Hili ni swali linalogonga vichwa vya wananchi wengi siku hizi. Hivi karibuni kule bungeni Dodoma kulitokea kadhia kubwa iliyosababisha baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kususia vikao na kutoka nje ya bunge hili.

Hii siyo mara ya kwanza kwa wabunge wa upinzani kuondoka bungeni wakionesha kutoridhika kwao na namna mijadala inavyoendeshwa. Lakini safari hii ondoka yao bungeni imeongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), siyo Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani kama ilivyozoeleka.

Si hivyo tu, bali ondoka yao ilikuwa mara tu baada ya mjumbe wa kundi la watu 201 kuwasilisha mchango wao bungeni. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba mjumbe aliyeongoza toka ile alitoa matamshi hatarishi alipotamka kuelekeza kwa wajumbe waliobaki kikaoni eti waliwaacha hao wa “INTERAHAMWE”.

Neno ‘interahamwe’ linavyojulikana ni kikundi chochezi cha mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda. Ni hivi karibuni nchini Rwanda wamefanya kumbukumbu ya miaka 30 ya hayo mauaji (1984-2014) yaliyosababishwa na kikundi cha Interahamwe.

Uchochezi wa chuki za kimbari kule Rwanda umesababisha mauaji mengi. Visa vya misuguano ya kikabila kule vililetwa na hao Interahamwe. Sasa Bunge letu la Katiba sioni visa vinavyoweza kuitana majina kama hayo ya Interahamwe.

Bungeni kulitokea mipasho, kejeli na vijembe miongoni mwa wabunge wenye misimamo tofauti ya itikadi zao. Yapo makundi makubwa (tunavyoona kwenye runinga) mawili. Kundi la wanaotetea serikali tatu na la wanaotetea serikali mbili.

Wale wa kundi linalotetea serikali tatu wengi wao wanatoka kambi ya upinzani, hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na CUF. Wanaotetea serikali mbili wengi wao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika kuchangia mawazo kwenye kamati zilizowasilisha ripoti zao kutoka sura ya kwanza na ya sita, inaelekea hoja za serikali mbili zilionekana kutopea, hivyo wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wakaghadhibika, ndipo wakaamua kutoka ndani ya Bunge na kususia vikao.

Ghadhabu au hamaki inapozidi mtu huwa anatoa uamuzi bila kufikiri na kupima madhara yake. Hulipuka tu na kutenda jambo pengine bila hata ya kukusudia. Ndivyo nadhani kiongozi yule wa UKAWA alivyokuwa wakati ule hata akatamka neno “Interahamwe” mle Bungeni wakati anatoka.

Historia ya neno “Interahamwe” inakumbusha uchochezi, ubaguzi na mauaji ya kimbari kwa wenzetu kule Rwanda. Neno hili linaathiri sana uhusiano baina ya watu. Lina uzito wa tusi kubwa pale unapomwita mtu “Interahamwe”.

Kuwaita waheshimiwa wabunge kwamba hao “ma-Interahamwe” ni kuwatukana. Lakini pia kitendo cha mbunge kumwita mbunge mwenzake “m-Interahamwe” ni kujidhalilisha yeye mwenyewe pia.

Ubaguzi wa aina yoyote ile ni mbaya na hatari. Upo ubaguzi wa rangi (racism), ambao duniani umewagawa watu wengi na kusababisha mauaji. Huu umetokea Afrika Kusini, Marekani na hata Ulaya. Kule Ulaya, dikteta Adolf Hitler wa Ujerumani aliua Wayahudi mamilioni kwa mamilioni (mauaji yanayojulikana kama “Holocaust”.

Aidha, huyo Adolf Hitler aliwabagua sana watu weusi hata alikataa kumvisha medali Mmarekani mweusi, Jesse Owens, mwaka 1936 aliposhinda medali ya mbio za kimataifa mjini Berlin. Ni chuki kweli!

Upo ubaguzi wa dini (fanatism). Huu nao ni ubaguzi wa hatari ambapo watu wa imani tofauti wanabaguana na hata kuuana. Hali hii ipo nchini Iran kati ya Wasunni na Washia. Ubaguzi upo Misri kuwa Muslim Brotherhood; upo Afrika ya Kati pale Wakristo na Waislamu wanauana hivi sasa; upo Nigeria kwa Boko Haram na hivi karibuni dalili za aina hii ya ubaguzi zimeanza huko Visiwani kwa kundi la “Uamsho”.

