Na Padri Stefano Kaombe
Kati ya vipindi muhimu kabisa vya kiliturujia katika Kanisa nikipindi cha Kwaresma, wengi wetu tuna kumbukumbu nyingi kuhusiana na kipindi hiki, hasa kaidadini ya kupakwa majivu siku ya Jumatano ya Majivu, Njia ya Msalaba kila Ijumaa, kufunga, kutopiga kinanda na ala zingine wakati wa kuimba na hasa utajiri mkubwa wa nyimbo za kipindi hiki. Makala hii, inapenda kukazia mambo matatu muhimu katika kipindi hiki nayo ni Ubatizo, Kufunga na Tabia njema.
a). Ubatizo: Kipindi chote cha Kwaresma, ni kipindi cha maandalizi ya ubatizo, kwa wakatekumeni kuingizwa katika imani na sisi tuliokwisha kubatizwa kurudia ahazi zetu za ubatizo siku ya Kesha la Pasaka, kilele cha maandalizi haya yote. Maandalizi haya ya karibu ya wakatekumeni tunayaona katika Dominika za Kwaresma kwa uwazi: Dominika I wanateuliwa, Dominika III, wanafanyiwa ‘takaso’ la kwanza, Dominika IV, wanafanyiwa ‘takaso’ la pili na Dominika V wanafanyiwa ‘takaso’ la tatu.
Kuna uhusiano mahususi kati ya Jumatano ya Majivu tunapofungua mlango wa Kwaresma na Kesha la Pasaka, tunapoadhimisha kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Kupakwa majivu ni ishara ya kifo, kwani Maandiko Matakatifu yanaweka wazi kabisa, Mungu alimwambia Adamu: “Kwa kuwa wewe ni uvumbi, nawe utarudi katika uvumbi” (Mwz 3:19). Laana hii ya kupotea katika uvumbi, Bwana wetu Yesu Kristo anaibadirisha kwa sadaka yake msalabani na siku ya Pasaka, anaupatia ulimwengu zawadi aali ya utukufu wa ufufuko wake. Ndio hija yetu hapa duniani, tutoke katika vumbi, katika kiza tuelekee katika utukufu, ndio maana katika Kesha la Pasaka tunaanza na kaidadini ya mwanga, tutembee maisha yetu yote katika nuru ya ufufuko.
Katika kipindi cha Kwaresma, tuwaombee wakatekumeni wajiandae vyema kuipokea imani ya Kristo Mfufuka. Kwa wabatizwa, ni wakati wa kuketi na kutafakari safari yetu: ninaikumbuka hata tu siku yangu ya ubatizo? Je, hija yangu hapa duniani ni yenye unyofu, tunatembea katika mwanga wa Kristo? Je, vazi jeupe tulilopewa siku ya ubatizo wetu linang’aa kwa uadilifu au hata tu silijui hata linipolitupa? Mafuta ya wakatekumeni na ya Krisma tuliyopakwa siku hiyo bado yanafanya nafsi zetu kuendelea kuwa laini na kung’aa kwa utakatifu na ukarimu? Midomo yetu na masikio yetu inasikia na kutangaza Habari Njema ya Kristo Mfufuka?
b). Kanisa limeruhusu desturi ya kufunga, inaisisitiza na nyakati nyingine imeiagiza: Funga siku ya Jumatano ya Majivu… Mwalimu wa Kanisa wa Malaika Tomaso wa Akwino anatuambia kwamba tunafunga kutokana na malengo matatu: “Kwanza, ili tuweze kutiisha hatamu (kutiisha) tamaa za mwili… Pili, tunakimbilia kufunga ili kwamba akili zetu kwa uhuru ziweze kutaamali mambo ya mbinguni… Tatu ilikufanya malipizi ya dhambi zetu…”
Mt.Basili Mkuu yeye naye alithibitisha umuhimu wa kufunga kwa ajili ya kujilinda dhidi ya nguvu za kishetani, anatuambia: “Kufunga ni silaha ya kujilinda dhidi ya mashetani. Malaika wetu walinzi wanakuwa wako tayari kukaa na wale ambao wamesafisha roho zao kwa kufunga.”
