Na Joe Beda Rupia
Amos Gabriel Makalla. Jina hili si geni kwa wengi. Huyu si mgeni katika nyanja za uongozi. Wala si mgeni hata kidogo katika siasa.
Kwa miaka mingi tu sasa amekuwa akisikika, kwanza katika viunga vya Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba kama ‘mtunza mkoba’ wa chama.
Akaja kuwa Mbunge wa Mvomero mkoani Morogoro. Kisha Naibu Waziri huku na kule. Baadaye Mkuu wa Mkoa katika mikoa kadhaa, hatimaye Katavi.
Akapumzika kwa miaka michache. Sasa Makalla ndiye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa maana hiyo si rahisi wala si sahihi kuubeza uzoefu alionao katika uongozi wa kitaifa!
Leo RC Makalla anataka mabasi yanayotumia kituo cha Mbezi Luis (Magufuli Bus Terminal – MBT) kuwaacha abiria wote kituoni hapo.
Yaani, mabasi yanayoingia Dar es Salaam yawashushe abiria wote MBT na ni marufuku kwenda kuwashusha kwenye terminal binafsi, nyingi zikiwa Shekilango.
Sidhani kama yupo sahihi sana. Au labda mimi ndiyo sijamuelewa! Ni kwa nini ameamua hivyo? Moja ya sababu anazotoa ni kuwasaidia kupata kipato wafanyabiashara wadogo waliopo MBT.
Wamachinga. Mama na baba lishe. Waendesha bodaboda na bajaji. Madereva teksi. Yaani siku hizi hata madereva teksi nao ni ‘wamachinga’!
Moja ya majukumu muhimu ya kiongozi wa kisiasa ni kutetea wanyonge. Kuhakikisha kuwa wanyonge, watu wasio na wa kuwatetea, hawakandamizwi kwa namna yoyote ile katika nchi yao.
Shida yangu mimi ni neno ‘wanyonge’. Hawa, wanyonge, ni akina nani?
Makalla anaamini kuwa wanyonge ni wafanyabiashara wadogo waliopo MBT ambao mabasi yasiposhusha abiria, wao watakosa mkate wao wa kila siku.
Yaani madereva teksi nao ni wanyonge wa nchi hii? Makalla, hivi una habari kuwa kuna abiria ni wanyonge kuliko hawa bodaboda, mamalishe na mateksi dereva?
Hivi unafahamu kwamba kuna abiria wanasafiri na pesa ya nauli tu, hata ya kula njiani hawana?
Hvi RC Makalla, unafahamu kuna wazazi hushindwa kuwarejesha watoto wao likizo kwa kuwa hawana fedha ya kutosha nauli, kula njiani, na kuwatoa stendi hadi nyumbani wanakoishi?
Mkuu wa Mkoa huenda wewe umeishi maisha mazuri kuliko sisi wengine. Hivi unafahamu kwamba nauli ya teksi kutoka Mbezi Louis hadi Kigogo au Keko ni sawa na nauli ya Dar es Salaam hadi Arusha?
Sasa hapo hatujazungumzia nauli ya teksi kutoka Mbezi Louis hadi Mbagala.
Labda unadhani bodaboda ni nafuu kuliko teksi, lakini ni bodaboda wangapi waaminifu? Utawajuaje?
Wangapi wenye uzoefu wa kusafirisha abiria kwa usalama katika barabara za Dar es Salaam? Abiria mwenye watoto na wazee atatumia bodaboda?
Sawa. Abiria wote washukie Mbezi Louis, wasio na uwezo wa nauli za teksi au bodaboda, walale kituoni ili mamalishe wauze chai na chakula.
Ni abiria wangapi wa mabasi yanayowasili Dar es Salaam usiku kutoka mikoa ya mbali wanaokuwa na hamu ya kula kwa mamalishe?
Swali jingine linaloniumiza kichwa ni, hivi kati ya abiria na mmiliki wa basi, ni nani anayefaidika au anayepata unafuu kwa mabasi kushushia terminal binafsi?
Lakini kwa kifupi, mantiki ya kwamba abiria wote washushwe Mbezi Louis ili mamalishe na madereva teksi wapate riziki, sioni kama ina maana sana!
Hakuna kipato chochote cha ziada kwa serikali au halmashauri kinachopatikana kwa abiria kushushwa MBT zaidi ya kuongeza msongamano tu.
Na kuna sababu gani ya kuongeza msongamano wa watu MBT? Uzoefu unaonyesha kwamba, mara nyingi stendi yenye msongamano mkubwa huwapa mwanya wahalifu kufanya wanayoyataka.
Mfano wa haraka ni matapeli. Hivi RC Makalla, unafahamu ni wasafiri wangapi tayari wamekwisha kuibiwa kitapeli Mbezi Louis?
Kwa sasa tunapambana na janga la corona, sasa kwa nini wasafiri warundikane eneo moja wakati kuna uwezekano wa kuwatawanya maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Amri kwamba mabasi yote yaingie MBT wakati wa kuondoka na kurudi Dar es Salaam hii inaeleweka na ni lazima itekelezwe.
Kwamba kituo hicho kimegharimu fedha nyingi, hakuna ubishi. Lakini hii hailazimishi abiria kushukia hapo kwa kuwa, kama ni kurudisha gharama, wenye mabasi ndio wanaolipa tozo kuingia stendi.
Kwa maana hiyo, kushuka abiria eneo hilo hakuathiri kabisa mapato ya stendi, hata uendeshaji wake zaidi ya kuongeza msongamano.
Kitu muhimu ambacho Serikali ya Mkoa au Manispaa ya Ubungo inapaswa kufanya ni kuzuia wizi, utapeli, usumbufu na kila adha wanayofanyiwa abiria Mbezi Louis.
Kwa kweli mbali na adha ya kusongwasongwa na wapiga debe kuanzia umbali wa mita 300 kutoka stendi, kuna maelfu ya tiketi feki zinazouzwa kila sehemu.
Badala ya RC Makalla kupambana na wamiliki wa mabasi na kuwalazimisha kuua terminal zao, ni vema akaelekeza nguvu kufunga vibanda zaidi ya 200 vya mawakala.
Eneo la Mbezi kuanzia stendi ya daladala kuelekea Malamba Mawili na Goba kumezagaa vibanda vya mawakala wa mabasi wanaouza tiketi.
Nimewahi kukutana na abiria wengi wakiwa na tiketi za mabasi ambayo ama yamekwisha kuondoka saa 12 aubuhi, au hayapo kabisa barabarani.
Ukiwauliza wamepata wapi tiketi hizo, wanakwambia wameuziwa na wakala aliyepo barabara ya Malamba Mawili.
Mtu ana tiketi ya Sumry Bus Service wakati kampuni hiyo kwa sasa imebadili biashara na kugeukia kilimo huko Sumbawanga!
RC Makalla, malalamiko kama haya huwezi kuyapata kwenye terminal binafsi. Huko hakuna utapeli kwa kuwa ni ofisi rasmi kabisa.
Sasa basi, piga marufuku mawakala wa vichochoroni ili kuwasaidia abiria kuepuka utapeli.
Abiria waelimishwe kwenda kununua tiketi ama ndani ya Magufuli Bus Terminal au kwenye ofisi za mabasi zilizopo kwenye vituo binafsi Shekilango.
Mzee Makalla, punguza msongamano MBT kwa kuwapa haki abiria kushukia wanakoamini kuwa ni karibu na wanakoelekea au majumbani kwao.