Hotuba iliyotolewa kwenye mkutano wa Uganda People’s Congress, tarehe 7 Juni, 1968

Chama sicho chombo cha Serikali. Serikali ndiyo chombo ambacho Chama hujaribu kutekelezea matakwa ya watu na kuyahudumia masilaha yao.”

… Bwana Rais, Mabibi na Mabwana: Serikali ni jambo lenye sehemu nyingi katika dunia ya leo. Inawezekana ulikuweko wakati ambapo kazi ya serikali ilikuwa ni kahakikisha tu kwamba raia wote wanaishi pamoja kwa amani, na kwamba wanaweza kwa pamoja kuyazuia mashambulio ya majeshi ya nje. Lakini siku hizi hilo ni mwanzo tu wa kazi ya serikali, na matatizo ya serikali. Serikali ya Kiafrika katika mwaka 1968, inayotaka kwenda kwa mujibu wa matakwa ya watu wake, lazima ishiriki kwa vitendo katika uchumi wa nchi; lazima iyaratibu mashirika ya biashara, uchumi, sanaa. Ni wajibu wa serikali ya kisasa kuwasaidia wapate maji safi. Ni wajibu wake kuziratibu na kutoa huduma za elimu na afya- na kadhalika.

Katikati ya shughuli zote hizi, serikali zinaweza zikapotea njia; zinaweza zikasahau ni nini madhumuni ya kazi zao zote! Wakati wa kutafuta utaratibu wa kilimo wa kistadi mno, ni rahisi sana kusahau kwamba madhumuni ya ustadi huo ni kuhudumia watu. Wakati wa kutafuta maendeleo, zinaweza zikasahau kwamba watu wanaweza kuwa na mambo fulani ya maana kwao ambayo hawako tayari kuyaacha kwa sababu ya maendeleo ya vitu. Na hata kama serikali iliyochaguliwa na watu wenyewe, au watumishi wake, haitasahau abadan kwamba madhumuni ya shughuli zake ni kuhudumia watu, bado inaweza kushughulika mno na matatizo ya kutoa huduma njema hata ikawa haina uhusiano na watu. Na ikiwa hivyo, watu wanaweza kutoelewa nini kunafanywa. Na wanaweza kuyavuruga matilaba yao wenyewe kwa kushindwa kuelewa ni ushirikiano gani unaohitajiwa kwao, na kwa nini inawapasa kuutoa.

Hebu nitoe mfano. Watu wetu wanataka maisha bora zaidi kwa nafasi zao na watoto wao. Wanatarajia serikali yao kuyaleta maisha hayo. Lakini, katika nchi inayotegemea kilimo, lazima mazao ya kilimo yaongezwe ndipo maisha bora yapatikane; na ili mazao yaongezeke inahitajika kufanya kazi kwa bidii zaidi na kwa njia za kisasa zaidi. Tuseme kwa mfano, serikali iwatoze watu kodi ili iweze kuwapatia wafanyakazi waliofundishwa ukulima, na kulipia mbolea. Hali ya maisha ya watu itakuwa bora kwa ajili hiyo- kama watazitumia huduma hizo! Lakini kama watu hawataweza kujifunza kwa mabingwa hao, na kama hawataitumia mbolea hiyo, basi hali yao itakuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa hapo mwanzo. Itakuwa mbaya zaidi kwa sababu wanalipa kodi zaidi na hawapati faida ya huduma ambazo zinatolewa na kodi zao. Kusema kweli, serikali itakuwa inajaribu kuwahudumia watu, lakini watu watakuwa wanayadhoofisha maendeleo yao wenyewe. Na baya zaidi, ni kwamba wanaweza wakawa wapinzani zaidi wa serikali yao kwa sababu ya kutoelewa kwao; na hapo wanaweza wakajiachilia kutumiwa kuipinga serikali yao wenyewe na wale wanaotaka kutumia nguvu ya watu kwa faida yao binafsi.

Kazi ya chama cha siasa kilicho imara ni kuwa kama daraja la kuwaunganisha watu na serikali waliyoichagua, na kuiunganisha serikali na watu inayotaka kuwahudumia. Ni wajibu wa Chama kuwasaidia watu kuelewa serikali yao inafanya nini na kwa nini; ni wajibu wake kusaidia watu kushirikiana na serikali yao kwa juhudi ya pamoja ili kuuondosha umaskini ambao umetulemea. Na ni wajibu wa Chama pia kuhakikisha kwamba serikali inaendelea kuyajua sana maoni, shida na matakwa ya watu. Ni wajibu wake kuwasemea watu. Pia ni wajibu wake kuwaelimisha watu na kuwasaidia kuona shughuli za serikali zina maana gani kuhusu usalama wao wenyewe kwa siku zijazo na fursa zao wenyewe za siku zijazo.

