Jumanne ya leo Aprili 12, 2022  ni siku ya kumi tangu kuanza kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Tunamuomba Allaah Mtukufu Azikubali Swaumu zetu.

Makala yetu leo inakusudia kuiangazia siku ndani ya Mwezi wa Ramadhani iitwayo ‘Laylatul Qadri’ (Usiku wa Cheo) ambayo ni bora kuliko miezi 1,000 isiyokuwa na usiku huo adhimu.

Nini Laylatul Qadri (Usiku wa Cheo)?

Laylatul Qadri (Usiku wa Cheo) ni usiku mtukufu unaopatikana ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Usiku huu una fadhila nyingi na miongoni mwa hizo ni kuwa ibada ifanywayo katika usiku huu, ikikubaliwa, malipo yake ni sawa na ibada ya miezi elfu moja (Miaka 83 na miezi 3). Katika Qur’aan Tukufu Sura ya 97 (Surat A-Qadri) aya ya 1 hadi ya 5, Mwenyeezi Mtukufu anatubainishia utukufu wa usiku huu kwa kusema: “Hakika Sisi tumeiteremsha Qur’aan katika Laylatul Qadri, Usiku wa Cheo Kitukufu. Na nini kitachokujulisha nini Laylatul Qadri? Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu. Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa kila jambo. Amani usiku huo mpaka mapambazuko ya alfajiri.”

Miongoni mwa yanayoupa ubora usiku huu (Laylatul Qadri) ni haya yafuatayo:

(1)  Mwenyeezi Mungu Mtukufu Ameiteremsha Qur’aan Tukufu katika usiku huu ndani ya Mwezi wa Ramadhani kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah), Aya ya 185 kuwa: “Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi…”  

(2) Usiku huu ni bora kuliko miezi elfu moja na kwamba atakayekubaliwa ibada yake katika usiku huu malipo yake ni makubwa sana.

(3) Kama ilivyodhihirika katika Sura iliyotangulia kuwa katika usiku huu Malaika hushuka na amani hutawala.

Akiuelezea sababu ya kupewa umma wa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) Mwanachuoni Marehemu Sheikh Mohamed Ali Swaabuny amebainisha katika kitabu chake cha Tafsiri ya Qur’aan Tukufu ‘Swaf-watut Tafaasiri’ kuwa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alipata habari ya mtu alivaa silaha akapigana Jihadi kwa miezi elfu moja (miaka 83 na miezi 3). Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akizingatia wastani wa kuishi kwa umma wake alimlilia Mola wake akisema: “Ewe Mola wangu wa haki, umeufanya umma wangu ni umma wenye umri mfupi sana na (hivyo) ni umma wenye matendo machache sana (yasiyolingana na wale walioruzukiwa umri mrefu wakawa na matendo mengi). Mwenyeezi Mungu Mtukufu akamwambia: ‘Nimekupa Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu moja aliyopigana Jihadi yule mtu uliyesikia habari zake.

Laylatu Qadri ni usiku wa kufanya ibada na kujikurubisha kwa Mwenyeezi Mungu na kwa kauli zenye nguvu hupatikana katika kumi la mwisho la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambalo waisilamu wanaotekeleza ibada ya Swaumu wanatakiwa wakeshe nyusiku (wingi wa usiku) zake hasa za witiri ili kupata fadhila za kuupata usiku huo na kupata bahati ya kuhesabiwa amali ya miezi 1000 na ziada.

Ni dhahiri kuwa asiyefanya juhudi za kuutafuta usiku huu na akaukosa atakuwa amepata hasara kubwa kama tunavyojifunza hayo katika Hadithi ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) iliyopokewa na Annasaaiy kuwa: “Imepokewa kutoka kwa Abuu Huraryah (Allaah Amridhiye) kwamba ilipofika Ramadhani, Mjumbe wa Allaah (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: {Umekujieni mwezi wa Ramadhani, ni mwezi wa Baraka.  Imefanywa Swaumu kwenu kuwa ni fardhi, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya Moto hufungwa na mashetani hufungwa. Katika mwezi huu, kuna usiku ulio bora kuliko miezi elfu.  Atakayenyimwa kheri zake, basi hakika amenyimwa!}.

Kwa nini usijitahidi kukesha na kuzidisha ibada katika kumi la mwisho la Ramadhani wakati Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ambaye amepewa dhamana ya kutokuwa na madhambi, pamoja na hayo, alikuwa anafanya juhudi kubwa na akiishirikisha hata familia yake katika hilo kama tunavyoona katika Hadithi zifuatazo:

Imepokewa kwa ‘Aaishah (Allaah Amridhiye) kwamba: “Mjumbe wa Allaah (Allaah Amrehemu na Ampe Amani)  alikuwa akijitahidi katika kumi la mwisho kuliko alivyojitahidi katika siku nyingine zozote.” [Hadithi hii inapatikana katika kitabu cha Hadithi za Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kiitwacho Sahihu Muslim].

Tunasoma katika Hadithi nyingine kuwa: Imepokewa kutoka kwa ‘Aaishah (Allaah Amridhiye):  “Ilipokuwa linaingia kumi (la mwisho) Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alipania shuka yake, akikesha usiku, na akiamsha ahli zake.” Na katika upokezi mwingine:  “Akikesha usiku na akiamsha ahli zake na akijitahidi na kupania shuka yake.” [Hadithi hii inapatikana katika vitabu vya Hadithi viitwavyo Sahih Al-Bukhari na Sahihi Muslim].

