Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesitisha ratiba ya mabasi 38 ya kampuni ya New Force yanayofanya safari zake kuanzia alfajiri.

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo amesema sababu kubwa ya kusitisha ratiba hiyo ni kutokana na wimbi la ajali ya za barabarani zinazohusu mabasi hayo.

“Uchunguzi wetu wa awali umeonesha kuwa madereva wengi wanaofanya safari za asubuhi hawazingatii alama za barabarani, hivyo tumejadiliana nao na tumefikia maamuzi ya kusitisha safari zao za alfajiri.” amesema Suluo.

Amesema kati ya mabasi hayo 38 mabasi 10 ni yale yanayoanza safari zake saa tisa alfajiri na mabasi 28 yanayoanza safari saa 11 Alfajiri hivyo watalazimika kuanza safari zao kuanzia saa 12 asubuhi.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu huyo wa LATRA amewataka madereva wa kampuni nyingine kuzingatia sheria za barabarani kwa usalama wa abiria.