KKK inatuelezea juu ya umuhimu wa kufunga, mosi kwa ajili ya toba ya ndani 1434, inataja kipindi cha kwaresma na hasa kila Ijumaa yake kuwa ni nyakati nzito za toba 1438. Pili, tunafuata mfano wa Yesu ambaye alienda jangwani kwa siku arobaini kufunga 534-40, soma Mk 1:13. Pd.Thomas Kinkead katika andiko lake juu ya ufafanuzi wa KKK aliandika “Tukumbuke kwamba ni miili yetu ndiyo inayotuingiza katika dhambi, hivyo, kama tunauadhibu mwili kwa kufunga na kujitesa, tunafanya malipizi ya dhambi zetu, hivyo Mungu anafuta sehemu ya adhabu yetu ya muda kwa mfungo wetu huo.
Papa Leo Mkuu katika mwaka 461 kwa hekima alitoa ushauri kwamba kufunga ni njia na si lengo lenyewe. Kwa wale ambao hawawezi kufunga kwa dhati kabisa, kwa hekima alishauri, “Kila tunachokiacha kwa kufunga kitolewe kama msaada kwa maskini.” Kuacha kufunga, hata kwa sababu stahiki za afya, hakumsameheshe mtu kuacha kutimiza agizo la kila mmoja wetu la kufanya toba (soma Lk 13:3 “Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo”). Tunapaswa kusema kwamba hatupati thawabu kwa kufanya malipizi, hata kama ni makali hivyo, kama tupo katika hali ya dhambi ya mauti. Kuwa katika hali ya neema ni muhimu sana ili kupata thawabu kwa kufunga.
Kujifunza kile ambacho tumekipoteza ni hatua ya kwanza katika kugundua upya urithi wetu. Kwa namna gani tufunge kama Wakatoliki? Zamani, kufunga kulikuwa ni muhimu kwa maisha ya kikatoliki kama vile ilivyo kwa Misa ya Dominika. Karibu theluthi moja ya siku katika mwaka zilikuwa ni siku za kufunga na 2/3 ya siku zilikuwa za kujikatalia. Si siku zote za kujikatalia zilikuwa siku za kufunga, lakini siku zote za kufunga zilikuwa pia ni siku za kujikatalia. Kila mmoja wetu anapaswa kuwasha moto wa kuishi Misa, uchaji na desturi njema za Kikatoliki ili jiwe kwa jiwe, tofali kwa tofali tuujenge ufalme wa Kristo.
Mt. Fruktuoso, askofu mtakatifu wa Taragon huko Hispania, wakati wa madhulumu ya Mfalme Valeriano katika mwaka 259, alichukuliwa msobe msobe kwenda kuuawa siku ya Ijumaa saa nne asubuhi. Alipopewa maji anywe aliyakataa, kwani muda wake wa kumaliza mfungo wake ulikuwa haujafika. Mtakatifu huyu japokuwa alikuwa amechoka sanakutokana na mateso ya gerezani na alikuwa na hitaji la kuwa na nguvu ili aweze kuvumilia maumivu yake ya mwisho, lakini alibaki kuwa thabiti: “Niko katika funga, hivyo nakataa kunywa maji, haijafika saa kenda; hata kifo chenyewe hakiwezi kunilazimisha mimi kuvunja funga yangu.”
