Kwani pale walipotumia chopa tatu kufanya mikutano ya hadhara katika kata 27 kugombea udiwani wananchi si waliwajibu kwa kupata kata tatu tu kati ya hizo 27? Au hivi karibuni walipotumia nguvu yao kubwa katika kuomba Jimbo la Kalenga, hata Chopa ilitumika, mbona wametoka kapa na kiti kikaenda kwa CCM kwa kishindo? Hivyo vyote si vinaashiria kutokubalika kwao? Kwanini hawasomi ishara za nyakari na wakatambua mbinu hiyo ya mikutano ya hadhara na wananchi haina tija?
Njia pekee na ya hekima na busara kwa UKAWA ilikuwa kuzungumza tatizo lililojitokeza bungeni na Mwenyekiti ili kamati ya maridhiano au ya uongozi au ile ya maadili ya Bunge ilitafutie ufumbuzi kuondoa mipasho na kejeli ndani ya Bunge.
Kinachohitajika hapa ni akili za kawaida tu yaani “common sense” wala siyo huruma (sumpathy) ya Wazanzibari. Haiji akilini kwa viongozi wa Tanganyika kupanda boti kwenda Unguja kutafuta huruma kutoka kwa Mwarabu. Hili linatukumbusha enzi za Sultani wa kwanza wa Zanzibar, Seyyid Said (1840-1856), alipojigamba kuwa “filimbi (zumari) ikipigwa Unguja, watu wa Kigoma wanacheza” ndiyo tunaiona leo CUF Zanzibar, lakini Wabara kwa hiari yao wanacheza na wanakwenda kutoa ripiti ya yaliyojiri bungeni mjini Dodoma! Je, huko siyo kujishusha (be subjective to Zanzibar) sisi Wabara?
Iliaminika kule Visiwani siku hizo kuwa wenye nchi walikuwa Waarabu na watu weusi walionekana kuwa wageni tu wa kutoka Bara. Ninayakariri haya kwa kuwa historia ina tabia ya kujirudia matukio yake. Huko nyuma gazeti la Arab Association lililoitwa “ALFALAQ” lilipata kuandika haya: “Wanachama wengi wa African Association ni wageni.” Wakati huo huo, gazeti la Waafrika wa Zanzibar “AFRIKA KWETU” lilipinga maoni hayo ya Waarabu liliposema “Sisi watu weusi wa Unguja na Pemba tumeshtushwa kujua kwamba wahamiaji wachache wana njozi za ajabu na potofu kwamba Visiwa vya Unguja na Pemba siyo nchi halali za Waafrika bali kwa bahati mbaya Waafrika wamejikuta katika visiwa hivi.
Mtu yeyote mwenye njozi kama hizi lazima afahamu kwamba anajidanganya”. (SOMA MAPAMBANO YA UKOMBOZI – ZANZIBAR – TPH uk. 63).
Kutokana na mawazo pinzani ya aina hiyo, hata Wazungu walikuwa wanawaona Waafrika wa Zanzibar kama watu wa hali ya chini ya Waarabu na Wahindi. Basi Mzungu mkoloni alionesha hali hiyo kwa kuandika hivi, ninamnukuu: “Waafrika kule Zanzibar walikuwa kama watoto ambao wana hulka za Waarabu ambao wamewafunza.”
Akaendelea: “Mwarabu kule Zanzibar anapewa heshima sana na Mwafrika” (soma MAPAMBANO YA UKOMBOZI ZANZIBAR – TPH uk. 28 na 29 foot notes).
Kwa mtazamo wa aina hii, hata Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitolea mifano ya unyonge wa Mwafrika kule Visiwani kwa mifano kadhaa.
“Juzi juzi tu wakati wa Vita Kuu ya II watu wa Zanzibar walidiriki kubadili majina yao ya asili yasifanane na Uafrika. Tunao mpaka sasa wanaobadili majina; Athmani anajiita Othman, Bakari anajiita Abubakar, Mgomi anajiita El-Mughumi, aukwepe Uafrika. Ukiwa Mwarabu kule Visiwani wakati ule wa vita unaweza kupata mchele. Lakini Mswahili hivi hivi hupati mchele (unapata dona/maharagwe au kauzu).
“Sasa ukiweza kuukwepa Uafrika ukajifanya Mwarabu utapata mchele. Na huku pwani sifa ya Mwarabu ni lugha, maana mama wa Kiswahili akikushukuru husema asante Mwarabu wangu, ndiyo anakusifu hivyo mama wa Kiswahili.” (Nyerere: Ujamaa ni Imani uk. 10). Hotuba aliyotoa kwa vijana Diamond Jubilee Jumamosi tarehe 30 Mei 1969, hapa imeonesha unyonge wa mtu mweusi, hasa kule Visiwani.