Baadhi ya wanazuoni wamesema usiku huu umeitwa Laylatu Qadri Kwanza: Kutokana na uwezo; nao ni utukufu na hadhi yake ukilinganisha na siku nyingine. Pili: Ni usiku ambao una makadirio na majaaliwa ya mwaka mzima na huandikwa yote yatakayotokea mwaka huo, na hii ni hikmah ya Allaah Mtukufu na kuonyesha usanifu katika utengenezaji Wake na uumbaji Wake; na   Tatu: Usiku huo una uwezo mkubwa kama alivyosema Mtume  (Allaah Amrehemu na Ampe Amani): “Atakayesimama usiku wa Laylatul-Qadr kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.” [Hadithi hii inapatikana katika vitabu vya Hadithi viitwayo  Sahih Al-Bukhari na Sahihi Muslim].

Ibada za kufanya katika Laylatul Qadri ni kumuomba sana msamaha Mwenyeezi Mungu, kuswali Swala za Sunnah, kukuthirisha kusoma Qur’aan Tukufu, kuleta Adhkaar (Kumtukuza na kumhimidi Allaah kwa kusema SUBHAANA LAAH, ALHAMDU LILLAAH, LAAILAAHA ILAA LAAH.) na kukaa ITIKAAFU msikitini. 

Nj muhimu kuyafanya haya ili kuepukana na hatari tunayoelezwa katika Hadithi ifuatayo: Imepokelewa kutoka kwa Anas na wengineo kwamba Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alipopanda juu ya minbar aliitikia ((Aaamiiin, Aaamiiin, Aaamiiin)). Alipoulizwa kwa nini ameitikia hivyo akasema: ((Amenijia Jibriyl akasema: “Ee Muhammad, ole wake yule ambaye unapotajwa hakuswalii, hivyo sema Aaamiiin”. Nikasema Aaamiiin. Kisha akasema: “Ole wake yule ambaye umeingia mwezi wa Ramadhwaan kisha ukatoka bila ya kughufuriwa (kusamehewa), kwa hiyo sema Aaamiiin”. Nikasema Aaamiiin. Kisha akasema: “Ole wake yule ambaye amewakuta wazazi wake au mmoja wa wazazi wake lakini wasimuingize Peponi. Hivyo sema Aaamiiin”. Nikasema Aaamiiin)) [Hadithi hii inapatikana katika kitabu cha Hadithi za Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kiitwacho Sahihu At-Tirmidhiy].

Juu ya Dua gani ya kuomba katika Laylatul Qadri, tufaidike na jibu alilopewa Bibi Aaishah alipomuuliza hilo Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kama tunavyoona katika Hadithi ifuatayo:

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Allaah Amridhiye) kwamba amesema: “Ee Mjumbe wa Allaah! Nieleze ikiwa nitajua usiku fulani ndio wa Laylatul-Qadr, niseme nini?” Akasema: ((Sema: “Allaahumma Innaka ‘Afuwwun Tuhibbul-‘Afwa fa’fu ‘anniy.” (Ee Allaah Hakika Wewe ni Mwingi wa kusamehe, Unapenda kusamehe basi Nisamehe)) [Hadithi hii imepokewa na An-Nasaaiy, Sunan Al-Kubraa, Ibn Maajah na Ahmad]

Tuhitimishe makala hii kwa kuzitaja kwa ufupi siku nyingine bora katika Uislamu, nazo ni:

Siku ya Arafa

Siku ya Arafa (Yaumu Arafah) ni siku ya tisa katika mwezi wa Dhil Hijjah (Mfungo Tatu) ambayo ni miongoni mwa siku bora kwa Waislamu, ambapo mahujaji husimama katika Mlima wa Arafa uliopo Makkah nchini Saudi Arabia, wakitekeleza moja ya nguzo muhimu za ibada ya Hijja.

Siku Kumi za Mwezi wa Dhil Hijjah (Mfungo Tatu)

Hizi ni siku kumi za mwanzo katika Mwezi wa Dhil Hijjah ambazo ni siku bora kabisa mbele ya Mwenyeezi Mungu ambazo amali yoyote inayotendwa humo ni yenye kupendwa mno na Mwenyeezi Mungu. 

Siku ya Ijumaa

Siku ya Ijumaa ni siku yenye fadhila nyingi na ni sikukuu kwa Waislamu ambapo Mtume Muhammad (Mwenyeezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani) amewataka watakaokuja katika mkusanyiko wa siku ya Ijumaa waoge.

Miongoni mwa yanayoipa ubora siku ya Ijumaa ni kufunguliwa milango ya mbingu ili kuitikiwa maombi (Dua) za waja wa Mwenyeezi Mungu. 

Mtume Muhammad (Mwenyeezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani) ametuambia kuwa siku ya Ijumaa kuna wakati ambao mja yeyote Muislamu atakayeomba katika wakati huo  atapewa alichoomba.  

Pia Mwenyeezi Mungu ameifanya Swala ya Asubuhi ya siku ya Ijumaa kuwa ni Swala Bora na kukaja amri pia ya kufunga biashara na shughuli nyingine pale adhana ya Ijumaa inaponadiwa ili kwenda kutekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa.

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah. 

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.

Simu: 0713603050/0754603050