Na Benny Kingson, JamhuriMedia, Tabora.
MAMLAKA ya udhibiti usafiri ardhini LATRA Mkoa wa Tabora imeyakamata magari 20 yanayofanya safari kutoka Tabora mjini kwenda wilayani Sikonge kwa kutoza abiria nauli kubwa kupita kiwango kinachotakiwa kisheria kwa madai ya gharama za uendeshaji kuongezeka.
Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Tabora Nelson Mmari akitoa taarifa kwa gazeti hili alisema kuwa magari hayo wameyakamata kufuatia ukaguzi walioufanya na kubaini yanatoza nauli kati y ash.4,000 hadi sh.5,000 badala y ash.3,700 inayotambulika kisheria.
Mmari alisema kuwa katika ukaguzi huo wamegundua wahusika wa magari hayo wamekuwa hawarudishi chenji kwa abiria wanapotoa pesa ili kulipa nauli na kwamba wamekuwa hawawapi tiketi zinazoonyesha malipo halisi.
“Serikali ilitangaza nauli halali Disemaba mwaka 2023 na kuanza kutumika nchi nzima na Mkoani Tabora tulimwambia Mkuu wa Mkoa ambaye aliwaita wadau wote wa usafirishaji na kuwaeleza na kuwahimiza kufuata sharia zote za umiliki wa vyombo vyao”alisema.
Alisema kuwa kuna magari kati ya 50 hadi 70 yanayotoa huduma ya usafirishaji toka Tabora mjini kwenda wilqayani Sikonge na kwamba kuna umbali wa Km 77 ambapo kama wamiliki wa magari watafuata sharia zilizopo na kuwafuatilia watu waliowaweka kusimamia magari yao watapata faida kubwa Zaidi.
Afisa Mfawidhi huyo alisema kuwa magari yote yanayofanya shughuli za usafirishaji yanatakiwa kuwa na mkanda wenye rangi yake kulingana na uelekeo waliopangiwa,kwa magari yanaenda wilayani Sikonge yanatakiwa kuwa na mkanda wa rangi ya kijani na ubavuni kuandikwe nauli inayotakiwa pamoja na eneo linapotoka na kuelekea.
“Magari yote yanatakiwa kuwa na tiketi,yale makubwa watoe tiketi za kieletroniki na haya ya wilayani yanatakiwa kutoa tiketi zinazoonyesha namba za gari,jina la kampuni,jina la abiria,siti yake na kiwango cha nauli nah ii inasaidia kuonyesha nauli halali inayotozwa,kulitambulisha gari na kumtambulisha abiria alipotoka na anapokwenda”alisema.
Alisisitiza kuwa wamiliki na madereva wa magari wasisingizie kupanda au kushuka kwa gharama za mafuta ili kupandisha nauli na kwamba gharama za uendeshaji siyo mafuta peke yake ni pamoja na vipuli na malipo ya wafanyakazi na mambo mengine ambayo ni ya kawaida”alisema.
Mmari aliwataka kufuata sharia za usafirishaji kwa kuvaa sare za Kaunda suti za rangi ya bluu ama tisheti zenye nembo ya kampuni,kutoza nauli halali na kutoa tiketi za kieletroniki na wanatoa tiketi za kawaida wahakikishe zinakuwa vigezo vyote ambapo watambue serikali ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza mabadiliko ya nauli.
Aidha aliwataka wamilikiwa magari kutotumia wapigadebe ama vishoka kuwakatia tiketia abiria kwa kuwa wanawaumiza na ni kinyume cha sharia na kwamba wanawaongezea gharama za uendeshaji kwa kupigwa faini pindi watakapobainika na kukamatwa ambapo watu hao wanajinufaisha kupitia mali zao.
Alisema kuwa mabasi yapo ya kutosha na hakuna tatizo la upungufu na kwamba abiria wahakikishe wanalipa nauli zao pindi wanapoona basi husika lipo kituoni na wapande na kuingia ndani ili wahudumiwe kwa kulipa nauli zao halali nakupatiwa tiketi halisi.