Sasa unaposikia viongozi wa UKAWA wote weusi wanakwenda Zanzibar kule watu weusi walikokandamizwa kwa miaka 50 iliyopita, unajiuliza vipi Wanatanganyika kwenda Visiwani kumwona nani? Ili iweje? Huu ni msukumo wa itikadi au ni katika kutafuta ulaji zaidi?
Bado inashangaza. Tangu lini CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi wakala sahani moja? Wakawa wamoja? Mbona itikadi zao zinatofautiana sana?
Vita yoyote inapiganiwa katika viwanja vya mapambano. Hapa pana VITA ya KATIBA. Na vita hii uwanja wake wa mapambano ni ndani ya Bunge Maalum la Katiba. Mimi ninavyomfahamu Profesa Lipumba kama askari katika Kambi ya JKT Ruvu miaka ile ya 1973 alikuwa mvumilivu sana, hodari katika kazi. Ile mikikimikiki yote ya ulikruti aliimudu bila ya kupata adhabu kwa utovu wa nidhamu au uzembe (malingering). Nikimwita mlugaluga wa Kinyamwezi ni mpiganaji.
Niliposikia uvumilivu wa vineno vya hovyo hovyo mle ndani ya Bunge vimemshinda sikuamini. Ile “endurance” yake yote imeyeyukia wapi askari huyu hata akimbie mapambano ya maneno? Kwanini alikata tamaa upesi vile? Ule moyo wake wa kupambana mpaka kushinda (his fighting spirit for a just cause) umekwenda wapi?
Labda niwakumbushe wana UKAWA kwamba kukata tamaa na kukimbia kutoka uwanja wa mapambano ni dalili ya kushindwa (despair is for the defeated). Ni kweli Profesa Mwenyekiti wa UKAWA na wenyeviti wa Chadema na NCCR-Mageuzi mko tayari kuwasaliti wanachama wenu kwa kukimbia kutoka uwanja wa mapambano, yaani Bunge Maalum la Katiba? SIAMINI na wala SINTOELEWA.
Wakati wa Vita Kuu ya II Uingereza, alitokea kiongozi shupavu wa Waingereza akiitwa Winston Churchill. Huyu alipiganisha vita katika Bunge la Uingereza. (House of Commons – Parliament), hakwenda kwa wananchi kuwahamasisha.
Tarehe 13 Machi 1940 alitamka bungeni kuwahamasisha wabunge kwa kutangaza sera yake kwa maneno haya “…to wage war by sea, land and air, with all our might and with all the strength that God can give us”. Our aim is VICTORY” (Sir Winston Leonard Spencer Churchill – House of Commons 13th March 1940).
Kutokana na hamasa ile wabunge wote walimuunga mkono, vita ikapiganwa mpaka Uingereza ikashinda 1945. Iweje viongozi wetu wa UKAWA kuamua kuondoka bungeni mahali pekee ambapo USHINDI WA KATIBA YA WANANCHI unaweza kupatikana? Badala yake wamekwenda kutafuta huruma (sympathy) ya wananchi? Ni uamuzi gani huo usiokuwa na tija?
Kwa ushauri wa kizee, nawasihi UKAWA mrejee ndani ya Bunge mkapiganie haki ya wananchi wasio na sauti. Mbona tunawaona mnapozungumza na tunasikia? Zaidi mnatakaje? Jengeni hoja, ongeeni na Mwenyekiti ili kukomesha lugha za zomea zomea na matusi, lakini na ninyi wenyewe msithubutu kuwasema marehemu, mtalaaniwa na mizimu yao. Wale hawawezi kujitetea, walitimiza wajibu wao kwa wakati ule, yale ndiyo yaliyoonekana kufaa kwa nchi hii. Ongeeni na waliohai wenzenu.
Zipo kamati za maadili, kuna kamati ya uongozi na ipo kamati ya maridhiano ambamo baadhi yenu ndiyo wajumbe, sasa mnakimbilia Zanzibar kwani kule ndiyo uchochoro wa kupitishia vilio vyenu? Au watu wa Zanzibar mmewaonaje hata muwafuate? Au ndiyo waliowatuma kwenda bungeni?
Mimi bado sielewi kwanini Zanzibar? Je, mkikataliwa mtageukia wapi? Upo usemi wa Kiingereza usemao “think before you leap.” Je, UKAWA mlifikiri kabla ya kuvuka bahari ya Hindi kuelekea Zanzibar na Pemba? Chonde chonde, watendeeni haki wananchi wanaotegemea KATIBA MPYA. Si wote tunaweza kupata fursa mlionayo ya kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Ni ninyi waheshimiwa 628 tu! Lakini kwanini Zanzibar? SINTOELEWA!