Hapa Mheshimiwa Augustino Lyatonga Mrema amegusia kule bungeni wakati akichangia mawazo yake katika rasimu ya Katiba. Kwa kumnukuu alitamka: “Kinachotokea huko kinaashiria ubaya, makanisa yanachomwa, viongozi wa dini wanashambuliwa na kuuawa, hii haitaishia Magogoni bali itafika mpaka Tanzania Bara. Sasa hata Arusha mabomu yanatokea…” Hali hiyo inasababishwa na ubaguzi wa dini.

Ubaguzi mwingine upo wa hali za watu (segregation). Huu unaonekana pale watu wanapowanyanyapaa watu wengine kwa sababu hawako katika hali moja. Hali zinazoleta huo unyanyapaa au ubaguzi ni kama vile ugonjwa wa ukoma, ukimwi, kifua kikuu au ulemavu wa viungo.

Aidha, hata umaskini uliokithiri unaweza kusababisha ubaguzi wa aina hiyo miongoni mwa watu. Hapa nimeonesha tu athari za ubaguzi — uwe wa rangi, wa dini au wa ugonjwa. Athari kubwa na mbaya zaidi za huo ubaguzi ni mauaji yasiyo na sababu.

Watanzania tuepuke vishawishi vya aina yoyote vitakavyotuingiza kwenye kubaguana. Nchi hii haitakalika hata kidogo. Bungeni pasiwe mahali pa kwanza kuonesha ubaguzi miongoni mwa watunga sheria wa nchi hii.

Aprili 17, mwaka huu niliona kwenye runinga Mhe. Waziri William Lukuvi alieleza hofu aliyonayo kutokana na kile kitendo cha baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, yaani wana UKAWA kutoka ndani ya Bunge na kusingizia wazo la uchochezi na hofu nchini alilozusha yeye.

Kama ni uchochezi, basi ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kule Kibandamaiti Machi 23, mwaka huu alipomtuhumu Mhe. Rais Jakaya Kikwete eti muundo wa serikali tatu ukipita, ataelekeza jeshi lichukue nchi, jambo ambalo si kweli na ni uchochezi wa hatari kabisa!

Waziri Lukuvi akishangaa alisema kwamba huyo ni bosi wao hawawezi kumsema! “Wananirukia mimi”. Aidha, Mheshimiwa Lukuvi alimsifia Mzee Mrema kuwa ni mpinzani wa kweli tena ni kiboko yao.

Aprili 14-15, mwaka huu kulitokea maneno na chokochoko nyingi bungeni miongoni mwa wabunge wa Zanzibar. Wajumbe kadhaa walitamka ya mioyoni mwao na wakalaumiana wao kwa wao. Nakumbuka mbunge mmoja wa Unguja alielezea yale yaliyojiri pale Kibandamaiti siku ya kuhitimisha kampeni za uchaguzi mwaka 2010. Alisema kwamba kiongozi mmoja wa CUF (jina limehifadhiwa) alidiriki kusema, “Huu uchaguzi ndiyo mwisho wa utawala wa weusi.”

Mbunge yule aliendelea kusema kwamba lakini ukimtazama msemaji yule, yumo bungeni, ni mweusi kupita chungu cha kupikia! (wajumbe walicheka).

Na yupo mbunge mwingine naye wa Unguja, katika kuchangia mawazo kwenye rasimu, alisema kwamba bungeni wapo baadhi ya Wapemba kule Pemba wanadiriki kununua utaifa wa kigeni ilimradi wakubalike. Hii maana yake wanaukana Uswahili.

Ukweli ule uliwaumiza sana UKAWA ndipo wakaanza kupandwa na hamaki na hasira. Ilipofika jioni ya tarehe 15 wabunge wale wa msimamo wa serikali tatu wakajikuta hoja zinawakandamiza.

