Na Deodatus Balile ,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wiki iliyopita Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limefanya marekebisho katika sheria mbalimbali, ikiwamo Sheria ya Shule ya Sheria Sura ya 425.

Yamefanyika mabadiliko kadhaa katika sheria hiyo, ila yaliyoigusa jamii ni ya Kifungu cha 2 cha sheria hiyo. Kifungu hiki awali kilimtaka kila mhitimu wa sheria kutoka vyuo vyote vinavyofundisha sheria kufanya mafunzo kwa vitendo katika shule hii ya sheria.

Sitanii, kabla sijasonga mbele naomba nitangaze masilahi. Kwamba mwaka 2019 mwishoni, nilijiunga na Shule ya Sheria. Nilisoma hadi Machi 19, 2020 kutokana na tangazo la Serikali la Machi 17, 2020 lililotangaza kufunga vyuo na shule kutokana na tishio la UVIKO – 19. Sisi chuo kilifungwa Machi 19, 2020. Baadaye tulielekezwa tusomee mtandaoni. Nilijaribu ila mazingira ya kazi yalibadilika.

Ghafla Kikosi Kazi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiliniletea madai ya kodi Sh milioni 250. Baadhi ya Kodi nilizodaiwa zilikuwa zimekokotolewa hata kabla ya kampuni yangu kusajiliwa. Wakati tumeanza majadiliano, fedha zote zilizokuwa kwenye akaunti zikachukuliwa. Zikabakizwa fedha za kitabu Sh 100,000. Walichukua hadi visenti.

Nilijaribu kuwasilisha kila kielelezo, lakini Kikosi Kazi kilikuwa kazini. Baadaye kikasema nilipe Sh milioni 126. Wakanipangia mpango wa kulipa na hakukuwa na hata mahala pa kukata rufaa. Wee acha tu. Nikaanza kulipa. Miezi mitatu baada ya kuanza kulipa, Kikosi Kazi kikaleta kodi nyingine mpya Sh milioni 240. Nusura roho iachane na mwili. Niliendelea kuwasilisha utetezi huku nikilipa zile Sh milioni 126 ambazo hadi kesho naamini hazikuwa halali, hadi nikazimaliza.

Sitanii, mapenzi ya Mungu yana sura nyingi. Hizo Sh milioni 126, nililipa nikamaliza. Hizi nyingine ambazo tumekuwa na mabishano makubwa, mara ya mwisho nilitoka ofisi za TRA Machi 16, 2021. Baada ya hapo yakatokea mabadiliko ya ‘Mkono wa Mungu’. Sikudaiwa tena, hadi Mei, 2024 Kikosi Kazi kilipoibuka kimyakimya, Kariakoo wakaandamana na kugoma.

Kumbe wakati Kariakoo wafanyabiashara wanagoma, mimi na wafanyabiashara wengine tulikuwa tunadaiwa kodi hadi za mwaka 2006. Yupo mfanyabiashara mmoja alidaiwa kodi miaka 17 iliyopita, wakimtaka aonyeshe nyaraka alizolipia. Wanajua zitakuwa zimechanika. Mkono wa Mungu ukaingilia kati tena, Alphayo Kidata akaondolewa TRA, akaingia Yusufu Mwenda. Tunaendelea na mazungumzo!

Nimeyasema haya, si kuhalalisha kuacha kwangu shule pale Law School, bali kueleza kwa nini niliandika barua ya kusitisha masomo kwa muda usiojulikana.

Kwa vyovyote iwavyo, kama ningechagua kuendelea na shule, Mahakama ya Mafisadi ipo pale Law School. Kila saa 7 mchana walikuwa wanapandisha watu kizimbani, hivyo ningetolewa darasani na kupandishwa kizimbani. Ilibidi niache shule nipambane na jalada la kodi zisizo stahiki.

Sitanii, mimi na kampuni yangu nalipa kodi. Nimekuwa msitari wa mbele kuhamasisha ulipaji kodi nchini na nimepambana na wakwepa kodi wakubwa wakalipa hadi Sh bilioni 20.

Bandari nimeishafisha, makontena 11,000 yaliyokuwa yanapotea hayapotei tena. Kwa kalamu yangu nimewezesha Tanzania kufunga flow meter za mafuta pale bandarini, badala ya mafuta kuingia nchini kwa kupima na kijiti. Yote hayo niliyafanya kwa kuchapishwa habari za uchunguzi katika Gazeti la JAMHURI.

Nilifahamu na nafahamu, kuwa habari hizi kwa kuziandika ni lazima niwe safi. Ndiyo maana kila tarehe 7 ya mwezi nahakikisha SDL/PAYE inalipwa au tarehe 20 ya kila mwezi VAT nahakikisha tumelipa, hata kwa kukopa kama sina fedha. Kodi husika nazilipa kwa wakati.