Huu ndio aina ya uchaji tunaopaswa kuuonesha katika mfungo wetu wa Kwaresma, katika kutii amri ya Kanisa…
Unapofunga jiulize, Je, funga yangu hii ni ya toba, najutia udhaifu na upotovu wangu? Je, funga hii inafanya nijue shida na mahangaiko ya wasio nacho, hivyo kujitambulisha nao? Je, funga hii inanifanya niwe mkarimu zaidi kwa wengine, kwa utayari wangu wa kuwa karibu na na kuwasaidia kwa kadiri ya uwezo wangu? Funga yangu hii inanipa ushujaa wakumkataa shetani na anasa zake zote? Je, funga yangu inanisaidia kuingoa kabisa mizizi ya dhambi katika nafsi yangu?
c. Kipindi cha Kwaresma kinapaswa kutawaliwa na tabia njema, kwa kila mtu na kila familia. Tabia hii tuzipande kwenye udongo mzuri wa nafsi zetu, tuzimwagilie kwa maji ya ubatizo, tuzipalilie kwa toba ili mwisho Bwana wetu Yesu Kristo atujalie zawadi ya uzima wa milele. Ni tabia za kikwaresma, lakini hasa zinapaswa kuendelea kuwa tabia zetu njema za kila siku, maisha yetu yote. Kwaresma hii itujengee stamina na uwezo wa kuendelea daima na tabia hizi. Si kila mmoja anaweza kuziishi zote, inategemea, uwezo, mazingira na hali yake. Zile unazoziweza au unayoiweza iishi kishujaa, watu wakutambulishe kwa tabia hiyo. Mfano mzuri ni Familia Takatifu, wao walikuwa na tabia njema tambulishi ya familia yao, wao kila mwaka walikuwa wanaenda Yerusalemu kwenye sikukuu, hii ilikuwa ndio desturi yao (soma Lk 2:41f). hapa tunataja desturi njema mbalimbali bila kuzingatia uzito wake:
- Angalau siku moja kwa juma, iweke kwa mlo wa kibiblia au wa kitamaduni, achana na vyakula vya viwandani: dafu badala ya soda, muhogo badala ya mkate, ugali au ndizi badala ya baga au piza.
- Bidii katika kazi, wajibika pale ulipo, usisubiri kusukumwa, tumtazame na tumwige Mt. Yosefu, “mfano wa watu wa kazi.”
- Chagua changamoto ya kimazingira. Acha kiyoyozi, maji ya baridi, panda mti, usitupe tupe hovyo chupa za plastiki na uchafu. Kila mmoja wetu anapaswa kuwa kinara wa kutunza ikolojia yetu. Kwaresma hii boresha mazingira yako.
- Funga, hata siku moja kwa juma, mf Ijumaa au kupunguza mlo, kuacha aina fulani cha chakula, mf kitimoto! Acha pombe! Huu ni wakati mzuri wa kujikatalia vile visivyo vya lazima, mf kwenda saloni!
- Jifunze historia za watakatifu. Wafundishe watoto wako mambo ya ajabu yaliyofanywa nao kwa ajili ya Kristo. Hata wewe leo, binafsi au na familia yako yote mwaweza kuwa watakatifu. Familia ya Josef na Wiktoria Umma na watoto wao wote saba kutangazwa kwao kuwa wote ni watakatifu kutokana na kifodini chao wakati wa Vita Kuu II ya dunia, kwa kuwahifadhi Wayahudi dhidi ya Wanazi, ni mfano kwetu kuwa nasi sote twaweza kushikana pamoja kama familia na kuwa watakatifu.
- Jifunze neno moja au mawili ya Kilatini katika juma, nahasa kile cha Misa, iwe Kyrie eleison au Pater Noster!
- Jijengee desturi ya kujisomea Maandiko. Kumbuka maneno ya Mt. Yeronimo: “Kutojua Maandiko ni kutomjua Kristo.” Kamwe hatuwezi kuwa “wakristo,” kama hatuchukui juhudi binafsi za kujisomea, kutafakari na kuweka katika matendo Neno la Mungu.
- Jitolee, maisha yana shughuli nyingi na ni kukimbizana na muda na pesa. Saa yako moja kwa ajili ya wengine ina maana sana, kuwasaidia wahitaji, kujenga urafiki mpya.
