Kwanza nianze kwa kuweka usahihi kwenye kichwa cha habari cha makala iliyopita katika safu hii ya Fasihi Fasaha.  Nilizungumzia juu ya “Usibadili bura yako na rehani”. Bura na rehani ni majina ya vitambaa vya hariri vyenye asili moja ya malighafi hariri ambayo ni nyuzi zinazotokana na viwavi vya mdudu nondo.
 Vitambaa au nguo za hariri zina thamani na ubora mmoja. Tofauti ipo katika usindikaji hariri, utengenezaji kitambaa na uvaaji wake. Rehani (debwani) hutumika kilemba na bura hutumika kikoi. Vyote ni vitambaa vya hariri.
Nilifananisha bura na rehani kama vyama vya siasa; kipwe cha upinzani au cha utawala, kie cha itikadi ya kinyonyaji au isiyo ya kinyonyaji bado ni vyama vya siasa kwa asili yake.


Katika mada hiyo, ukweli niliweka msisitizo kwa wanasiasa wetu waangalie kwanza asili ya vyama na itikadi za vyama vyao kabla ya kuweka misimamo yao na kuhama vyama kwa sababu tu wamekosa waliyoyahitaji.
Kukosa mahitaji iwe imetokana na kuongopewa, kufanyiwa inda, kuwekewa mizengwe au kupinduliwa taratibu za chama  kusiwe ni hati jadidi kwao kuhama chama. La msingi ni kuwa na msimamo na rhati ya moyo katika kushiba itikadi, imani na ahadi za uanachama.
Nilipokuwa naandaa makala ile, mikikimikiki na mitikisiko ndani na nje ya vyama vya siasa ilichipuka mithili ya uyoga msituni na kusambaa haraka nchini kama moto katika nyasi kavu nyikani, kuanzia kwa wanachama, mashabiki, viongozi hadi kwa makada wa vyama. Wote wameingia mkumboni kuhama vyama.
Wapo waliohama kutokana na dhamira zao, wapo waliofuata mkumbo na wapo waliowafuata viongozi wao. Alimradi kitendo cha kuhama kimepewa ufalme wake bila kulinda na kujali rasilimali itikadi, imani, madhumuni na malengo ya chama wanachotoka na chama wanachoendea.


Uyoga ule uliochipua msituni na moto ule uliosambaa nyikani, tayari umeleta kizaazaa kwa watu mbalimbali kukejeli, kusimanga, kusuta na kuweka hoja na maswali yanayohitaji majibu safi yasiyo na shaka ndani yake. Kipi hasa kilichowachopoa hadi kuhama vyama?
Wanapohama vyama wanalenga mambo gani katika uhai wa vyama vyao na mustakabali wa Taifa letu, linalohitaji kuwa na nguvu za kiuchumi, kiulinzi na kiutamaduni ili kurudisha utu wa wananchi na wasiendelee kunyanyaswa na kunyonywa na watu wenye nguvu za kiuchumi.
Baadhi ya wanaharakati, wasomi, viongozi na wananchi wanasema kuwa mtu kuhama chama ni haki yake ya kidemokrasia na ni uhuru wake kikatiba wa kwenda popote na kufanya lolote alimradi asivunje sheria. Kwa maana hiyo ni ruhusa kuhama.


Je, kuhama huko kuna tija kwa nani; kwa mtu binafsi au kwa Taifa? Ni kweli lengo la kuhama ni kuleta mabadiliko katika uongozi, utawala na uchumi huko aendako? Mbona vyama vyao vina itikadi, sheria, kanuni na taratibu za kufanya mabadiliko ya demokrasia ya kweli na utawala bora wa kuthamini utu wa mtu? Aidha, kuwapeleka kwenye nguvu za kiuchumi na pato la kila mtu?
Wanapohama wanatafuta nini? Wanapokuwa ving’ang’anizi katika mahitaji maana yake ni nini? Zinapotolewa nukuu katika hotuba na kauli za viongozi waasisi wa Taifa hili kinyume na maana na malengo ya waasisi hao, maana yake nini kwa hao wahamaji?
Maswali na hoja kama hizo zinatolewa katika vikao visivyo rasmi huko mitaani, vijiweni na hata maofisini. Wanaohoji wana sababu zinazowakereketa hadi kunena hivyo. Kwa hili mimi sina la kushadidia wala kujadili.


Binafsi nakerwa ninaposikia watoa hoja wanapomsakama mtu mmoja kuonekana ana uchu wa madaraka wakati wapo tele  wenye uchu wa madaraka na fedha. Je, kumtusi au kumpiga mgombea mwenzake katika nafasi waitakayo aikose, si uchu wa madaraka?
Wiki iliyopita nilisema katika mchakato huo wa kuhama vyama, wanaofaidika kwa asilimia kubwa ni vyama vile vinavyowapokea wahamiaji. Vyama hivyo vinakuwa katika chereko chereko za kuongeza idadi ya madiwani na wabunge.
Kutoa rushwa ya fedha, nguo, vyakula au ngono siyo vitendo vya uchu wa madaraka? Kumfitini mgombea mwenzako ili asiwe katika kinyang’anyiro hicho si uchu wa madaraka? Ni kweli mtu yeyote ana wajibu wa kuomba uongozi ili awe na madaraka, lakini si kila mtu aombe uongozi. Sasa fujo na hiyana za nini wakati wa kuomba hayo madaraka? Mabadiliko yatafutwe kwa amani na usalama.