Basi akapewa fursa mmoja wa kundi la 201 kuchangia mjadala. Katika mchango wake pamoja na mawazo yake mazuri, alitamka pia kuwa sasa UKAWA wamechoshwa na matusi na kebehi bungeni. Wao kwa umoja wao wameamua kusema yametosha (enough is enough), wanaondoka bungeni (walk out) na kuwaachia hao ‘Interahamwe’! Wakabwaga manyanga – wakakimbia vita! Haooo wakajitokea nje kupanga mikakati yao ya baadaye!

Katika kikao cha April 16, mwaka huu baadhi ya wabunge walisikitishwa na kitendo cha UKAWA kutoka bungeni na kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba. Mmoja wa wachangiaji siku ile alikuwa Mhe. Augustino Lyatonga Mrema. Kama bado nakumbuka vizuri alitoa uzoefu wake katika mambo ya Serikali, hasa kuhusiana na hali ya usalama wa Taifa letu.

Ninamnukuu, “Kuna watu wanafanya mchezo wa kuigiza na kusahau kuwa waasisi wa Muungano walitaka kulinda usalama wa nchi na watu wao, ulinzi umekuwapo mpaka leo, amani, utulivu na usalama pande zote mbili… nataka mjue maadui hawapo mbali, wanarudi, tena kwa kasi, hali ya usalama wa nchi yetu si mzuri, tutizame majirani zetu Kenya, wanapakana na Somalia, mambo yanayotokea huko, tujiulize pia ni nini kinachotokea Zanzibar, hivi niwaulize wenzangu, pengine mnalo jibu, hivi UAMSHO ni mnyama gani yule?”

Lakini siyo Mheshimiwa Mrema peke yake mwenye wasiwasi wa hali ya usalama au na ule mchezo wa kuigiza wa wale waliotoka bungeni. Yupo mjumbe wa lile kundi la 201 Mhe. Askofu (mstaafu) Donald Mtetemela. Yeye Aprili 17, mwaka huu aliwakumbusha wenzake kuwa wapo bungeni si kuwaua watu.

Kauli ya Mwenyekiti wa UKAWA, Profesa Ibrahim Lipumba, (kuwaita Interahamwe) inaweza kuleta hatari na kuamsha machungu ya Wanyarwanda na inaweza kuleta utata kati ya Tanzania na Rwanda. Hivyo, basi alitaka kauli ile ikemewe.

Si hivyo tu, lakini Baba Askofu alionesha kukerwa na kitendo au tabia iliyojitokeza katika Bunge lile ya kutukana waasisi wa Taifa hili. Akauliza ule utamaduni wetu (Watanzania, hasa Waafrika) wa kuheshimu viongozi umekwenda wapi?

Alishangazwa kuona watu wanathubutu na kudiriki kutukana viongozi ambao sasa ni marehemu. Basi akatoa angalizo kuwa ukiona mtu anagombana na marehemu au anamkashifu na kumkosoa marehemu, basi pana maswali mengi ya kujiuliza – kuhusu maadili ya mtu huyo! Marehemu wanahukumiwa na Mungu tu.

Mimi kwa mtazamo na fikra zangu naona upo mmomonyoko mkubwa wa maadili katika Taifa letu. Tendo la kususa vikao na tabia ya kuwasema marehemu siyo tabia asilia za Waafrika kusini mwa Jangwa la Sahara. Ni tabia ngeni zimeigwa kutoka mataifa ya Ulaya.

Aidha, kwa wasomi wa uchumi wanajua wazi kuwa kurefusha vikao au kuendeleza vikao ni kuumiza uchumi wa nchi, kwa Kiingereza tunasema “economic sabotage au strangulation of the economy” kusikia mtaalam wa masuala ya uchumi ndiye anaongoza kuunyonga uchumi wa Taifa hili!

Zipo njia kadhaa kule bungeni za kumaliza hizo tofauti zinazojitokeza. Hasa hasa nimepigwa na butwaa kusikia UKAWA wameamua kwenda Zanzibar kuwaeleza wananchi wa kule nini kilichojiri ndani ya Bunge. Kwanini kwanza wasiwaeleze wananchi wa pale Dodoma lilipo Bunge? Au kwanini wasiwaeleze kwanza wananchi wa Dar es Salaam au Mwanza au Arusha kwenye wapigakura wao wengi? Kwanini Zanzibar? Hapo sielewi kabisa mantiki ya kuchagua Zanzibar.