- Kama u mzazi, fuatilia malezi ya watoto wako: je, wanafanya vizuri shuleni? Je, jirani wanasema nini juu yao, kweli wanapendwa na Mungu na jirani kama alivyokuwa mtoto Yesu?
- Kuwa na kitabu chako cha sala ambao umezitunga mwenyewe kwa matumizi yako binafsi. Kumbukumbu kubwa ya pale ulipohitaji uongozi au msaada, nyakati za furaha au huzuni. Leo hii tuna sala mbalimbali maarufu, sala ya Mt. Inyasi, ni kwa kuwa kuna watu walikaa chini na kuandika fikra na tafakari zao.
- Kuwa na moyo wa shukrani. Hakika asiye na moyo wa shukrani, si mfuasi wa Kristo. Mbele yao uwepo wema au ubaya, joto au baridi, urafiki au uadui, kusifika au kulaaniwa, uwe na shukrani.
- Ni wakati wa sakramenti zaidi, hasa Ekaristi na Kitubio. Kwaresma hii isipite bila kwenda kuungama, aidha, usibaki tu kushiriki Misa siku za Dominika, jiongeze katikati ya juma pia.
- Rozari ya familia, hapa na pale vikwazo, ila msonge mbele, wafundishe wanafamilia. Wahenga walituambia “Nani kama mama?” Vivyo hivyo, nasi kuwa karibu namateso ya Yesu, kujua ukuu wa sadaka yake kwetu, tunapaswa kukaa miguuni mwa Mama Maria na kujifunza toka kwake, kutafakari pamoja naye kama watoto watii na wema.
- Sali zaidi, weka muda maalum, pahala pa sala. Sala nikuzungumza na Mungu, huwezi kumpenda mtu bila kuwa na mawasiliano naye. Tujenge mawasiliano thabiti naMungu kwa njia ya sala.
- Sikiliza nyimbo za dini. Ni sehemu muhimu ya imani yetu, zenyewe zinasaidia kutuinua na kumtazama na kumsikiliza Mungu. Nyimbodini ni muhimili muhimu katika maisha yetu ya kiroho, tuwe na huzuni au furaha, bado utupa tumaini kuu la msaada wa Mungu na faraja yake. Kipindi hiki cha Kwaresma, ziwe kama kivuli chetu, popote tutembeapo, kuchota neema au kusambaza neema.
- Tembea kwa miguu mapema asubuhi tafakari juma lililopita au lijalo. Mshukuru Mungu kwa mema yote, shukrani itakupa nguvu mpya, hewa safi ya kiroho katika mapafu yako.
- Wahi kanisani. Huu ni ugonjwa sugu. Hakika kama wewe ni mmoja wa “manunda” wa kuchelewa kanisani, kama utafanikiwa angalau tu kuung’oa mzizi pori na kurofi huu wa uchelewaji, utakuwa umepiga hatua kubwa mbele kuwa karibu na Kristo.
- Zima mitandao ya kijamii, angalau saa moja kwa jioni moja kwa juma. Jisomee, andika sala, kaa na familia kwa masimulizi matakatifu.
Haya ni machache katika hija yetu ya maisha ya kiroho, ila kila mmoja kwa neema ya Mungu ana uwezo wa kujijenga kiroho kwa kuwa na tabia njema. Tabia hii unapaswa kuianza leo, kamwe usingoje kesho, kwani kesho ni ya mchimba kaburi. Kama utajikubali kuwa wewe ni mavumbi, kwa hakika hakuna chochote kitakachoweza kukuzuia usiwe karibu na Kristo, shuhuda wa ukweli huu ni Mt. Paulo Mtume:
Ni nani atakayetutenganisha na upendo wa Kristo? Je, nidhiki, au ni shida au adha au njaa au uchi au hatari au upanga? Lakini katika mambo hayo yote tunashinda nazaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo wala wenye uwezo. Wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakiwezi kukutenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu (Rum 8:35ff).
Kwaresma njema.
Parokia ya Roho Mtakatifu: Kitunda
Jumatano ya Majivu 2024.