Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia, Dar es Salaam

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa rai kwa Serikali kupunguza gharama za uendeshaji wa nchi ikiwemo maisha ya kifahari kwa viongozi wa kitaifa huku wananchi wakilia ukali wa hali ngumu kutokana na baadhi ya bidhaa kuongezewa kodi .

Rai hiyo imetolewa leo Juni 26,2024 Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha sheria na haki za binadamu Wakili Fulgence Masawe wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema licha ya kuwa na bajeti kubwa ya Trilion 49.35 ya mwaka 2024/2025 na kati ya fedha hiyo wameanisha kupunguza deni la nchi na kutekeleza miradi mikubwa huku vyanzo vya mapato vikiwa ni vichache na baadhi ya Mamlaka za Serikali zikifanya vibaya katika matumizi ya fedha kwa mujibu wa ripoti ya mkaguzi wa hesabu za serikali CAG .

“LHRC tunapendekeza Serikali kupunguza kodi ya ongezeko la thamani kwenye bidhaa zote zenye uhitaji mkubwa hasa matumizi ya nyumbani ikiwemo bidhaa za vyakula gesi ya kupikia ili kupunguza ukali wa maisha kwani ni kweli kwamba katika kipindi cha miaka miwili mfululizo kutokana na sababu mbalimbali za siasa za ulimwenguni gharama za maisha zilipanda ikilinganishwa na kipindi kabla ya miaka miwili ” amesema Wakili Masawe.

Wakili Masawe amefafanua kuhusu sheria ya ushuru wa bidhaa katika sura ya 147 ya bajeti amesema marekebisho yaliyopendekezwa kwenye sheria ya ushuru wa bidhaa sura hiyo yalijumuisha kupunguza ushuru baadhi ya bidhaa ikiwemo maji ya kunywa yaliyosindikwa nchini kutoka Tsh 63.8 hadi Tsh 56 kwa lita na kutoza kwa lita ya Un-denetured Ethyl alcohol yenye kilevi cha asilimia 80 au zaidi kutoka nje huku asilimia 10 ya ushuru kwenye thamani ya dau la kamari na ada ya matangazo ya michezo ya kubahatisha na bahati nasibu ya Taifa .

Amesema kwa mujibu wa bajeti hiyo vyanzo vya mapato vimeendelea kuwa vilevile huku wanaochangia bajeti kwa njia ya kodi ni wananchi wachache hivyo kuna haja ya serikali kubuni vyanzo vipya vya mapato, akitolea mfano mchango wa halmashauri kwenye bajeti yetu ni mdogo sana, halmashauri nazo zimeshindwa kubuni vyanzo vipya mfano kupima ardhi kwa wingi na kumilikisha kwa wakati hati za wananchi badala yake wanawapa tenda kampuni binafsi na wamekuwa wakiwatoza ghafama kubwa .

Aidha ulinganifau wa bajeti kwa kuangalia nchi za Afrika Mashariki Tanzania ndiyo nchi ya tatu kwa ukubwa na ina watu milioni 65.5 na bajeti yake ni Trilioni 49.35 ikifutiwa na Kenya kuwa na watu milioni 54.03 na bajeti yake kuwa Trilioni 77 Uganda milioni 47.25 na bajeti yake kuwa Trilioni 50.