Habari za hivi majuzi zinasema suala la Burundi litajadiliwa na Kamati Maalum ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) linaloshughulikia utatuzi wa migogoro. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdullah Mwinyi amesema ujumbe wa Rais Pierre Nkurunziza umekubali kuhudhuria mkutano huo utakaofanyika mjini Arusha wiki hii.

Kamati hiyo pia itatoa fursa kwa raia na asasi za kiraia kutoa maoni yao kuhusu mgogoro wa Burundi ambao umepelekea mamia ya watu kupoteza maisha yao. Moja ya asasi iliyosambaza risala yake ni Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika (PALU) ambao wamependekeza kuwa Nkurunziza asiruhusiwe kushika uwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mpaka akubali kushiriki mikutano ya usuluhishi.

Kwa mujibu wa Katiba ya EAC uwenyekiti unatakiwa ushikwe na Nkurunziza baada ya Rais Magufuli kumaliza muda wake. Wengine wamediriki hata kusema kuwa Burundi ifukuzwe kutoka EAC.

Wakati Kamati ya EALA inapanga mkutano wa usuluhishi, tarehe 6 mwezi huu mawaziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Uganda, na Angola walihitimisha kikao cha faragha kuhusu Burundi uliofanyika mjini Arusha. Hii ni baada ya mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika Arusha kuahirishwa kwa vile ujumbe wa Nkurunziza ulikataa kuhudhuria wakisema hawatakaa meza moja na wale “wanaochochea vugugu nchini Burundi”.

Wakati huo huo Rais Yoweri Museveni wa Ugana ameteuliwa na marais wenzake wa EAC kuwa msuluhishi katika mgogoro wa Burundi. Yeye aliahidi kung’atuka baada ya mihula miwili, lakini sasa anaendelea na mhula wa tano akiwa ametawala nchi kwa muda wa miaka 30.

Sasa anatarajia kugombea urais mwezi ujao baada ya kubadili katiba iliyoweka ukomo. Alifanya mabadiliko hayo mnamo 2005 na tangu wakati huo amekuwa akisema “shamba ambalo nimelisafisha, kulipalilia na kulilima mwenywe sasa iweje niwaachie wengine walivune?” Kwa maneno mengine nchi imegeuzwa shamba lake.

Hata hivyo, EAC imemteua kuwa msuluhishi wa Burundi, jambo ambalo limekubaliwa na AU,  UN na wafadhili.

Kwa muda huu Rais Magufuli ni Mwenyekiti wa EAC na ndio maana huwa anamtuma waziri wake wa mambo ya nje, Augustine Mahiga kushughulikia mgogoro wa Burundi. Mpaka sasa hajasafiri nje ya nchi na haieleweki iwapo atahudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) unaotarajiwa kufanyika mjini Addis Ababa kuzungumzia mgogoro wa Burundi.

Tanzania ina nafasi nzuri kwa vile Burundi imekuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania. Wengi tutakumbuka wakati ule marais wa EAC walipokuwa wakikutana Tanzania na Burundi zilitengwa kwa sababu ilionekana sisi hatukuwa tayari kujiunga na miradi ya EAC. Wenzetu walijihesabu kama nchi zilizokuwa na utashi (Coalition of the Willing – CoW).

Mgogoro wa Burundi ulianza rasmi wakati Mahakama ya Katiba ilipoamua kuwa Nkurunziza alikuwa na haki ya kugombea urais kwa muhula wa tatu, ingawa katiba iliyosainiwa na pande zote mjini Arusha iliweka kikomo cha mihula miwili. Ni kwa sabau muhula wa kwanza Nkurunziza alikuwa amechaguliwa na wabunge na sio kwa kura za wananchi. Hivyo muhula huo haukupaswa kuhesabiwa, ilisema mahakama.

 Katika jopo la majaji watano mmoja alitofautiana nao kwa kusema kuwa hao wabunge waliwawakilisha wananchi kwa hiyo awamu ya kwanza ilipata ridhaa ya wananchi.  Huyo jaji alilazimika kukimbia nchi, baada ya kudai kuwa majaji wenzake walikuwa wamelazimishwa kumuunga mkono Nkurunziza. 