Mshangao wangu mwingine ni kule kugeuka ghafla kwa Chadema kukubali kushikamana na CUF. Sote tunajua kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, Kambi ya Upinzani Bungeni inaongozwa na Chadema. Ingawa kabla ya uchaguzi kambi ya upinzani iliongozwa na CUF na walitoa nafasi za uongozi wa uwaziri kivuli kwa Chadema.

Safari hii hao hao Chadema waliwanyima ushirikiano kiuongozi, uwaziri kivuli watu wa CUF ati hawakuwahitaji, wanajitosheleza. Leo hii Chadema wamekuwa mstari wa mbele kuomba waungane na CUF katika UKAWA na waende pamoja Zanzibar. Wenzangu, hapo inaingia akilini kweli kuona ushirikiano wa aina hii?

Waingereza wanaita muungano wa aina hii kuwa ni muungano wa kujinufaisha binafsi “marriage for Convenience’s sake”, na kibiolojia huitwa “symbiotic life”. Hapa ni dhahiri CUF na Chadema wameungana ili kujinufaisha tu, hawakuungana ili kunufaisha Taifa wala kwa msukumo wa itikadi za vyama vyao. Maana inajulikana wazi kuna tofauti sana kati ya itikadi na sera za vyama hivyo.

Mbunge wa Zanzibar alitamka wazi wazi katika Bunge Maalum la Katiba kuwa Chadema hampati kura ng’o kule Visiwani. Kule tunajuana kuna CCM na CUF basi. Sasa sielewi Chadema wamesukumwaje kumsindikiza Mwenyekiti wa UKAWA anapokwenda kutoa ripoti yake kwa bosi kule Zanzibar.

Mbona kihistoria inajulikana tangu enzi za Sultani wa kwanza kule Visiwani aliyeitwa Seyyid Said (1840-1856) kuwa huyo Sultani alidai kuwa “filimbi au zumari ikipigwa Unguja, watu wa Kigoma na Unyanyembe wanacheza” (soma MAPAMBANO YA UKOMBOZI ZANZIBAR – TPH uk. 23). Si mnaona?

Mwenyekiti wa CUF akifuatana na wenzake kutoka Chadema na NCCR-Mageuzi wanaamua kwenda Unguja kufanya mkutano Kibandamaiti, mgeni rasmi ni Katibu Mkuu wa CUF? Mmiliki wa CUF. Huko ni kucheza kwa mlio wa zumari kutoka Zanzibar. Hawaendi kuelezea yaliyojiri bungeni, bali wanakwenda kupiga ripoti kwa bosi. Hii ni nini sasa? Tamaa ya kutawala inawasukuma UKAWA kuunganisha vyama vya upinzani ilimradi washike dola.

Jambo jingine nisilolielewa mimi ni namna Chadema wanavyokuwa na imani kuwa wananchi wanawasikiliza sana. Ndipo wanapata moyo wa kusema daima, “tutaandamana, tutakwenda kwa wananchi katika mikutano ya hadhara tutawaeleza kile kilichojiri bungeni.”

Kwani pale walipotumia chopa tatu kufanya mikutano ya hadhara katika kata 27 kugombea udiwani wananchi si waliwajibu kwa kupata kata tatu tu kati ya hizo 27? Au hivi karibuni walipotumia nguvu yao kubwa katika kuomba Jimbo la Kalenga, hata Chopa ilitumika, mbona wametoka kapa na kiti kikaenda kwa CCM kwa kishindo? Hivyo vyote si vinaashiria kutokubalika kwao? Kwanini hawasomi ishara za nyakari na wakatambua mbinu hiyo ya mikutano ya hadhara na wananchi haina tija?

Njia pekee na ya hekima na busara kwa UKAWA ilikuwa kuzungumza tatizo lililojitokeza bungeni na Mwenyekiti ili kamati ya maridhiano au ya uongozi au ile ya maadili ya Bunge ilitafutie ufumbuzi kuondoa mipasho na kejeli ndani ya Bunge.

