Wiki iliyopita mchezaji wa zamani wa timu ya Chelsea na West Ham United, Frank Lampard, alitangazwa rasmi kuwa Kocha Mkuu wa Chelsea (The Blues).

Timu hiyo inayopatikana katika Jiji la London, Uingereza, imeingia mkataba wa miaka mitatu na Lampard ambaye kabla ya mkataba wake huo wa kuinoa Chelsea alikuwa kocha wa Derby Country, klabu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza England.

Lampard ametangazwa kurithi mikoba ya mtangulizi wake, Maurizio Sarri, aliyeifundisha timu hiyo kwa msimu mmoja na kisha kutimkia katika Klabu ya Juventus ya Italia.

Meneja huyo ataanza kazi katika mazingira magumu mara baada ya timu hiyo kufungiwa kusajili wachezaji msimu mmoja, adhabu ambayo msingi wake ni kitendo cha klabu hiyo kusajili wachezaji wenye umri chini ya miaka 18. Usajili ambao unatajwa kukiuka taratibu zilizowekwa.

Licha ya mashabiki wa timu hiyo kumpokea kwa shangwe kocha huyo, wanapaswa kufahamu kwamba ataanza kazi katika mazingira magumu kuliko makocha waliomtangulia katika klabu hiyo, kwani aliyekuwa mshambuliaji machachari wa Chelsea, Eden Hazard, amekwishahama, akienda kujiunga na miamba ya Hispania, Real Madrid.

Hata kama bado wapo washambuliaji aina ya Pedro Eliezer Rodríguez Ledesma na Willian Borges da Silva, bado inaonyesha pengo la  Hazard halijapata ufumbuzi.

Hali hiyo imeifanya timu hiyo kuwarudisha baadhi ya wachezaji wao waliowapeleka kwa mkopo katika klabu mbalimbali. Wachezaji hao ni pamoja na Kourt Zouma, Michy Batshuay, Tammy Abraham, Christian Purisic na Tiemoue Bakayoko.

Mara baada ya Lampard kumwaga wino katika timu hiyo, ratiba ya Ligi Kuu ya England (EPL) ilitolewa huku ikibainika kwamba kiungo huyo wa zamani wa klabu hiyo aliyeitumikia timu hiyo kwa mafanikio makubwa ataanza kibarua chake katika uwanja wa ugenini dhidi ya timu ya Manchester United, katika dimba la Old Trafford, Agosti 11, mwaka huu.

Baada ya mechi hiyo Lampard atarejea katika Uwanja wa nyumbani wa Stamford Bridge kwa ajili ya kukabiliana na mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza, Leicester City katika wiki ya pili ya Ligi Kuu ya England.

Lampard atakuwa na kibarua kizito hasa kwa kurejea kumbukumbu za walioshika nafasi kama hii yake kwa sasa, kwa mfano, Roberto Di Matteo, aliwahi kuichezea klabu hiyo na baadaye kuwa kocha wa timu ya Chelsea na mara baada ya kurithi mikoba ya kuinoa timu hiyo mwaka 2012 alitwaa taji la ubingwa barani Ulaya na Kombe la FA, ingawa msimu uliofuata hakufanya vizuri katika klabu hiyo na kutimuliwa, nafasi yake ikatwaliwa na Rafael Benitez.

Ikumbukwe Lampard atarejea kama kocha katika klabu hiyo na atawafundisha baadhi ya wachezaji aliocheza nao kwa muda mrefu katika timu hiyo, wachezaji hao ni pamoja na David Luiz, Kurt Zouma, Gary Cahill na Willian.