NA MOSHY KIYUNGI
Hapana shaka wadau wa muziki wanazikumbuka baadhi ya nyimbo
mashuhuri zilizotamba wakati huo za Embakasi na Nyakokonya,
zilizopigwa na bendi ya Orchestra Les Mangelepa.
Les Mangelepa ilikuwa na wanamuziki wengi wao wakiwa ni raia toka
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ilikuwa na makazi yake katika jiji la
Naiorbi nchini Kenya.
Bendi hiyo ilitikisa vilivyo sehemu nyingi za Afrika Mashariki, ilianzishwa
rasmi mwaka 1976 wakati vijana watano walipojiunga kuanzisha katika
jiji la Nairobi, nchini Kenya.
Vijana hao walikuwa wakipiga muziki katika bendi ya Baba Gaston,
walipogawanyika, baadhi yao ndio hao waliounda kikosi cha Les
Mangelepa wakiongozwa na Bwammy Walumona ‘La Capitale’.
Inaelezwa kuwa kifo cha bendi ya Baba Gaston iliyokuwa ikiongozwa
na Baba Nationale Ilunga wa Ilunga, kilisababishwa na kukimbiwa na
vijana hao waliokuwa tegemeo katika bendi yao.
Bendi Les Mangelepa ilijipatia umaarufu mkubwa kati ya miaka ya 1970
na 1980 baada ya kufyatua nyimbo zilizowakuna wapenzi wa muziki wa
dansi katika nchi za Afrika ya Mashariki na Kati.
Baadhi ya nyimbo hizo zilikuwa ni; Embakasi, Maindusa, Walter, Safari
ya Mangelepa, Odesia, Dracula, Saad na Maboko Pamba.
Les Mangelepa ilileta ushindani mkubwa katika jiji hilo la Nairobi, dhidi
ya bendi kubwa zilizokuwemo jijini humo.
Baadhi ya bendi hizo ni pamoja na Les Knoirs, Les Wanyika, Orchestra
Shikashika, Super Mazembe, Baba Gaston na nyingine nyingi.
Baada ya ‘kushiba’ umaarufu, baadaye iliingiwa na mtafaruku mkubwa
wa uongozi.
Magelepa ikaamua kubadili uongozi, ambapo Kabila Kabanze Eveny

akawa kiongozi wa bendi.
Bendi hiyo ikarejea kwenye umaarufu wake kwa kupiga muziki wa
Kikongo, kama walivyokuwa Super Mazembe na Baba Gaston.
Mwaka 1986, Bammy Walumona aliondoka katika bendi hiyo na
kuamua kuokoka, lakini aliiacha Mangelepa ikiwa imesheheni
wanamuziki wengi wenye vipaji mbalimbali.
Wanamuziki hao walitunga na kuimba nyimbo nyingi zilizokuwa kivutio
cha mashabiki na wapenzi wa muziki, ikanokana kama haina mpinzani
miongoni wa bendi zilizokuwa zikipiga katika jiji hilo.
Wanamuziki waliokuwa wakiunda kikosi cha Les Mangelepa
kiliwajumuisha kina Bwami Walumona ‘Le Capitale’ ambaye ndiye
aliyekuwa kiongozi wa bendi hiyo.
Kabila Kabanze ‘Evani’ aliongoza safu ya waimbaji wakati Kalenga
Nzaazi ‘Vivi,’ Lutulu Kaniki ‘Macky’ na Babibanga Watshilumba ‘Kai’
walikuwa waimbaji mashuhuri wakati huo. Kai pia alikuwa ni mpuliza
tarumbeta na turombone.
Kwenye drums na gitaa la besi alipiga Kasongo Fundi Petit Jean,
Lukangika Maindusa ‘Moustano’ alikuwa akipiga gitaa la solo na rhythm
wakati Mwepe Mutshi ‘Cavalou’ naye alisimama kwenye tarumbeta.
Mwanamuziki mwingine alikuwa Lumwanga Maoyombo ‘Ambassador’
aliyekuwa akiliungurumisha gitaa zito la besi na rhythm. Drums
ziligongwa na Mukala wa Mulumba ‘Bebe’, naye Tabu Ngongo
Ildephonce ‘Super Sax’ na Tshimanga Zadios walikuwa wakipuliza
saxophone.
Kundi hilo machachari pia lilikuwa na wanamuziki wengine kina Twikale
wa Twikale na Kabe Kimambe ‘Elombe’ walikuwa wakibofya kinanda na
kupiga gitaa la solo. Kabebe Mukangwa ‘Picolo’ na Tambwe Lokasa
walikuwa akiliungurumisha gitaa zito la besi.
Tumba ziligongwa na Mukala Kanyinda ‘Coco’ ambaye alikuwa na
uwezo wa kupuliza hata saxophone.
Mwanamuziki mwingine alikuwani Padd ‘Ma Wauwau’ aliyekuwa
akipuliza saxophone.
Tungo za nyimbo za Mangelepa zilishika chati katika miji mingi hapa
nchini hususan kwenye kumbi za burudani na maeneo ya starehe na
mabaa.
Wimbo wa ‘Embakasi’ na ‘Kanemo’ zilitungwa na mwanamuziki

Kalenga Nzaazi ‘Vivi’, hadi leo ukipigwa popote watu wengi hufuatilia
neno kwa neno.
Nyimbo za ‘Mimba’ na ‘Nyako Konya’ zilizotungwa na mwanamuziki
Badi wa Tshilumba nazo zinaendelea kukonga nyoyo za wapenzi wa
muziki hadi leo.
Wimbo wa ‘Maindusa’ ulioimbwa na kupigwa kwa umahiri mkubwa ni
utunzi wake Lukangila Maindusa wakati wimbo wa ‘Mimba’ na ‘Malawi’
zilitungwa na mwanamuziki Kabila Kabanze ‘Evani’ wimbo ambao
huanza kwa sauti ya juu sana wa ‘Walter’ ni utunzi wake Badi Banga wa
Tshilumba wakati Mangelepa baadaye wakaftyatua albamu nyingine
yenye nembo ya Madima ikiwa imesheheni nyimbo za ‘Madina’,
‘N’kimba’, ‘Lolo Mukena’ na ‘Kawala’.
Bendi hiyo itakumbukwa na wapemnzi wa muziki wa nchini Zambia
ambako ilifanya ziara ikitoa burudani ikiwa humo na baada ya kurejea
wakatoka na vibao vikali vya ‘Dajala’, ‘Saad’, ‘Tshibola’, ‘Mankwazi’ na
‘Safari ya Zambia’ wimbo ambao ulipigwa kwa ala tupu.
Mwaka 1978, Mangelepa walirekodi nyimbo zilizokuwa na sehemu ya
kwanza na ya pili za ‘Walter’, ‘Pambana pambana’, ‘Maboko Pamba’
pamoja na ‘Haleluye’. Nyingine zilikuwa ni ‘Dracula’, ‘Mangelepa
Kamili’, ‘Kizunguzungu’, ‘Suzanne’ na ‘Trouble’.
Bendi ya Les Mangelepa haipo tena katika ulimwengu wa muziki, huku
baadhi ya wanamuziki wake wametangulia mbele ya haki, wengine
wameokoka na kuacha kabisa kupiga muziki wa kidunia.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba 0784331200