Kinachohitajika hapa ni akili za kawaida tu yaani “common sense” wala siyo huruma (sumpathy) ya Wazanzibari. Haiji akilini kwa viongozi wa Tanganyika kupanda boti kwenda Unguja kutafuta huruma kutoka kwa Mwarabu. Hili linatukumbusha enzi za Sultani wa kwanza wa Zanzibar, Seyyid Said (1840-1856), alipojigamba kuwa “filimbi (zumari) ikipigwa Unguja, watu wa Kigoma wanacheza” ndiyo tunaiona leo CUF Zanzibar, lakini Wabara kwa hiari yao wanacheza na wanakwenda kutoa ripiti ya yaliyojiri bungeni mjini Dodoma! Je, huko siyo kujishusha (be subjective to Zanzibar) sisi Wabara?

Iliaminika kule Visiwani siku hizo kuwa wenye nchi walikuwa Waarabu na watu weusi walionekana kuwa wageni tu wa kutoka Bara. Ninayakariri haya kwa kuwa historia ina tabia ya kujirudia matukio yake. Huko nyuma gazeti la Arab Association lililoitwa “ALFALAQ” lilipata kuandika haya: “Wanachama wengi wa African Association ni wageni.” Wakati huo huo, gazeti la Waafrika wa Zanzibar “AFRIKA KWETU” lilipinga maoni hayo ya Waarabu liliposema “Sisi watu weusi wa Unguja na Pemba tumeshtushwa kujua kwamba wahamiaji wachache wana njozi za ajabu na potofu kwamba Visiwa vya Unguja na Pemba siyo nchi halali za Waafrika bali kwa bahati mbaya Waafrika wamejikuta katika visiwa hivi.

Mtu yeyote mwenye njozi kama hizi lazima afahamu kwamba anajidanganya”. (SOMA MAPAMBANO YA UKOMBOZI – ZANZIBAR – TPH uk. 63).

Kutokana na mawazo pinzani ya aina hiyo, hata Wazungu walikuwa wanawaona Waafrika wa Zanzibar kama watu wa hali ya chini ya Waarabu na Wahindi. Basi Mzungu mkoloni alionesha hali hiyo kwa kuandika hivi, ninamnukuu: “Waafrika kule Zanzibar walikuwa kama watoto ambao wana hulka za Waarabu ambao wamewafunza.”

Akaendelea: “Mwarabu kule Zanzibar anapewa heshima sana na Mwafrika” (soma MAPAMBANO YA UKOMBOZI ZANZIBAR – TPH uk. 28 na 29 foot notes).

Kwa mtazamo wa aina hii, hata Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitolea mifano ya unyonge wa Mwafrika kule Visiwani kwa mifano kadhaa.

“Juzi juzi tu wakati wa Vita Kuu ya II watu wa Zanzibar walidiriki kubadili majina yao ya asili yasifanane na Uafrika. Tunao mpaka sasa wanaobadili majina; Athmani anajiita Othman, Bakari anajiita Abubakar, Mgomi anajiita El-Mughumi, aukwepe Uafrika. Ukiwa Mwarabu kule Visiwani wakati ule wa vita unaweza kupata mchele. Lakini Mswahili hivi hivi hupati mchele (unapata dona/maharagwe au kauzu).

“Sasa ukiweza kuukwepa Uafrika ukajifanya Mwarabu utapata mchele. Na huku pwani sifa ya Mwarabu ni lugha, maana mama wa Kiswahili akikushukuru husema asante Mwarabu wangu, ndiyo anakusifu hivyo mama wa Kiswahili.” (Nyerere: Ujamaa ni Imani uk. 10). Hotuba aliyotoa kwa vijana Diamond Jubilee Jumamosi tarehe 30 Mei 1969, hapa imeonesha unyonge wa mtu mweusi, hasa kule Visiwani.

Sasa unaposikia viongozi wa UKAWA wote weusi wanakwenda Zanzibar kule watu weusi walikokandamizwa kwa miaka 50 iliyopita, unajiuliza vipi Wanatanganyika kwenda Visiwani kumwona nani? Ili iweje? Huu ni msukumo wa itikadi au ni katika kutafuta ulaji zaidi?

Bado inashangaza. Tangu lini CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi wakala sahani moja? Wakawa wamoja? Mbona itikadi zao zinatofautiana sana?