Wapinzani wakadai kuwa hata hiyo Mahakama ya Katiba haiwezi kuwa huru kwa sababu majaji wake wameteuliwa na Nkurunziza.  Kuna wanaosema kuwa hoja hii haina mashiko, kwani hata katika nchi za magharibi kama Ufaransa majaji wa Mahakama ya Katiba huteuliwa na Rais.  Hata Rais Barack Obama anateua majaji wa mahakama ya juu.

Hivyo, baada ya Mahakama ya Katiba kumruhusu, Nkurunziza aligombea urais mwezi Julai 2015 na akachaguliwa kuongoza muhula wa tatu kwa kupata asilimia 70 ya kura. Uchaguzi huo ulisusiwa na wapinzani. Marekani na EU wakakataa kutuma waangalizi wa uchaguzi.

Wakati Nkurunziza analaumiwa kwa kugombea urais muhula wa tatu, hatusikii lawama kutoka nchi za magharibi zikielekezwa kwa marais wa Rwanda, Uganda na DRC (Congo) ambao pia wameongeza mihula yao.  Kagame na Kabila nao, sawa na Nkurunziza, waliteuliwa kushika muhula wa kwanza na kwa hiyo wanadai hauhesabiki.

Kagame aliteuliwa kuwa Rais mwaka 2000, kisha akachaguliwa kwa kishindo mwaka 2003 na 2010. Sasa awamu yake ijayo itakuwa ya nne lakini yeye anasema ni ya tatu. Pia anakusudia kuondoa kikomo aendelee kuchaguliwa bila kikomo. Kama ni kosa kwa Nkurunziza kwanini isiwe kosa kwa Kagame na wengine?

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) lilipiga kura tarehe 12 Novemba mwaka jana na kupitisha azimio likilaani  kile lilichokiita “mauaji, utesaji na ukandamizaji wa haki za binadamu” nchini Burundi. Ufaransa ndio ilitayarisha muswada wa azimio hilo na kuzihimiza nchi 15 wanachama wa Baraza hilo kuunga mkono. Hapa inabidi tujiulize iweje azimio kuhusu nchi ya Kiafrika lipigiwe debe na nchi ya Ulaya badala ya Waafrika wenyewe?

Hata hivyo, nchi za Kiafrika zikisaidiwa na Urusi zilipinga kipengele kinachotaka Burundi iwekewe vikwazo. Mwishowe azimio likapitishwa bila ya kipengele cha vikwazo. Sasa baada ya kupitishwa kwa azimio hilo ikatangazwa kuwa UN itafanya mipango ya kuhamisha baadhi ya askari wake kutoka DRC (Monusco) hadi Burundi .

Wazo mbadala likatolewa kuwa badala ya UN kutuma majeshi yake ni vizuri Umoja wa Afrika (AU) ukafanya kazi hiyo. Ikapendekezwa kuwa majeshi ya Monusco yanaweza yakaunganishwa na majeshi ya AU. Rais Obama wa Marekani akampigia simu Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na wakazungumzia hali ya Burundi.

AU ina sera ya kuwa na vikosi kila kanda barani Afrika. Hivyo, kwa upande wa Afrika Mashariki kuna kile kinachoitwa kikosi cha akiba  cha Afrika Mashariki (East African Standby Force). Ni kikosi hiki ndicho kinachofikiriwa kupelekwa Burundi.  

Uamuzi wa kupeleka wanajeshi 5,000 huko Burundi ulichukuliwa Disemba, 2015 na Baraza la Amani na Usalama la AU.  Nkurunziza alipewa muda wa kukubaliana na uamuzi huu, lakini akaupinga na kusema majeshi yake yatapambana na “kikosi cha uvamizi” cha AU.

Aghlabu tunapozungumzia majeshi ya UN au ya AU, kisichotajwa ni kuwa majeshi hayo huwa yanafadhiliwa na mataifa makubwa kama Marekani. Bendera ni ya UN au AU na askari ni Waafrika, lakini Marekani na Ulaya wanatoa kila kitu kuanzia silaha hadi sare na posho. 

Wakati AU imechachamaa kupeleka majeshi ya kulinda amani kuzuia mauaji nchini Burundi, wachunguzi wanahoji iweje AU hiyo hiyo ilikaa kimya wakati majeshi ya Ufaransa yalipoishambulia Ivory Coast mwaka 2010. Halafu kuna uvamizi wa Libya (2011), Mali (2012) na CAR (2013) uliofanywa na majeshi ya kigeni. Je, yalikuwa wapi hayo majeshi ya AU ya kulinda amani? 

Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza katika Jumuiya ya EAC kuunga mkono upelekwaji wa majeshi ya kulinda amani nchini Burundi (MAPROBU). Ingawa Nkurunzinza amesema hii itakuwa ni sawa na uvamizi wa nchi yake na majeshi ya kigeni, Waziri Mahiga awali alikuwa amesema lengo lingekuwa ni kuwalinda raia na wala si kupambana na jeshi la nchi au na serikali yake. 

Suala hili lilizungumzwa na Mahiga alipokutana na Mwenyekiti wa AU, Bi Nkosazana Dlamini-Zuma mjini Durban na mjini Addis Ababa. Baadae likatolewa tamko rasmi likimuomba Nkurunzinza kushirikiana na MAPROBU.

Mpaka sasa haieleweki ni nchi zipi zitatoa majeshi yake kuchangia hii Maprobu. Burundi yenyewe imetuma majeshi yake kulinda ‘amani’ huko Somalia na DRCongo. Sasa nayo inatakiwa ilindwe amani yake.

Ni vizuri tukajiuliza, kwanini mataifa makubwa yanachangamkia sana utumiaji wa majeshi ya usalama nchini Burundi?

Suali hili linagusiwa na Charles Kambanda,  mwanasheria kutoka Rwanda anayeishi Marekani. Aliwahi kuwa profesa katika Chuo Kikuu cha Rwanda. Hivi karibuni akihojiwa na idhaa ya redio KPFA, alisema mgogoro wa Burundi ni wa kisiasa na kiini chake ni maliasili ya nchi hiyo inayogombaniwa na mataifa makuu ulimwenguni.

Kambanda amesema nchi za kibeberu zimenuia kuudhoofisha utawala wa Burundi ziweze kuudhibiti. Kwa njia hii nchi hizi zitakuwa na nafasi ya kunyonya utajiri na maliasili za Burundi.

Anasema kinachofanyika nchini Burundi si tofauti na DRC, kwa vile kuna kampuni za kimataifa zinazogombania maliasili katika maeneo haya. Mbinu wanazotumia ni kutengeneza mazingira kurahisisha uporaji wa maliasili unaofanywa na kampuni za kimataifa kupitia madalali wao wa kienyeji.

Hii ndio hali ilivyo katika maeneo ya DRC mashariki ambayo inapakana na Burundi. Na Burundi nayo inazalisha asilimia sita ya madini ya nikeli (nickel) duniani. Tayari kampuni za kigeni zimewarubuni baadhi ya viongozi wa upinzani ambao ndio watakaokuwa madalali.

Kambanda anasema hii ndio sababu ya kimsingi inayozifanya nchi za Marekani na Ulaya kuhimiza na kuwezesha kile wanachokiita “kikosi cha kulinda amani” huko Burundi. Wamefaulu kuuza wazo hilo kwa AU ingawa EAC na SADC haziko tayari kuunga mkono. Badala yake zinataka yafanyike mazungumzo kufikia maridhiano.

Naye mwandishi, Gearóid Ó Colmáin anasema Marekani na wenzake wa Ulaya wana mkakati wa kuidhibiti Burundi kwa kumuondoa Nkurunziza na kuuweka utawala utakaolinda maslahi yao. Hivi ndivyo ubeberu umekuwa ukifanya katika nchi nyingi za Afrika, Asia, Amerika Kusini na Mashariki ya Kati.

 Anasema mkakati huu umekuwa ukiendeshwa kupitia vyombo vya habari tangu 2005. Lengo lao ni kuchora upya mipaka ya nchi za maziwa makuu kama wanavyofanya katika nchi za Kiarabu. Katika nchi hizo mataifa ya kibeberu yalichora upya mipaka ya nchi na kuwatawaza wafalme vibaraka chini ya kile kinachoitwa makubaliano ya Simon-Picot. Hii ilifanyika baada ya vita kuu ya kwanza na ingali inaendelea hadi leo.

Si ajabu, kwani hivi karibuni ilitangazwa kuwa mjumbe wa serikali ya Marekani anayeshughulikia kanda ya maziwa makuu anatembelea Burundi, kisha atafika Dar es Salaam, Rwanda, DRC na Addis Ababa. Akiwa mjini Addis atahudhuria mkutano wa kilele wa AU pamoja na wajumbe wenzake kutoka Marekani. Wanachokitafuta ni nini?