Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dar es Salaam
Kituo cha sheria na haki za binaadamu(LHRC) kimeahidi kufanyakazi na Chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari(JOWUTA) katika kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu sheria za kazi na sheria zinazohusu sekta ya habari.
Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho LHRC,Wakili Fulgence Massawe ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na viongozi wa JOWUTA makao makuu ya LHRC.

Wakili Massawe alisema LHRC ni mdau mkubwa wa wanahabari ma tasnia ya habari hivyo wakati wote wapo tayari kufanyakazi na JOWUTA kusaidia kuboresha tasnia ya habari nchini.
“Tunajua changamoto katika sekta ya habari,ikiwepo asilimia zaidi ya 80 ya wanahabari kutokuwa na mikataba wala ajira lakini pia tunajua uchumi mbaya wa vyombo vya habari”alisema
Hata hivyo alisema uchumi mbaya wa vyombo vya habari sio kigezo cha kushindwa kuheshimiwa sheria za kazi zilizopo nchini.
“Tutashirikiana kutoa elimu kwa wanahabari,waajiri na wadau ili kuona ni jinsi gani waandishi wanafanyakazi kwa kuzingatia maadili lakini wanakuwa na uhuru wa kufanyakazi na katika mazingira bora”alisema.

Awali Mwenyekiti wa Taifa wa JOWUTA Mussa Juma alimweleza Wakili Massawe JOWUTA inahitaji ushirikiano na wadau mbalimbali katika kutetea maslahi bora ya waandishi wa habari.
“Bado kuna waajiri wengi hawalipi wanahabari na wala hawatoi mikataba jambo ambalo ni kinyume cha sheria za kazi hivyo JOWUTA itaendelea kupigania haki za wanahabari ikiwepo mazingira bora ya kazi”alisema
Alisema tayari JOWUTA imesaidia baadhi ya wanahabari kwenda mahakamani kudai stahiki zao lakini bado changamoto ni kubwa.
“Tumekuja hapa kujadiliana juu ya ushirikiano wetu lakini pia kama viongozi wapya wa JOWUTA kujitambulisha kwa wadau”alisema
Juma ambaye pia ni mjumbe wa kamati tendaji wa shirikisho la waandishi wa habari Afrika Mashariki na Kati alitaka LHRC kufanyakazi na JOWUTA hasa kuelekea katika chaguzi ambapo wanahabari wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi.
Awali Katibu Mkuu wa JOWUTA Seleman Msuya alieleza JOWUTA ndio chama pekee kisheria nchini chenye jukumu la kulinda na kutetea maslahi bora ya kazi kwa waandishi na mazingira bora ya kazi.
“Sisi ndio tunaweza kuwapeleka waajiri mahakamani na tunafanya hivyo lakini bado changamoto ni nyingi ndio sababu tunaomba ushirikiano na wadau wakiwepo LHRC.

Katika ziara hiyo pia mweka hazina wa JOWUTA Lucy Ngoi alishiriki na kueleza kutokana na hali ngumu za kimaisha kwa waandishi wengi hata uchangiaji wa ada za cha imekuwa ni tatizo.
Viongozi wa JOWUTA bado wanaendelea na ziara kwa wadau mbalimbali kuelekea uzinduzi wa mafunzo ya wanahabari kuhusiana na kuripoti vyema uchaguzi mkuu lakino wakiwa salama ikiwepo kutonyanyaswa na vyombo vya dola ama vyama vya siasa.

.