Wilaya ya Busega mkoani Simiyu imefanikiwa kumpata muwekezaji kutoka Malaysia atakayewekeza Sh trilioni 6 kwenye Hifadhi ya Kijereshi ili kukuza utalii katika eneo hilo.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Busega, Raphael Chegeni, wakati wa kuhitimishwa kwa tamasha la kukuza utalii wa ndani lililofanyika katika kata hiyo, lililopewa jina la ‘Lamadi Utalii Festival.’
Akifungua tamasha hilo awali, Naibu Waziri wa Utalii, Constantine Kanyasu, anasema litakuwa linafanyika mara moja kila mwaka kama moja ya mikakati ya kukuza utalii wa ndani katika Mbuga ya Serengeti, Hifadhi ya Akiba ya Kijereshi na Ziwa Victoria.
Anasema serikali inashughulikia suala la utaratibu wa malipo ya watalii wanapoingia katika vivutio hivyo, jambo ambalo hivi sasa ni kikwazo kwa wageni wengi.
“Single entry ni kikwazo, kwa hiyo tunalishughulikia wageni watapita getini kuja Lamadi na watarudi hifadhini bila kutozwa gharama yoyote,’’ anasema Kanyasu.
Naye Chegeni anasema kutokana na uwepo wa Hifadhi ya Kijereshi katika jimbo lake, serikali imeamua kujenga barabara yenye urefu wa kilometa 80 hadi Lamadi ambako ni kilometa tatu hadi katika hifadhi hiyo.
“Hivi sasa tunasema utalii wa ndani unawezekana. Lamadi ni mji wenye fursa nyingi, imezungukwa na vivutio vingi ambavyo vinaweza kuifanya iwe ya tofauti na yenye mvuto na kupendwa na watalii,” anasema Chegeni.
“Kupitia tamasha hili na hifadhi zilizoizunguka Lamadi, mpaka sasa tumepata mwekezaji kutoka Malaysia, ambaye atawekeza mradi wa Sh trilioni 6. Pia wawekezaji wengine wanaohitaji kuwekeza tunawakaribisha,” anasema Chegeni.
Aidha, anawataka vijana wanaojishughulisha na kazi ya kutembeza watalii (Tour Guides) kuitumia Mbuga ya Serengeti kuboresha maisha yao, kwani baadhi ya vikwazo vya kazi zao vimeanza kushughulikiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera, anasema Lamadi imezungukwa na vituo vya utalii wa ndani vingi ambavyo vina uwezo wa kuipa fursa kubwa ya kuitangaza Tanzania.
“Tamasha hili la Lamadi Festival ni tamasha ambalo tumeliandaa kwa ajili ya kutangaza fursa kwa vijana kupitia utalii wa ndani, pia watu wasizoee tu kuwa kuna tamaduni za Kimasai.
“Tunataka watu wajue kuna tamaduni za Kisukuma na Kikurya, hata wageni watakapofika Lamadi waweze kujivunia kula samaki ambao wanapatikana kwenye Ziwa Victoria,” anasema Mwera.
Anaongeza kuwa tamasha hilo litaambatana na tamasha jingine litakalofanyika kila baada ya miezi mitatu la kuuza vitu vya asili (culture traditional) la ‘Lamadi Trade Fair.’
Naye Diana Chambi kutoka TANAPA anasema endapo wakazi wa Lamadi wataitumia fursa hiyo wana uwezo wa kuutangaza utalii vizuri.
Revocatus Titus, mkazi wa Lamadi anayefanya kazi ya kuongoza watalii, anasema vijana wasibague kazi na wale wenye ujuzi kuhusu mambo ya utalii wachangamkie fursa hiyo ili kujiingizia kipato.
“Tamasha hili linahamasisha vijana wa eneo hili wapate moyo wa kusomea mambo ya utalii na itasaidia wale wenye nyumba za kulala wageni kujenga nyumba za kisasa zaidi na kutoa nafasi ya kazi kwa vijana ambao wamesomea mambo ya kutunza nyumba hizi,” anasema Titus.