Katika Gazeti la JAMHURI la Jumanne Juni 12, 2012, kuna makala iliyoandikwa na Mobhare Matinyi akishutumu Waislamu kuhusiana  na madai yao mbalimbali, wanayoyalalamikia kila siku hapa Tanzania.

Ukiiangalia makala haya utaona yeye alikerwa na kitabu cha Padre Dk. John Sivalon wa Kanisa Katoliki na siasa za Tanzania Bara mwaka 1953 hadi 1985.

 

 

Sasa kwa kuwa mwandishi ana chuki na Waislamu, akaweka mistari miwili mitatu tu ya huyo Padri Sivalon, kisha dhamira yake na chuki zake akazipeleka kwa Waislamu ambao ni adui zake kana kwamba Waislamu walishirikiana na Sivalon kuandika aliyoandika.

Wapenzi wasomaji ukiangalia anuani aliyoweka mwandishi kuna taswira za CV yake, lakini unakutana na maneno ambayo ameandika katika makala yake hayana mfano na ile inayoonekana, kwamba ni taswira ya CV yake. Hali hii inazidi kutia wasiwasi katika elimu ya Tanzania, elimu ambayo kila mwaka hutangaziwa wananchi ‘Seminari zapeta’.

Ninacho mezani kitabu cha Padri Sivalon nakisoma vizuri, nakirudia tena na inathibitika kwamba anachokisema padri huyu ni kitu tofauti mno na anachokiandika Matinyi, ndiyo maana nikauliza ni Padri Dk. John Sivalon au Waislamu? Matinyi ambaye ufahamu wake wa mambo unatia mashaka, haelewi wanachokinukuu Waislamu kutoka kwa Padri Sivalon na pia haelewi Sivalon alisema nini katika kitabu hicho.

Mimi nitamfahamisha kwa ufupi kadri inavyowezekana. Lengo la utafiti wa Padri Sivalon katika kipindi kile ni kuwa alishangazwa na kanisa kupiga usingizi wakati wananchi wanateseka na hali ngumu mno – kuwahi kutokea ya uchumi – ambayo ilivuka hali ya udhalili kiasi kwamba bidhaa zilikuwa ni kitu cha anasa kiasi cha kufanya maduka kubaki mbao tupu; sukari kiroba kimoja cha kilo 25 mnapanga foleni kuanzia asubuhi hadi jioni katika kata au kijiji ili mkigawane hicho kiroba.

Sivalon akaona achunguze kulikoni waumini wanateseka huku kanisa likipiga usingizi wakati lilipaswa kuwasemea na kuwatetea? Katika utafiti wake akagundua kwamba kanisa na serikali ni pacha. Sasa nani atamlaumu nani? Kama vile haitoshi, akagundua kwamba kanisa ambalo ni pacha na serikali huwaona wakomunisti na Waislamu ni maadui zao.

Nadhani hapa ndipo Matinyi anapochanganyikiwa badala ya kupambana na Sivalon, anahamisha mada kwa Waislamu. Waislamu humnukuu tu huyu padri basi.

Mhariri, mimi ni Msumbwa wa Unyamwezini Tabora. Leo nashangaa naambiwa Msumbwa ana utamaduni wa Ghuba ya Uarabuni? Yaani Usumbwa na Uarabu wa Ghuba ni utamaduni mmoja? Hili linawezekanaje? Uongo mtupu!

Ni upuuzi na ubabaishaji wa hali ya juu usio na faida yoyote. Hakuna mwingiliano wa kikabila au vinginevyo kati ya Msumbwa au wengine aliowataja kuanzia Dar es Salaam hadi Ujiji, ni takataka na upuuzi mtupu tu aliouandika.

Inavyoonyesha kwanza hajui malalamiko ya Waislamu. Yeye na wenzake wasiojua hupewa kurasa katika magazeti kupotosha madai. Katika mchezo huo wa kupotosha wanadhani itawapa nafuu kumbe ndiyo wanachochea kuni moto unarindima. Katika maneno yake kuhusu shule imeonyesha wazi kapotosha kweli kweli.

