Toleo lililopita kupitia gazeti hili nilitoa makala yenye ushauri kwa Rais Jakaya Kikwete asizungumzie usalama wa nchi nyingine na ajikite kutatua matatizo ya kiusalama na tishio la kutoweka kwa amani kwenye nchi yetu kabla ya kuwashauri viongozi wa nchi nyingine.

Hii ilitokanana ushauri wake kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda uliozua nongwa na maneno yasiyokuwa na afya kwa mustakabali wa amani ya nchi zetu mbili. Ni matumani yangu kuwa Mheshimiwa Rais hakuubeza ushauri wangu na kwa uungwana wake naamini ameuchukua na kuufanyia kazi kwa dhati ushauri huo kama nilivyo muomba maana siamini kuwa ameufanya kuwa shuruti au amri bali amekuwa na hiyari na moyo wa dhati kuukubali.

 

Leo baada ya kusherehekea kwa amani na upendo sikikuu ya Eid el Fitri, kwa dhati kabisa naunga mkono kauli ya Rais wetu JK alipokuwa anahitimisha ziara yake majuzi mkoani Kagera. Alipokuwa Kagera nilimsikia Rais akiwakoromea baadhii ya watendaji wa serikali nakuwaambia “Tanzania sio shamba la bibi”

 

Alitoa kauli hiyo akiwakemea maafisa wa serikali yake kwa kufanya mambo ndivyo sivyo ikiwa ni pamoja na kugawa ardhi kwa wageni na kuwapa hifadhi bila kufuata taratibu za kisheria. Alisikika akiwaambia maafisa wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kuwa “Kuna mtu anaitwa Kangole. Anaishi kule mpakani Mtukula ndiye anayeingiza wahamiaji nchini, ameshajua bei zenu anawahonga anaingiza watu wake ushahidi upo, PCCB mnafanya nini?”

 

Nikimsoma JK katikati ya mistari kupitia kauli hiyo naona naye alikuwa analalamika tu kama mimi ninavyomlalamikia raia mwenzangu wa kawaida. Sikuiona tofauti ya kuwa mwajiri mkuu na Amiri Jeshi Mkuu na mtu kama Mtoi wa Kijiji cha Milungui kule Lushoto, anayelalamika na mwanakijiji mwenzie kuhusu suala la maji!

 

Baada ya kauli hiyo JK aliwataka wageni walioingia kinyemela wafungashe virago warudi kwao na kuwataka watendaji na maafisa wake wafuate taratibu maana Tanzania si shamba la bibi. Na kweli “Tanzania sio shamba la bibi kila mtu ajifanyie tu anavyotaka.”

 

Mimi naunga mkono kauli hii kwa asilimia 1000 kama wale jamaa waliozoea kusema ndiooo huku wanapiga yale madawati na kuzunguka kwenye vile viti kana kwamba wao ni kutoka sayari nyingine hata kama wakiwa wanapitisha muswada au maamuzi ya kwenda kumtaabisha na kumkandamiza mpiga kura wao.

 

JK anasema Tanzania sio shamba la bibi huku majuzi tu watu 9 pamoja naaskari wawili wa kituo cha Oysterbay walikamatwa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wakiwa wanasafirisha vipande 70 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 305 ambapo meno hayo kimahesabu ni sawa na tembo 35.

 

Thamani yake ni zaidi ya shilingi 805 milioni. Tembo hao ni wa humuhumu Tanzania ambamo ndio JK anasema si shamba la bibi. Kwa nini nisiungane naye kwa kusema kuwa Tanzania si shamba la bibi ili watu hawa waziache tabia zao?

 

Si huenda wakasikia sauti zetu kwa sababu zitakuwa za watu wawili? Nikiwa naungana na Rais wetu anayeiongoza Serikali kuwaambia watendaji wake kuwa “Tanzania sio shamba la bibi” kwenye vyombo vya habari nimesikia eti askari magereza watatu watiifu kwa viapo vyao na kwa muajiri wao mkuu na amiri jeshi wao mkuu ambaye ni JK, wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara walikamatwa wakiwa na gari la jeshi lamagereza likiwa na silaha limepakia nyara za serikali zikiwemo twiga, pundamilia,  swala na mbuni wenye thamani 56 milioni.

 

Vyote hivyo vikiwa vimetoka kwenye shamba hili hili ambalo tuna sema leo sio shamba la bibi. Mimi najiuliza; kwani bibi alimuachia nani alilinde shamba hili kama babu hayupo? Na huyo babu alimwambia nani kuwa hili sasa ni shamba la bibi?

