Na Isri Mohamed, JamhiriMedia, Dar es Salaam
Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA), Godbless Lema, ametangaza rasmi kumuunga mkono Tundu Lissu anayegombea nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho na John Heche anayegombea makamu mwenyekiti.
Akizungumza na wanahabari leo Januari 15, 2025, jijini Dar es Salaam, Lema amesema licha ya kuwa mwenyekiti aliyepo madarakani, Freeman Mbowe ni kaka yake lakini anamuomba apumzike na amuachie Lissu nafasi hiyo.
“Nimeona hoja nyingi wanasema Lissu hana pesa, sio tajiri kwa hiyo hawezi kuendesha chama, sasa kama kuna kitu kinatakiwa kuwafanya wanachama wamchague Lissu basi ni kutokuwa kwake na pesa, kwa sababu chama hakipaswi kujengwa na fedha za mtu mmoja” amesema.
Akizungumzia tuhuma alizopewa Lissu kuwa ni mropokaji amesema “Hivi Lissu anaropoka nini?, kazi kubwa ya upinzani ni kupiga kelele,”
Lema amesema Mbowe alimwambia wajipange kwani anataka kuachia chama amechoka na anahitaji wamsaidie, sasa ameshangaa kuona anagombea tena badala ya kumuunga mkono Lissu.
“Mwenyekiti amefanya kazi kubwa sana, hakuna anayebisha, maisha yake yote ameishi ndani ya chama, amekaa kwenye chama akiwa mdogo, yeye ndiye muasisi wa chama hiki, anaweza kuwa hataki kugombea tena lakini ameshashambuliwa sana, kwa hiyo anataka kujisafisha, nimshauri tu zipo njia nyingi za kujisafisha na akamuunga mkono Lissu, ili yeye aendelee kukisaidia chama kwa heshima” amesema Lema.
Lema amesema endapo Mbowe atalazimisha kuendelea kugombea, basi ahakikishe uchaguzi unakuwa wa huru na haki.
“Tukienda kwenye uchaguzi, Mbowe akashindwa basi ‘legacy’ yake itakufa, lakini kama akishinda na uchaguzi ukawa unalalamikiwa bado atajivunjia heshima yake, kwa hiyo ahakikishe uchaguzi unakuwa wa huru na haki” amesema.
Uchaguzi wa Chadema unatarajiwa kufanyika Januari 21, 2025.