Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Tanzania kimesema kitazidi kumbana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, afute kauli yake sambamba na kuwaomba radhi Watanzania.
Akizungumza bungeni mjini Dodoma Juni 20, mwaka huu, Pinda alisema, “Na mimi nasema wanaokaidi amri halali ya Jeshi la Polisi muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine ya kupambana na wakaidi zaidi ya kuwapiga.”
Waziri Pinda alitamka maneno hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya matukio ya vurugu yanayotokea mara kwa mara, hususan katika mikoa ya Mtwara na Arusha.
Kufuatia kauli hiyo, LHRC imetangaza matamko ya kumtaka Waziri Mkuu huyo kufuta kauli yake hiyo, kuwaomba radhi Watanzania na kulielekeza Jeshi la Polisi kufuata sheria na taratibu zilizopo wakati wa kutekeleza majukumu ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
Katika mahojiano na JAMHURI Dar es Salaam hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Helen Kijo-Bisimba, amesema kituo hicho kimeshirikiana na baadhi ya Watanzania na asasi za kiraia kutoa matamko hayo.
“Mpaka sasa tumekusanya saini 1,000 (za Watanzania) kudai kauli hii ifutwe ili kulinda maisha ya Watanzania,” amesisitiza Dk. Kijo-Bisimba. Mahojiano zaidi kati ya Dk. Kijo-Bisimba na JAMHURI yamefanyika kama ifuatavyo:
JAMHURI: Dk. Kijo-Bisimba, mojawapo ya matamko yenu ni kumtaka Pinda alielekeze Jeshi la Polisi kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. Unadhani jeshi hilo lina haja ya kusubiri kuelekezwa na Waziri Mkuu ndipo litekeleze majukumu yake kwa kufuata sheria na taratibu za nchi?
Dk. Kijo-Bisimba: Hapana, Jeshi la Polisi halipaswi kufuata amri ambayo si halali, ingawa uzoefu unaonesha kuwa matamko kama lile la Mheshimiwa Pinda hutekelezwa.
JAMHURI: Mmeeleza kushtushwa na kutofurahishwa na kauli hiyo ya Waziri Mkuu inayowataka polisi kuwapiga wanaokaidi kutii sheria. Je, kwa upande mwingine, mna ujumbe gani kwa raia wanaokaidi kutii sheria bila shuruti?
Dk. Kijo-Bisimba: Kila raia hapaswi kukaidi kutii sheria, raia wanapaswa kutii mamlaka na sheria. Lakini wanaokaidi kutii sheria washughulikiwe kwa mujibu wa sheria. Sheria ichukue mkondo wake kwa wasioitii, si kusema piga tu. Adhabu [za kisheria] ziko nyingi, kuna kifungo na kutoza faini.
JAMHURI: Je, kuna tukio lolote la unyanyasaji lililotekelezwa na Jeshi la Polisi dhidi ya raia kufuatia kauli hiyo ya Waziri Mkuu?
Dk. Kijo-Bisimba: Hapana, ila uzoefu unaonesha kwamba raia wamekuwa wakiuawa wakiwa mikononi mwa polisi katika maeneo mbalimbali nchini.
JAMHURI: Mmetumia mbinu gani kukusanya saini za watu kwa ajili ya kumtaka Waziri Mkuu afute tamko lake?
Dk. Kijo-Bisimba: Tumetumia mtandao [wa Internet] na fomu kutuma taarifa na kukusanya saini.
JAMHURI: Unadhani kweli Waziri Mkuu Pinda atajibu matamko yenu kwa kufuta kauli mnayoilalamikia?
Dk. Kijo-Bisimba: Sisi tunaamini atafuta kauli ile, asipoifuta tutaangalia hatua ya kuchukua zaidi ikiwa ni pamoja na kumpelekea barua rasmi. Kauli ile ni kinyume cha utawala wa kisheria, na tuna wasiwasi kuwa inaweza kujenga uhasama baina ya wananchi na polisi.
LHRC imetangaza msimamo wake huo siku chache baada ya baadhi ya Watanzania wa kada mbalimbali kujitokeza kukemea kauli hiyo ya Waziri Mkuu na wengine kuiunga mkono.