 

Kabla mshangao wangu haujakoma, kwenye pekuapekua yangu nikakutana na kioja kingine eti ofisa mmoja wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ana kesi ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni nne.

 

Nikapigwa na bumbuwazi! Huyu si ndio mlinzi wa shamba la bibi? Inakuwaje tena naye anakutwa na mali za shamba la bibi kinyume cha sheria? Hivi hili shamba limelaaniwa na nani? Mbona hata walinzi nao wanamhujumu bibi?

 

Kwani babu hana nduzu zake wengine wamsaidie bibi anayeonekana ameshindwa kulinda shamba? Nikiwa najiuliiza na kutafakari kauli kuwa “Tanzania sio shamba la bibi” huku nikitaka kuamini kweli kuwa sio shamba la bibi nakumbuka kampuni zote za madini nchini ambazo zinachimba madini sehemu mbalimbali kwenye ardhi ya Tanzania (shamba la bibi).

 

Kampuni hzi zinatuachia mashimo ambayo hatutaweza hata kuyafugia samaki. Nakumbuka kuwa zina misamaha mikubwa ya kodi, ukiachilia mbali gawio kiduchu tunalo pata. Kwa mujibu wa taarifa ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wahesabu za serikali (CAG) misamaha ya kodi iliyotolewa kwa kampuni za uchimbaji madini pekee kwa mwaka 2011 ilikuwa Sh bilioni 109.

 

Jumla ya misamaha iliyotolewa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) ikifikia Sh bilioni 239. Taarifa za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zinabainisha kuwa ingawa katika miaka mitano ilopita (2008 – 2011) mapato ghafi ya dhahabu yameongezeka kutoka US$ 500 millioni hadi US$ 1.5billioni kwa sababu yakuongezeka uzalisha na bei ya dhahabu, lakini mapato kwa serikali yamebaki kuwa US$ 100 millioni kwa mwaka kwa wastani.

 

Hii imesababishwa kwa kiasi kikubwa na msamaha wa kodi kwa kampuni (Corporate income tax holidays). Kwa hakika hakuna kampuni hata moja iliyowahi kulipa kodi hii hadi 2012. Taarifa ya IMF inaonesha pia kwa kuzingatia hali hii, hakuna mategemeo kuwa kipato kutokana na madini kitaongezeka.

 

Taarifa ya Tume ya Bomani ilikadiria serikali kupoteza Sh bilioni 39.8 mwaka 2006/7 na Sh bilioni 59 kwa mwaka 2007/8 kutokana na msamaha wa kodi ya mafuta tu (fuel levy exemptions) kwa kampuni sita tu. Kufikia mwishoni mwa 2011, kampuni za uchimbaji madini zilikuwa zinadai takribani US$ milioni 274 kurejeshewa kutokana na msamaha wa kodi hiyo.

 

Tanzania haliwezi kuwa shamba la bibi, tuungane na JK kuwaambia watendaji wake hivyo. Kama “Tanzania sio shamba la bibi”, kwa nini kampuni zote za simu nchini zina misamaha ya kodi wakati tunajua kuwa biashara ya mawasiliano kwenye kampuni hizo inawaingizia faida kubwa sana huku serikali ikiwa hainufaiki?

 

Nani anaweza kuthubutu kusema kuwa kampuni za simu zinajiendesha kwa hasara na hivyo hazipati faida yoyote kwenye hili shamba la bibi? Na kwamba kutokana na hilo kuziondolea misamaha nikuwaudhi wajukuu wa bibi?

 

Mbali na hilo, nani hajui kuwa kampuni zote zilizo kwenye EPZA zina misamaha ya kodi? Kwa nini tuzisamehe kodi kampuni hizi kubwa halafu tukimbizane na mia tano za machinga wa pale Mwanza na kwingineko?

 

Au ni laana ya yule babu mwenye shamba lake aliyesema “Serikali ya wala rushwa haikusanyi kodi kwa watu wakubwa bali inafukuzana na vijitu vidogo vidogo” ndo tunaishuhudia? Takwimu za mwaka 2011/2012 zinaonyesha kuwa jumla ya misamaha ya kodi kwenye kampuni zote ni shilingi 1.8 trilioni sawa na 4.3% ya pato laTaifa (GDP).

 

Kama tunasamehe kiasi chote hicho cha fedha huku walimu wakiwa na madai yao muhimu ambayo serikali kila kukicha inayapiga danadana tunaweza kweli kuthubutu kusema Tanzania sio shamba la bibi na hivyo tuungane na JK tupaze sauti zetu tuseme kwa pamoja kuwa”Tanzania sio shamba la bibi”?