Vita yoyote inapiganiwa katika viwanja vya mapambano. Hapa pana VITA ya KATIBA. Na vita hii uwanja wake wa mapambano ni ndani ya Bunge Maalum la Katiba. Mimi ninavyomfahamu Profesa Lipumba kama askari katika Kambi ya JKT Ruvu miaka ile ya 1973 alikuwa mvumilivu sana, hodari katika kazi. Ile mikikimikiki yote ya ulikruti aliimudu bila ya kupata adhabu kwa utovu wa nidhamu au uzembe (malingering). Nikimwita mlugaluga wa Kinyamwezi ni mpiganaji.

Niliposikia uvumilivu wa vineno vya hovyo hovyo mle ndani ya Bunge vimemshinda sikuamini. Ile “endurance” yake yote imeyeyukia wapi askari huyu hata akimbie mapambano ya maneno? Kwanini alikata tamaa upesi vile? Ule moyo wake wa kupambana mpaka kushinda (his fighting spirit for a just cause) umekwenda wapi?

Labda niwakumbushe wana UKAWA kwamba kukata tamaa na kukimbia kutoka uwanja wa mapambano ni dalili ya kushindwa (despair is for the defeated). Ni kweli Profesa Mwenyekiti wa UKAWA na wenyeviti wa Chadema na NCCR-Mageuzi mko tayari kuwasaliti wanachama wenu kwa kukimbia kutoka uwanja wa mapambano, yaani Bunge Maalum la Katiba? SIAMINI na wala SINTOELEWA.

Wakati wa Vita Kuu ya II Uingereza, alitokea kiongozi shupavu wa Waingereza akiitwa Winston Churchill. Huyu alipiganisha vita katika Bunge la Uingereza. (House of Commons – Parliament), hakwenda kwa wananchi kuwahamasisha.

Tarehe 13 Machi 1940 alitamka bungeni kuwahamasisha wabunge kwa kutangaza sera yake kwa maneno haya “…to wage war by sea, land and air, with all our might and with all the strength that God can give us”. Our aim is VICTORY” (Sir Winston Leonard Spencer Churchill – House of Commons 13th March 1940).

Kutokana na hamasa ile wabunge wote walimuunga mkono, vita ikapiganwa mpaka Uingereza ikashinda 1945. Iweje viongozi wetu wa UKAWA kuamua kuondoka bungeni mahali pekee ambapo USHINDI WA KATIBA YA WANANCHI unaweza kupatikana? Badala yake wamekwenda kutafuta huruma (sympathy) ya wananchi? Ni uamuzi gani huo usiokuwa na tija?

Kwa ushauri wa kizee, nawasihi UKAWA mrejee ndani ya Bunge mkapiganie haki ya wananchi wasio na sauti. Mbona tunawaona mnapozungumza na tunasikia? Zaidi mnatakaje? Jengeni hoja, ongeeni na Mwenyekiti ili kukomesha lugha za zomea zomea na matusi, lakini na ninyi wenyewe msithubutu kuwasema marehemu, mtalaaniwa na mizimu yao. Wale hawawezi kujitetea, walitimiza wajibu wao kwa wakati ule, yale ndiyo yaliyoonekana kufaa kwa nchi hii. Ongeeni na waliohai wenzenu.

Zipo kamati za maadili, kuna kamati ya uongozi na ipo kamati ya maridhiano ambamo baadhi yenu ndiyo wajumbe, sasa mnakimbilia Zanzibar kwani kule ndiyo uchochoro wa kupitishia vilio vyenu? Au watu wa Zanzibar mmewaonaje hata muwafuate? Au ndiyo waliowatuma kwenda bungeni?

Mimi bado sielewi kwanini Zanzibar? Je, mkikataliwa mtageukia wapi? Upo usemi wa Kiingereza usemao “think before you leap.” Je, UKAWA mlifikiri kabla ya kuvuka bahari ya Hindi kuelekea Zanzibar na Pemba? Chonde chonde, watendeeni haki wananchi wanaotegemea KATIBA MPYA. Si wote tunaweza kupata fursa mlionayo ya kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Ni ninyi waheshimiwa 628 tu! Lakini kwanini Zanzibar? SINTOELEWA!