Bwana Rais, kazi ya vyama vyetu vya siasa ni ngumu zaidi kuliko ilivyokuwa pale tulipokuwa tunapigania uhuru. Pale tuliita mikutano ya umma; tulipiga kelele kutaka Uhuru; tuliwatukana wakoloni ambao, lazima niongeze, walistahili sana kutukanwa! Lakini sasa tunajenga nchi. Tunapokuwa na mikutano ya umma hatuwezi kuitukana serikali – kwa sababu sisi ni serikali, na watu ndio serikali. Kazi yetu sasa ni kuelimisha, kueleza, na kujenga. Ni wajibu wetu kuwaongoza watu katika kazi ya kutoa mashauri ya kusaidia maendeleo; ni wajibu wetu kuwasikiliza, kushirikiana nao na kufanya kazi nao. Na ni wajibu wetu kuwasemea kwa chombo chetu- serikali.

Maana ukweli ni huu; kwamba Chama sicho chombo cha Serikali. Serikali ndiyo chombo ambacho Chama hujaribu kutekelezea matakwa ya watu na kuyahudumia masilaha yao. Kwa hivyo ni wajibu wa Chama kuamua misingi mikuu ambayo Serikali itaendesha shughuli zake; ni wajibu wake kuamua siasa ambazo Serikali yake itazifuata. Bila shaka, Chama hakiwezi kuwa badala ya Serikali; hakiwezi kuifanya ile kazi iliyotafsiliwa ya kutunga sheria na kuzitekeleza, ambayo ni wajibu wa serikali kuifanya. Lakini Chama chenye mizizi yake katika mioyo ya watu tu, chenye wafanyakazi wenye ari vijijini na kwenye miji nchini mote- Chama cha namna hiyo tu ndicho kinachoweza kuiambia Serikali ni nini matilaba ya watu, na kama matilaba hayo yanatekelezwa kwa njia ya kuridhisha. Kuweko Chama kama hicho ndiko kunakoweza kuhakikisha kwamba Serikali na watu wanashirikiana kutekeleza matilaba ya watu.

Hii ndiyo sababu Mkutano wa Chama ukawa tukio muhimu kuliko yote katika kalenda ya siasa ya nchi. Bunge ni muhimu; Wabunge ni muhimu. Lakini Wabunge wanaweza kuwawakilisha watu ikiwa tu wanaungwa mkono na Chama chenye nguvu kilicho na maelfu kwa maelfu ya wanaume na wanawake watendaji, watambuzi na wenye kujitolea nafsi zao kwa ajili ya umma. Marais, Mawaziri, Wabunge, na kadhalika, majina yao yanaweza yakaandikwa magazetini, wanaweza wakaonekana kwenye kionambali. Lakini wakiwa ni viongozi safi, watakuwa ni safi hasa kwa sababu wanaungwa mkono na Chama chenye nguvu, ambacho kinajua na kuelewa mahitaji ya watu na maoni ya watu. Na ikiwa viongozi kama hao hawavitumii vyeo vyao kama ipasavyo, au hawana fungamano na watu, basi aghalabu itakuwa ni kwa sababu Chama kinashindwa kuwasemea watu, na kuwa jicho la watu.

Bwana Rais, si jambo la kawaida kuja kwenye Mkutano wenu wa Chama na kuzungumzia umuhimu wa Chama. Kila aliyepo hapa leo lazima awe yupo hapa kwa sababu anajua kwamba Chama ni muhimu! Lakini pamoja na hayo, sisi wafanyakazi wa Chama wakati mwingine tunajidharau. Tunajua kwamba serikali ina mamlaka ya kutekeleza sheria, na kwamba Chama hakina mamlaka hayo. Tunajua kwamba Rais na Bunge wanatunga sheria, na kwamba Mkutano wa Chama hauzitungi. Kwa hiyo, baadhi yetu tunaanza kufikiri kwamba wanachama wa vyombo hivyo ni muhimu zaidi, na tunaanza kutoshughulika na kazi yetu ya Chama. Inavyoonekana Tanzania yaelekea kwamba baadhi yetu hatufanyi kosa hilo; badala yake tunajaribu kuwaonyesha wengine umaarufu wetu kwa kujitutumua na kutumia madaraka yetu kuwatishia watu wengine. Lakini pamoja na hayo, ukweli ni kwamba Chama ndicho msingi wa Serikali ya kidemokrasi kama kinafanya kazi yake sawasawa. Na mfanyakazi wa Chama ndiye mtu muhimu kuliko wote katika miji yetu na vijiji vyetu, kama anaifanya kazi yake sawasawa- yaani kama anafanya kazi pamoja na watu, na kama watu wanamkinai na kuwa na imani naye kma mmoja wao, ambaye wanamwendea wakati wa shida, au wanapokuwa na mawazo, au wanapokuwa hawaelewi kitu fulani. Kama mna shaka na ukweli wa maneno haya, tazameni kote Afrika – kusema kweli, tazameni dunia nzima- mwone nini kimetendeka katika zile nchi ambako vyama vya siasa vimeshindwa kuwa, au vimekoma kuwa, vitendaji na viwakilishi vya watu…