 

Hivi wenye akili watatuelewa kweli? Tena ikiwa ni siku kadhaa baada ya twiga wetu kuchukuliwa sijui ni bure au kwa bei sawa na bure na kusokomezwa vichwa na kuingizwa kwenye ndege ya Waarabu pale uwanja wa kimataifa wa ndege (KIA), huku eti serikali ikiwa haijui kuwa kuna viumbe hai kutoka kwenye shamba la bibi vimeibiwa?

 

Hivi, na wale walioficha fedha Uswiss wameona hazifichiki kwenye hili shamba la bibi au wameona sio mwafaka kuficha fedha kwenye mabenki ya shamba la bibi? Kwa nini wahangaike kwenda kuzificha nje kama zilipatikana kihalali kwa mauzo ya mazao kwenye hili shamba la bibi au kama ujira uliopatikana kutokana na kazi halali kwenye hili hilishamba la bibi?

 

Au kwani kuna utaratibu mgeni wa kuficha nje vinavyopatikana kwenye shamba la bibi? Kama ndio, je, unafuata sheriana taratibu za shamba la bibi? Ndugu zangu, mtakumbuka kuwa kuna na lile swala la rada ambalo baadae tulirudishiwa chenji yetu.

 

Hivi walioingia dili na wale Wazungu wa BaE System walilinda shamba la bibi kweli au nao waliingia kila mtu akajichumia miwa na matunda na kujaza tumbo lake?

 

Mimi huwa nawaza hadi naumwa na kichwa! Kama hayo hayatoshi eti kuna meli za mafuta za Iran zilipeperusha bendera ya Tanzania baada yakuwekewa vikwanzo vya kimataifa kutokana na mpango wao wa silaha za nyuklia.

 

Imewezekana vipi kitenge kizuri cha bibi ajifunge mtu mwingine wenye bibi tusiambiwe? Hii ni dharau au heshima yenye ridhaa ya dhihaka? Labda pia tukumbuke tulikotoka ili tuamue pamoja kama kweli “Tanzaniani shamba la bibi au sio shamba la bibi”. Ile kampuni ya Deep Green Finance ilichota kiasi cha shilingi 10 bilioni pale BoT kwenda kwenye kampuni isiyojulikana, eti pesa ziende kusiko julikana? Kweli?

 

Meremeta nayo inatuhumiwa kukwapua zaidi ya 155 bilioni kwenye akaunti ya madeni ya nje EPA, kampuni ya Kagoda nayo kupitia EPA ambayo mpaka sasa wananchi wengi wanajiuliza kuwa ilikuwa ya nani ukaguzi uliofanywa na kampuni ya Enerst and Young ulionyesha kuwepo kwa ufisadi uliotumia hati ya kughushi ikiwa ni pamoja na viwango visivyo sahihi vya kubadilisha fedha.

Ukaguzi ulionyesha kati ya 133 bilioni malipo zaidi Sh 90 bilioni yalifanyika kwa kutumia hundi za kughushi ikiwa ni pamoja na kampuni ya Kagoda iliyokuwa kinara wa wizi kwa kuchota Sh 40 bilioni. Yupo aliyekuwa mgombea mmoja wa chama cha upinzani aliwatuhumu mgombea wa chama hasimu kuwa fedha za EPA zilimuingiza madarakani.

 

Japo madai hayo hayajawahi kukanushwa, tukubali kwa muda kuwa yalikuwa madai ya uongo. Je, na hizo kampuni zilizochota na kukausha hazina yetu zimechota kwenye shamba la nani? Ni la bibi huyu huyu au bibi mwingine wa babu mwingine?

 

Kama Tanzania si shamba la bibi litakuwa shamba la nani baada ya bibi tunayemsingizia kuwa ndiye mwenye shamba kuendelea kukaa kimya huku watu wakizidi kujichotea kwa makarai? Wengine mnaweza kuungana na mimi kwa dhati kabisa bila mashaka yoyote kuunga mkono kauli ya JK kuwa Tanzania sio shamba la bibi?

 

Na je, tukikubaliana kuwa Tanzania si shamba la bibi mnaweza kuwa tayari kuwataja wanaolimiki shamba hili na kulinajisi kwa namna watakavyo wao kwa kuwa wao wanajiona kuwa ni Watanzania zaidi wenye hati miliki ya shamba la marehemu babu kuliko Watanzania wengine?


Mwandishi wa Makala haya anapatikana kwa Na:

+255 (0)713246764 au +255 (0)784246764