika hospitali ya Rabisia, Tegeta jijini Dar es Salaam.

Pia katika kata ya Makiba, wakala wa Chadema, Rashid Jumanne, na mwenyekiti wa Chadema tawi la Valeska, Nison Mbise, walijeruhiwa vibaya asubuhi wakati wanaelekea katika vituo vya kupigia kura na watu wasiojulikana.
Aidha katibu wa CCM, wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, amelazwa hospitalini baada ya kushambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, alipokuwa njiani akiwasindikiza mawakala wake kwenda kituoni kwa ajili ya kusimamia zoezi la upigaji kura.

Vitendo hivyo pia vimeripotiwa katika Kata ya Nyabubinza, Nyasa na Simiyu. Mawakala katika vituo vinane kati ya vituo 13, walikamatwa na jeshi la polisi, akiwemo diwani wa Chadema, Zakayo Chacha Wangwe.

“Pia kuna matukio yameripotiwa kuhusu viongozi wa vyama vya siasa na mawakala wa vyama kukamatwa akiwemo, katibu wa Chadema wilaya ya Ubungo ambaye pia ni mratibu mkuu wa uchaguzi wa kata ya Saranga, Perfect Mwasiela, aliyekamatwa Novemba 25, pamoja na Mbunge Suzan Kiwanga aliyekamatwa na kuwekwa ndani kwa siku nne.

Vilevile ni pamoja na kukamatwa kwa Meya wa Ubungo ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Ubungo, Boniface Jacob, siku ya uchaguzi ambaye pia ndiye aliyeapishwa kuwa wakala mkuu kwenye majumuisho ya kura za mwisho katika kata.

“Jeshi la polisi halijasema hadi sasa sababu za kuwakamata na kuwashikilia watu hao,” amesema Anna Henga.