Jina la Tanzania leo limetimiza miaka 55. Kabla ya tarehe 29 Oktoba 2019, Tanzania ilijulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ni mwanafunzi wa miaka 18 wakati huo, Mohammed Iqbal Dar, aliyebuni jina hilo katika shindano la kubuni jina jipya, jina lililotuunganisha na kutugawanya.

Inafahamika kuwa si wote waliyofurahia Muungano. Nimehadithiwa na wazee waliyoshuhudia siku hiyo wakisema kuwa kuna watu waliangua kilio.

Si sahihi kusema kuwa sababu zote zinazotetea kuvunjika kwa Muungano zipuuzwe kwa kukosa mantiki tunapozilinganisha na zile zinazotetea kuendeleza Muungano.

Mathalani, tarehe ya leo pia mwaka 1961 Syria ilijitoa kwenye muungano wake na Misri uliyodumu miaka mitatu tu. Mbegu za kuvunjika kwa muungano huo zilipandwa mapema kwenye makubaliano kati ya Syria na Misri. Ingawa wazo la muungano lilianzishwa na viongozi wa Syria, kiongozi wa Misri Gamal Abdel Nasser alilikubali na kubuni mkataba wa muungano ambao uliipunguzia Syria ushawishi na usawa ndani ya Jamhuri mpya iliyoundwa tarehe 1 Februari 1958.

Nasser alisisitiza kupitishwa kwa kura ya maoni, kuvunjwa kwa vyama vyote vya siasa, na kuwepo marufuku ya wanajeshi kujihusisha na siasa.

Aidha, baada ya muungano kuanza nafasi muhimu za kisiasa, kiutawala, na kijeshi zilishikwa na raia wa Misri. Bunge jipya la wajumbe 600 lilitoa nafasi 400 kwa Misri na 200 tu kwa Syria. Muungano ukaonekana na wa-Syria kuwa siyo wa nchi mbili bali uliyodhibitiwa na Misri pekee. Baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Syria ya 28 Septemba 1961 Syria ikajitoa kwenye muungano huo.

Kwa upande wetu yapo yanayofanana na yaliyotokea kwa Misri na Syria. Muungano ulipendekezwa na Sheikh Abeid Amani Karume na kukubaliwa na Mwalimu Julius Nyerere. Tanganyika kwa Zanzibar, kama Misri kwa Syria, ndiyo ilikuwa nchi kubwa zaidi na hali hii imeonekana kuhatarisha maslahi ya nchi ndogo ndani ya muungano.

Ni Mwalimu Nyerere, kama Nasser, anayepata shutuma zaidi kwa kuweka ndani ya hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar vipengele ambavyo baadhi ya watu wanasema vinainyima Zanzibar uhuru wake kamili.

Bila kuingia kwenye mjadala huo tunaweza kusema kuwa zipo tofauti kati ya Misri/Syria na Tanganyika/Unguja. Tofauti kubwa ni kuwa, pamoja na changamoto zilizopo, sisi muungano wetu bado unadumu. 

Sisi hatuna bunge moja tu: tuna Bunge la Muungano lenye jukumu la kusimamia masuala yanayohusu Muungano pekee, na kuna Baraza la Wawakilishi lenye kusimamia masuala ya Zanzibar pekee.

Zaidi ya hapo tofauti zetu tunazijadili na baadhi zimepata suluhu, ingawa wapo wanaosema kuwa majadiliano yanachukua muda mrefu sana.

Kusema kuwa Muungano unadumu haina maana kuwa hawakosekani watu ambao wangepewa nyenzo wangeukongoa haraka tu, na bila kusita.

Baadhi yao hujenga hoja ambazo zinatujaza maswali kuliko kutoa majibu. Wakati wa mijadala ya Bunge la Katiba, nilishangaa kusikia baadhi ya wabunge wa Bunge la Muungano wakihoji uhalali wa Muungano, wakiashiria kuwa Tanzania yenyewe haipaswi kuwepo.

Mbunge wa Butiama hakuwa kwenye kundi hilo, lakini angekuwa mmojawapo ningetaka anipe ufafanuzi iwapo Muungano ni batili, yeye anapata wapi ujasiri wa kupaza sauti ndani ya mhimili uliyoundwa na Muungano batili? Kama Muungano ni batili, Bunge la Muungano ni batili, mchakato wa uchaguzi wake yeye ni batili, na – muhimu kuliko yote – ubunge wake ni batili.

Mtu atayefikia hatua ya kutambua hali hiyo ataondoka kimya kimya Bungeni – kwa sababu hata kudai ajiuzulu itakuwa kumlazimisha atoe heshima kwa taasisi ambayo haipaswi kuwepo kikatiba. Tutatarajia akaanzishe utaratibu wake mpya wa kuhoji uwepo wa Muungano.

Lakini tatizo halitaishia hapo. Ataanzaje kutumia vyombo vya sheria batili zilizopitishwa na bunge batili kuanza kudai ukiukwaji wa mchakato batili wa kikatiba uliyounda Tanzania?

Kuna kipindi baada ya kuvunjika kwa muungano wa nchi za Muungano wa Kisoshalisti wa Kisovieti kilichoibua nchi nyingi mpya ambazo hazikuwa tena chini ya ile Urusi ya zamani. Zama hizo, kusambaratika kwa nchi kulionekana kuwa suala linalojenga demokrasia na kupanua uhuru wa watu kujiamulia masuala yao.

Bila shaka, katika nchi zile zilizokuwa chini ya Urusi ya zamani, demokrasia imepanuka kwa kiasi fulani. Lakini nina hofu kuwa wale walioanza kupata uwezo wa kutambua matukio muhimu ya ulimwengu kwenye mazingira kama hayo wamegandishwa mawazo wakiamini kuwa kila tatizo la kutoelewana dawa yake ni moja tu: kutengana. 

Uamuzi wa Uingereza kujitoa kwenye Jumuiya ya Ulaya na matatizo yanayojitokeza ya kukamilisha mchakato wa kujitoa ni ishara kuwa kinachoaminiwa kuwa jawabu kinaweza kuwa chanzo cha matatizo mengine mengi.

Kama ilivyo kweli kuwa wapo wanaodhani kutengana ni jawabu, tupo wengi tunaoamini umoja ni silaha inayolinda uhuru wa nchi moja moja changa wa kuhimili nguvu za kiuchumi za mataifa makubwa. Labda na sisi tuna kasoro ya kukua kwenye enzi ambapo umoja lilikuwa somo tulilosikia kila mara, na likashika mizizi na kuimarisha imani zetu kuwa linajibu matatizo mengi ya msingi yanayokabili nchi changa.

Kwenye zama hizi za kudumisha uhuru wa mawazo tunakubali kutofautiana na wenye mawazo tofauti lakini hatuachi kuwashangaa wanaochochea kutengana.

Barua pepe: [email protected]