Na Mussa Augustine, JamhuriMedia
Chama Cha Madereva wa Malori na Mabasi ya Masafa Marefu na Mafupi Tanzania (TLDTA) kimesema kuwa uwekezaji wa kuboresha Bandari ya Dar es salaam unaotaka kufanywa na serikali ya Tanzania kwa shirikiana na serikali ya Dubai kupitia kampuni ya DP World utakua na tija kubwa katika sekta ya usafirishaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwenyekiti wa chama hicho Hassan Dede amesema kuwa Serikali ya Dkt.Samia Suluhu Hassan ina nia nzuri ya kukaribisha wawekezaji hivyo uwekezaji wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam kupitia DP World utasaidia kujitokeza wafanyabiashara wengi wa magari ya Usafirishaji wa mizigo nakwamba hali hiyo itachangai kuongezeka kwa ajira za madereva.
“Mimi kama mwenyekiti jambo hili ni kubwa kwetu kwani hakutakua na ucheleweshwaji wa mizigo tena,naipongeza serikali kwa sasa mizigo mingi inapatikana katika Bandari yetu ukiacha Bandari ya Msumbiji na Mombasa,Wafanyabiashara wa Zambia na Congo wanaiamini sana Bandari ya Dar es salaam ,hivyo kama mradi huu wa DP World utatekelezwa sekta ya Usafirishaji itaheshimika na Madereva watakua na maisha mazuri” amesema Hassan.
Amesema kuwa mzigo unaotoka Bandari ya Dar es Salaam ni mwingi lakini unaposafirishwa kupelekwa nchini Zambia unakwama katika mpaka wa Zambia na Tanzania kutokana na miundombinu ya Barabara za Zambia kuwa mibovu hivyo ameishauri Serikali ya Tanzania kukutana na Serikali ya Zambia kuona namna ya kuiondoa changamoto hiyo.
Pia amesema kuwa kwa sasa madereva wanasubiri mzigo kwa muda wa siku 1 hadi 2 nahiyo ni kutokana na kuwepo kwa changamoto ya kimtandao wakati wa kuskani mzigo bandarini,lakini uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam utakaofanywa na Kampuni ya DPW itasaidia kuondoa mizigo kwa haraka zaidi.
Kwa upande wake Mwinjilisti wa Kimataifa Alphonce Temba ambaye pia ni Mfanyabiashara maarufu hapa nchini amesema kwamba faini inayotozwa na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) pamoja na Wakala wa Barabara TANROAD pindi mafuta yanapomwagika wakati Malori ya Usafirishaji wa mafuta yanapopata ajari ni uonevu mkubwa hivyo ameishauri serikali kufanyia marekebisho sheria zinazosimamia kodi itokanayo na mafuta yaliyomwagika Barabarani.
“Yaani mafuta yamemwagika,halafu bado TRA na TANROAD wanatoza kodi ,huu sio ungwana hata kidogo,naomba sana wabunge wajaribu kuona hili kwani ni uonevu wa hali ya juu,na wafanyabiashara wa Malawi na Zambia wamekua wakilalamikia kodi hii kwasababu kwao haipo,ipo hapa kwetu Tanzania,sasa tusipoangalia tutawafukuza wafanyabiashara wa kigeni kwenye Bandari yetu” amesema Mwinjilisti wa Kimataifa Temba.
Nakuomgeza kuwa” Mimi kama Mwinjilisti wa Kimataifa, nina mambo 15 ambayo naweza kuishauri serikali ili iweze kupata Mapato yatakayoisaidia serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na sio lazima tutegemee watu kutoka nje ,hivyo nipo tayari kushirikiana na serikali kwa jambo lolote lenye kuleta maendeleo kwa Taifa.