Mimi nawaomba wasomaji tuzungumze mantiki. Twende stesheni ya reli tusafiri twende kwangu Usumbwani Tabora. Lakini treni hakuna. Treni ilikuwapo asubuhi na jioni kila siku na treni ndogo iitwayo Punguza zikifuata nyuma kuchukua wale waliobaki ili nao wasafiri.

Sasa imekuwaje? Nadhani tuwaulize waliohodhi mashirika hayo wanaoitwa ‘seminari zapeta’ watupatie majibu ilikuaje wakapeta halafu mashirika yakatokomea.

Bado mimi nataka twende Tabora. Basi twende Ubungo tukapande mabasi, tushukuru tumefika Tabora salama kwa mabasi ya Waarabu Mabbruk, Sabena na NBS. Lo! Wapi Kamata, UDA!

Hapa Tabora miaka ile ya 1960 nikiwapo mimi mmoja wao tulikuwa na shule zifuatazo Chemchem, Mbugani, Kazeh Hill, Kitete, Cheyo, Town School, Kiloleni, Mtendeni na Isevya. Hizi ni za serikali na ni za msingi.

Halafu White Fathers, St. Francis Xavier, St. Mary na St. Mary Secondary (Milambo), hizi ni kwa Wakristo. Halafu HR Primary School na Uyui Secondary za Wahindi.

Sasa upotoshaji wa wapotoshaji unaanza suala likiwa la Waislamu, akina Matinyi na wenzake zile shule zinazoitwa H.H Aga Khan pale Tabora na Tanzania yote huziita za Wahindi, yaani zile za Wajerumani, Waingereza na Wazungu wao huziita za Wakristo. Neno Wazungu hawalitaki ila kwa Waislamu analeta neno la upotoshaji ‘Wahindi’,  ‘Bohora’, ‘Ismailia’ ili apoteze watu. Namwambia kachelewa.

Msomaji neno H.H. Aga Khan ni nembo tu kwa sababu huyo Aga Khan alikuwa patroni, lakini mmiliki ni East African Muslim Welfare Society (EAMWS). Katibu kwa hapa Tanganyika alikuwa  Tewa Said Tewa  na baadaye Abdallah Fundikira na kina Bibi Titi Mohamed. Na hapa Tabora alikuwa mzee wangu Bilali Rehani Waikela, yaani kwa akili ya wapotoshaji hawa kina Waikela kwao wao ni Wahindi.

Hapa Tabora shule za Waislamu zilikuwa H.H Aga Khan Primary School (baadaye Uhuru) na H.H Agha Khan Secondary (sasa Kazima Secondary).

Taifisha ya miaka ile inawashushua wanaodai eti ililetwa ili Waislamu wasome. Kwanza kama unataka Waislamu wasome utataifishaje na kile cha kwao? Pale Dodoma wakati wa hafla ya sherehe za Idd el Fitr, Bakwata walipomtaka Rais Kikwete arudishe shule za Waislamu zilizotaifishwa, mlifikiri Bakwata wanasema wasichokijua?

Bakwata ilidai shule zilizoitwa H.H Aga Khan ambazo mmiliki wake ni East African Muslim Welfare Society, ambayo kutokana na maendeleo yake utawala ukaivunja na kuipiga marufuku hapa Tanganyika. Baadhi ya viongozi wake kama mzee Waikela wakawekwa kizuizini walipopinga kufutwa kwa taasisi yao ya Kiislamu ya EAMWS, Mzee Waikela yu hai hadi sasa.

Mimi bado nazungumzia shule hapa Tabora. Utaona katika orodha niliyotaja ya shule za Tabora EAMWS ilikuwa na shule zake ambazo hao waite Waislamu usiwabadili jina. Ukichunguza Tabora miaka yetu ile zile shule za Serikali au Waislamu, Kihindi au Kikristo kwa mazingira ya Tabora shule zote za msingi wanafunzi ni Waislamu, na hapa ujue sizungumzii sekondari za serikali ambazo zilikuwa ni Tabora Boys na Girls, wanafunzi wake wakikusanywa kutoka sehemu mbali mbali nchini.