Nadhani “kwa bahati mbaya”, wahusika walichukua fedha nilizoweka katika kampuni kama mtaji, mfano kulipia gharama za uchapaji na mishahara, wakazitafsiri kama mapato, badala ya kuziweka katika kundi stahiki la mtaji. Kama Vodacom wanavyojenga mnara ukahesabiwa kama mtaji, gazeti kulipia matangazo, mishahara au uchapaji ni gharama za kuendesha biashara na ndio mnara wetu huo. Hii si mada ya leo. Imani yangu ni kubwa kwa CG Mwenda, hili nalo litakwisha. Naushukuru uongozi mpya unalifanyia kazi.

Sitanii, nirejee kwenye mada ya msingi. Pale Law School kwa kipindi cha miezi mitano niliyokaa darasani, nilishuhudia mambo ambayo kwa mawazo yangu nadhani hayako sawa. Kwanza, ukiacha wanafunzi wanaotoka vyuoni moja kwa moja, madarasa haya yanakuwa na watu wazima. Katika umri wa miaka 50 na zaidi, kuna jinsi ya kufundishwa. Nasikia siku hizi wamerekebisha, ila sisi darasa letu lilikuwa na wanafunzi 764.

Hiyo Cohort ya 30 niliyokuwamo, nilipata mshangao. Kuingia darasani, ilikuwa tunagombea kama wasafiri wa Mbagala na daladala. Siku moja ugomvi wa kuingia darasani, ulipasua kioo cha mlango na kikakata wanafunzi. Utashangaa kwa nini tulikuwa tunasukumana kuingia darasani. Viti na meza vilikuwa vichache. Ukumbi tuliokuwa tunautumia, ukichelewa kupata kiti unapanda juu kwa watazamaji. Hakuna meza, unaandika kama kondakta katika basi linalotembea.

Spika zilizowekwa, zilikuwa zinakoroma. Ilikuwapo projector, lakini uoni wa maandishi ulikuwa bidhaa adhimu. Kuna nyakati projector ilikuwa inatoa maneno yamekatika. Joto ndani ya darasa/ukumbi kama kawa. Kimsingi, mazingira ya kujifunzia yalikuwa ya hovyo kuliko hata baadhi ya shule za msingi. Kama kawaida, Watanzania tulikuwa hatusemi. Ukisema nilipasue hili gazetini, wanafunzi wanakwambia utasababisha “tukamatwe sote, acha kaka.”

Ukiacha mazingira ya darasa, kuna baadhi ya walimu walikuwa kichomi. Sijui kama hadi leo wanaendelea hivyo au wamebadilika. Ila nadhani bado wako hivyo, maana unakuta wanaofaulu katika darasa la wanafunzi 700 hawafiki 50. Hili si la kujivunia. Mimi nimekwenda Law School baada ya kuwa nimefanya kazi miaka 26.

Nikiwa nimepata fursa ya kusoma katika vyuo vinavyoheshimika sana duniani kama Hull University cha Uingereza. Ghafla nasokomezwa katika chumba kinachofukuta joto pale Law School!
Sitanii, baadhi ya wakufunzi waliniacha hoi. Wanajifanya kutukoga kwa Kiingereza, kumbe bila kujua wanakipiga kwenye mashimo.

Mmoja akasema: “I heared” kumbe alistahili kusema “I heard”. Yeye anadhani kila ‘Past Tense’ lazima uongeze ‘ed’. Hajui kuna ‘regular and irregular tenses.’ Hii ilinipa shida. Huyu ndiye aliyekuwa anatunyamba tusivyo na akili, tusivyo na uelewa. Na kijana huyu wengi tumefanya kazi na baba yake, lakini anatamba huku akianika ujinga wake mbele ya wanafunzi wake bila kujua!

Kati ya mambo mnayosikia yamewafanya wanafunzi wanaoingia Law School wanashindwa mitihani ni pamoja na utaratibu wa kufundisha kwa baadhi ya wahadhiri.

Mhadhiri anadesa kwenye laptop, anamtaka mwanafunzi akariri kichwani Mkataba wa Haki za Watoto, Katiba na Nyaraka za kisheria zipatazo 159. Hili la nyaraka nitaligusia tena. Mwingine anakutaka ukariri Kanuni za Bunge zote kichwani.

Hapa ndipo nasema kuna tatizo. Nyaraka za kisheria ziko kama maandiko matakatifu. Hupunguzi wala kuongeza neno. Kama ni hati ya kiapo kwa mfano, sehemu inapokaa anwani, majina ya watoa kiapo na kamishna wa kiapo, milele yako vile vile. Fomu ipo tayari. Kwa Law School, ukipewa kuiandaa hati ya kiapo kwenye mtihani ukapatia maeneo 19, ukakosea moja, hilo swali umelikosa lote. Ajabu kweli. Kuna sababu gani ya kuwakaririsha watu fomu wakati fomu hizi zipo tayari na hazibadiliki milele?

