Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kanda ya Victoria ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Ezekia Wenje amezungumza na wanahabari mapema leo Januari 16, 2025 jijini Dar es Salaam, kujibu tuhuma mbalimbali zilizotolewa dhidi yake.

Wenje ameleezea kwanini amejiondoa kwenye kumuunga mkono Tundu Lissu katika uchaguzi mkuu wa CHADEMA unaotarajiwa kufanyika Januari 21, 2025.

“Ni kweli nimi nilikuwa timu Lissu, sasa kwanini nimejiondoa, Mwenyekiti Freeman Mbowe alipokuwa gerezani kwa kesi ya ugaidi, Lema na Lissu walianzisha kampeni ya ‘Join the Chain’, wakachangisha fedha kwa ajili ya kuandaa mkutano wa Baraza Kuu na mkutano mkuu.

“Walijua mwenyekiti Mbowe hawezi kutoka gerezani kwa sababu ana kesi ya ugaidi, hivyo ile kampeni yao ililenga kumpindua Mbowe ili Lissu awe mwenyekiti na Msigwa awe Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, nilivyogundua hivyo nikajiondoa, nilikataa uasi” amesema.

Wenje amesema fedha hizo zilikusanywa kupitia akaunti za CHADEMA, wanachama wakijua ni kwa ajili ya mkutano mkuu, lakini nyuma ya pazia malengo ya Lema na Msigwa yalikuwa ni kufanya mapinduzi.