Nawasifu sana wanaharakati kote duniani, ambao wanashikilia suala moja na kulipigania bila woga, bila kujali yatakayowakuta.
Uanaharakati upo wa aina nyingi. Mtu yeyote anaweza kuwa mwanaharakati. Unaingia kwenye kundi hilo iwapo unajaribu kushawishi mabadiliko ndani ya jamii kwa madhumuni ya kuleta mageuzi kwenye siasa, mazingira, uchumi au masuala ya jamii.
Kwa fasili hii, mpiga kura yeyote ni mwanaharakati kwa sababu anapopiga kura anafanya uamuzi wa jinsi gani na kwa muelekeo upi maisha yake yabadilike katika nyanja hizo nilizogusia.
Lakini upo ule uanaharakati wa kiwango cha lami, wa mtu ambaye anajitambulisha kama mwanaharakati au anakubalika ndani ya jamii kuwa ni mwanaharakati. Hana jambo ambalo analikubali, na ni nadra kuonekana anasifia kitu, au kwa kutoona suala la kusifia au kwa kuamini kuwa kazi yake si kusifia bali ni kukosoa tu.
Mwanaharakati wa aina hii akiaga nyumbani kwamba anakwenda kazini, basi tunataka kuamini kuwa huo ni wajibu wake kwa muono wake yeye.
Lakini upo upande wa pili. Kuna mtu ambaye anaaga nyumbani kuwa anakwenda kazini akiamini kuwa kazi yake inamtaka adhibiti harakati za wanaharakati. Kwa mtazamo wake, anakwenda kutimiza wajibu unaompa ruhusa ya kudai mshahara wake mwisho wa mwezi.
Nafanya makusudi kujikita kwenye dhana ya mjadala juu ya wajibu wa mwanaharakati na wajibu wa wadhibiti wa wanaharakati bila kugusia mifano halisi ili kufupisha mjadala. Nigusie tu kuwa mifano halisi ya unaharakati tuliyonayo ni ya wanasiasa walio mstari wa mbele kupigania suala moja au jingine.
Niliyoyasema juu ya uanaharakati wa kiwango cha lami, nayasema bila kejeli nikiamini kuwa ndani ya mipaka inayotuongoza chini ya sheria, wanaharakati nao wanayo nafasi yao.
Lakini bila shaka migongano ipo, tena si kidogo, kwa sababu ya upande mmoja au mwingine kutozingatia sheria zilizopo, au pande zote kutokubaliana iwapo kuna sheria zinazokiukwa au, muhimu pia, kutokuwepo makubaliano juu ya uhalali wa sheria zilizopo.
Naamini kuwa mwanaharakati wa kweli wa kiwango cha lami husukumwa zaidi na matokeo ya harakati zake kuliko kuwa na hofu juu ya athari za kisheria zitakazomkabili. Atakuwa tayari kusimama kizimbani na akikutwa na hatia na baada ya kumaliza rufaa zote, atatumikia adhabu itakayotolewa. Harakati zake ataziendeleza gerezani au zitaendelezwa na wenzake waliobaki nje.
Mwaka 1963 nchini Afrika Kusini wakati wa utawala wa kibaguzi wa nchi hiyo, Nelson Mandela, alitumia fursa kabla ya kuhukumiwa kifungo jela kwa kosa la hujuma, uendelezaji Ukomunisti na kushirikiana na dola za nchi za nje kutoa hotuba iliyoweka msimamo juu ya harakati za Chama chake cha African National Congress (ANC) kuendesha mapambano ya silaha dhidi ya utawala wa kibaguzi.
Alimaliza hotuba yake bila kutetereka kutetea msimamo wake na wa wenzake wa kupinga utawala wa kibaguzi kwa njia ya mapambano aliyosimamia kwa kusema: “…niko tayari kufa…” Huku akitambua uwezekano wa kupewa hukumu ya kifo.
Alihukumiwa kifungo cha maisha na akabaki gerezani kwa miaka 27 mpaka alipotoka jela na akachaguliwa kuwa rais wa Afrika Kusini.
Wanaharakati wa aina ya Mandela, ambao wapo tayari kwa lolote kutokana na harakati zao, hawapo wengi duniani. Lakini tusameheane inapotokea kuwa mara kwa mara wapo wanaharakati tunaowadhania kuwa ni wa aina ya Mandela lakini ukweli ni tofauti kabisa.
Kwenye misafara ya mamba hata kenge wamo. Yapo maeneo ya Uganda ambapo wapo kenge wa Mto Nile ambao ni wakubwa na hukaribia urefu wa mamba. Ukiwaona kwa mbali unaweza kudhani ni mamba.
Wataalamu wanasema tabia zote tunajifunza, kwa hiyo sitadiriki kusema kuwa mwanaharakati huzaliwa. Nitasema tu kuwa si kila mtu anayejiita mwanaharakati anaweza kuhimili mikiki ya wale ambao wanaaga nyumbani kwenda kudhibiti wanaharakati.
Uanaharakati wa kweli unafanyika ndani ya tanuri ambalo si kila mmoja anaweza kuhimili joto lake. Wapo watakaostahamili na wapo wanaotamani tu kuwa na uwezo huo.
Binadamu ana njia nyingi za kujiletea mabadiliko. Hahitaji kujifanya mamba kwa kila suala, lakini anapoamua kujivisha mzigo huo, basi hana budi kutathmini vema uamuzi wake na matokeo yake.
Aliyekuwa mpinzani mashuhuri nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, aliamua akiwa kijana kujiunga na mapambano ya silaha dhidi ya utawala wa ubaguzi wa Rhodesia, lakini alivyokaa msituni kwa muda mfupi akaamua kwamba hayakuwa maisha anayoweza kuendelea nayo. Aliaga na alielezea baadaye kuwa alichukua uamuzi huo kwa kuzingatia kuwa familia yake ilikuwa muhimu zaidi na akarudi uraiani.
Hata hivyo, harakati zake kwenye siasa zilimfikisha kushika wadhifa wa waziri mkuu wa Zimbabwe kati ya mwaka 2009 hadi 2013, akifanikiwa kutimiza lengo la uongozi ingawa si kwa njia aliyoanza nayo.
Kwa wapiganaji wa Zimbabwe waliobaki msituni, Tsvangirai hakuwa na hadhi ya mamba hata kidogo, lakini ni mtu aliyepima joto la jikoni akaamua kwamba halimudu na akaamua kufuata njia mbadala za kuleta mabadiliko.
Somo hapa ni moja tu: ingawa hawana hadhi ileile ya mamba, hata kenge wana nafasi yao ndani ya jamii.