Sitanii, ninaye rafiki yangu aliyesoma sheria Chuo Kikuu cha Manchester Uingereza. Nilipompelekea mtaala tunaousoma Law School alipigwa butwaa. Alinitumia mtaala wa chuo chao, ambao baada ya kumaliza somo la historia, sayansi na maarifa ya sheria (Jurisprudence), somo la pili linalofuata mwaka wa kwanza ni uandaaji wa nyaraka za kisheria (legal drafting).

Uandaaji wa nyaraka za kisheria, wanaosoma astashahada (certificate), ni somo wanalofundishwa katika nusu ya kwanza ya mafunzo wanayopewa ya mwaka mmoja nchini Uingereza. Hapa kwetu sijui tunakosea wapi. Kwamba badala ya mtaala ule wa Law School kuuingizwa katika mitaala ya vyuo vikuu wanafunzi wakatoka vyuoni wakifahamu hayo yote wajifunzayo na kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo baada ya masomo yao vyuoni (internship) kama ilivyokuwa zamani tukazalisha wanasheria wengi na wazuri kwa wakati mmoja, hapa kwetu tunaandaa ulaji!

Kifungu cha pili kilichofutwa kama kilivyoandikwa mwanzo, kuna watu hawakuwaza kukuza maarifa, bali waliwaza ulaji. Waliangalia idadi ya wahitimu wa sheria katika vyuo mbalimbali na kuona wote hao wakipitia Law School watapata fedha za kutosha.

Kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, ukiniuliza masomo yanayotolewa Law School yaweje, nashauri yapelekwe katika mitaala ya mwaka wa kwanza kwa kila chuo kinachotoa mafunzo ya sheria. Basi. Maana masomo yenyewe ni miezi sita tu pale Law School, muda uliobaki ni mafunzo kwa vitendo nje ya chuo.

Pia, ikumbukwe si wote wanaosoma Law School wana nia ya kuwa mawakili. Sheria ilivyokaa sasa baada ya mabadiliko haya, imetoa uhuru stahiki. Si dhambi mtu kusoma sheria akawa na uelewa wa kisheria na akatoa ushauri wa kisheria ambao utasaidia watu kufanya uamuzi au kutenda kwa mujibu wa sheria. Ikitokea mabishano ya kisheria yanayohitaji utatuzi mbele ya mahakama, basi mawakili ndio washiriki utatuzi huo mahakamani.

Sitanii, bahati mbaya nyingine, wengi wa walimu wanaofundisha pale Law School zaidi ya asilimia 90 hawakupata kusoma pale Law School. Hawa walitumia utaratibu wa zamani unaotumiwa na nchi kama Uingereza, Marekani na nyingine wanaosailiwa na Jaji Mkuu (bar) kuthibitisha kuwa wameiva na wanaifahamu sheria, wanaweza kufanyakazi ya uwakili kutetea wenye uhitaji. Hawa ambao hawakusoma Law School, baadhi yao ndio wanaowahenyesha wanafunzi wanaoingia Law School.

Tabia binafsi nazo zinapaswa kudhibitiwa. Wapo walimu wenye tabia binafsi mbaya, ambao ukiwaangalia unasema tu kuwa hawa vijana na mabinti hawakufundwa katika familia zao. Lakini wapo walimu waungwana usipime. Leo uliza mtu yeyote aliyepita pale Law School, hauwezi kukuta anawasema vibaya Dk. Godfrey Taisamo, Jaji Robert Makaramba, Prof. Hamudi Ismail Majamba, Harold Sungusia na wengine wachache. Lakini wale kizazi cha Gen – Z, ni shida kweli.

Sitanii, mabadiliko haya ya sheria, Law School wayachukulie kama kengele. Leo, jimbo lao limepunguzwa ukubwa kutokana na kushupaza kwao shingo. Wembe uliotumika kuwanyoa umehifadhiwa. Wasipochukua tahadhari, ushauri nilioutoa wa mtaala wa Law School kuingizwa kwenye mitaala ya vyuo naona ukichukuliwa, hapo ndipo watalia na kusaga meno.

Najua msomaji unajiuliza kwa andiko hili na hofu ya wanafunzi wengi wa kitanzania kuwa nitarudi tena Law School kwa andiko hili? Jibu ni ndiyo. Kuna masuala namalizia, si muda mrefu nitatia tena timu Law School. Binafsi naamini katika uhuru wa kutoa mawazo. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827

Please follow and like us:
Pin Share