Na Isri Mohamed

KLABU ya Coastal Union imetangaza kuachana na mlinda lango wao, Ley Matampi Raia wa Congo kwa makubaliano ya pande zote mbili.

Matampi alijiunga na Wagosi wa Kaya mnamo Agosti 2023, akiwa na miaka 34 na kuonesha kiwango kizuri mpaka kufikia hatua ya kuchukua tuzo ya kipa bora wa msimu uliopita (2023 – 2024 ), akiuvunja ufalme wa Djigui Diarra aliyetawala kwa misimu miwili mfululizo.

Mashabiki na wadau wengi wa soka wameonesha kushangazwa na uamuzi wa Coast kumuacha Matampi, lakini wenyewe wanasema alikua ana makosa mengi ambayo yameigharimu timu katika mechi za msimu huu.

Kwa upande wake Matampi anasema alikuwa anawadai waajiri wake hao mishahara ya miezi mitatu.

Akiwa na uzi wa Coastal Union ambao kwa sasa wamehamia mkoani Arusha, Matampi ameiwezesha kumaliza msimu uliopita wakiwa nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu Tanzania bara, nafasi iliyowapa tiketi ya kucheza michuno ya kombe la shirikisho barani Afrika.

Kabla ya kujiunga na Coastal Union, Matampi amewahi kuzichezea klabu za TP Mazembe, Kabuscorp na Al Ansar.