Nazungumzia shule za msingi Cheyo, Kitete, Kazeh Hill, Chemchem, Mbugani, Town School, White Fathers, St. Francis Xavier, St. Marys, HR Primary School, H.H Agakhan, Mtendeni na Isevya. Shule hizi kwa mazingira ya Tabora, theluthi mbili ya wanafunzi walio madarasani kwa shule karibu zote ni Waislamu. Je, hao hawapendi shule? Madai ya Waislamu ni kwa vipi madarasa ya shule za msingi yafurike Waislamu, lakini wapotee inapokuja form one?

Je, ni mazuzu? La hasha. Hebu mimi nijibu hili. Kuna kamchezo hapa kwa sababu hao wanaoitwa ‘wamepeta’ tulikuwa nao madarasani tena wengi wao dhaifu kweli kweli. Mimi sikuona hiyo alama ya ushujaa wa ‘upetaji’. Hapa ndipo katika madai kwamba inakuwaje shule za msingi zimefurika Waislamu lakini inapokuja suala la sekondari wanatoweka? Je, nini kinatokea hapa katikati?

Bahati nzuri, juzi katika somo moja la Islamic Knowledge baada ya wakuu wa shule za Kiislamu kutaka waone fomu za mitihani ambazo matokeo yalikuwa ni takribani karibu yote ni F, ghafla A, B, C, D zikarejeshwa kimya kimya. Je, hii ni nini? Si ndiyo kamchezo kanakotiliwa shaka miaka yote na Waislamu? Sasa mambo haya na Ghuba ya Uarabuni wapi na wapi?

Yaani ati Msumbwa na mtu wa Ghuba ya Mashariki ya Kati kabila yao moja, utamaduni wao mmoja inaingia akilini kweli? Ingekuwa vizuri hao ‘wapetaji’ wangetuonyesha vifo vya mashirika na taasisi zote za wizara, na kile kinachoitwa ‘njoo kesho njoo kesho’ kikitamalaki kila sekta.

Hivi kweli wapetaji wa kweli ‘njoo kesho njoo kesho’ ya nini? Ni vurugu na ghasia tu katika ofisi kiasi cha watu kudai mafao ya kuvunjika kwa East African Community tangu mwaka 1977 bila wapetaji kulipatia ufumbuzi dai la wazee. Umepeta nini? Ni lazima madai ya kwa nini katika shule za msingi kufurika Waislamu lakini kuanzia Form One uwaambie wameanguka mtihani, kwa nini wao tu? Yataendelea hadi ukweli utadhihiri.

Ndugu Matinyi anakerwa na anataka kipengele cha kabila na dini kiwekwe kwenye sensa ya Taifa, lakini hakerwi na anayetoa takwimu za dini za watu, huyu mbona anashangaza sana?

Anakukera yule anayesema kwamba kama idadi unayoitaja ya dini za watu ni hii, umeitoa wapi wakati kipengele hicho hakipo? Hii inamkera Matinyi. Haoni uhalali wa kuthibitisha takwimu hizo nyumba kwa nyumba, anataka kuficha nini Matinyi?

Kwa kuhitimisha kwa leo madai ya Waislamu yataendelea kusikika kila mara hadi hapo ufumbuzi wa matatizo yao utakapopatikana. Hakuna uwezekano wa ujanja wa wimbo wa serikali kuwa haina dini ukafaulu kunyamazisha madai haya ya Waislamu.

Haiwezekani ati ka wimbo katamu, serikali haina dini ikifika Jumapili serikali inafunga ofisi za umma, wakati wa Krismas inaremba ofisi za umma kwa marembo ya dini, huku hiyo serikali ukiingia mkataba na dini kuendesha shule na hospitali za dini maarufu MoU.

Hakutakuwa na mwafaka katika mizozo hii kwa njia za ujanjaujanja. Watu wanataka kuona sasa haki inatendeka, inaposemwa serikali haina dini ionekane na wote. Upotoshaji wa Ghuba na Uhindi wanaotumia hauna nafasi, hawawezi kufaulu kwa kuwa uelewa wa watu unapanuka kila siku.

* Mwandishi wa makala haya Kassali Mussa Alli amejitambulisha kuwa ni msomaji wa JAMHURI.