Walioshitakiwa walikuwa 13, SP Christopher Bageni, ACP Abdallah Zombe, ASP Ahmed Makele, PC Noel Leornard, WP 4593 Jane Andrew, CPL Nyangerela Moris, PC Michael Shonza, CPL Abeneth Saro, DC Rashid Mahmoud Lema, CPL Emmanuel Mabura, CPL Felix Sandys Cedrick, CPL Rajab Hamis Bakari na CPL Festus Philipo Gwabisabi.
Kwanini wameshitakiwa watu wote hawa halafu mtu mmoja ndiye aliyepatikana na hatia na akahukumiwa kunyongwa? Tutaona hapa.
Kwa kumbukumbu, kesi hii ilianzia Mahakama Kuu ya Tanzania mbele ya Jaji Massati JK. Wakati upande wa mashitaka ukifunga kesi yao mahakama ikawaondoa watuhumiwa watatu PC Noel Leornard, CPL Nyangerela Moris na CPL Felix Sandys Cedrick kwa kuwaona hawana kesi ya kujibu, hivyo ikaona hakuna haja ya kuwataka kujitetea na kuendelea kuwa katika kesi.
Kwa hiyo wakabaki 10 ambao sasa walikutwa na kesi ya kujibu, hivyo kesi ikaendelea na hao 10 akiwamo Bageni. Wakati wameanza kujitetea, mmoja wao hao 10, DC Rashid Mahmoud Lema alifariki dunia, hivyo kesi yake ikaishia hapo na sasa idadi ikabaki tisa.
Mwisho wa kesi hapo Mahakama Kuu, Jaji Massati aliwaachilia huru watuhumiwa wote tisa waliokuwa wamebaki kwa kuwaona hawana hatia. Moja ya hoja kubwa ya kuachiliwa kwao huru ilikuwa kwamba kati ya wote hao tisa waliobaki katika kesi hiyo hakuna hata mmoja kati yao aliyefyatua risasi na kuua.
Ikumbukwe aliyefyatua risasi na kuua ni CPL Saad ambaye hakuwahi kufikishwa mahakamani baada ya kutoroka mapema ‘liliposanuka’. Kwa hiyo Mahakama Kuu iliona kutokuwepo kwa CPL Saad ili atiwe hatiani kwa kuua au amtaje mtu mwingine aliyempa amri ya kuua ili wote wahukumiwe kwa kosa moja, iliona ni udhaifu ambao unatosha kuwaachilia watuhumiwa wote tisa, na iliwaachilia wote huru. Kwa ufupi iliona hakuna kinachowaunganisha na mauaji zaidi ya tu kuwa walikuwa kwenye tukio.
Serikali/Jamhuri haikuridhishwa na uamuzi huo, hivyo ikakata rufaa Mahakama ya Rufaa ikipinga hukumu hiyo dhidi ya watuhumiwa wote tisa walioachiliwa. Rufaa ikasajiliwa kwa namba 358/2013. Rufaa ilipangwa kwa majaji watatu; Jaji Luanda, Jaji Mjasiri na Jaji Kaijage.
Wakati rufaa inapangwa kusikilizwa, serikali/Jamhuri ikawafutia rufaa watuhumiwa watano; WP 4593 Jane Andrew, CPL Emmanuel Mabura, PC Michael Shonza, CPL Abeneth Saro na CPL Festus Philipo Gwabisabi. Kwa hiyo kwenye idadi ya wale tisa wakabaki wanne; ACP Abdallah Zombe, SP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makele na CPL Rajab Hamis Bakari. Hivyo rufaa ya Mahakama ya Rufaa ikaendelea na hawa wanne.
Rufaa ilisikilizwa na mwisho mahakama ikawaondoa watatu; ACP Abdallah Zombe, ASP Ahmed Makele na CPL Rajab Hamis Bakari kuwa hawana hatia na ikawaachilia huru, ikabaki na mmoja SP Christopher Bageni ambaye ilimkuta na hatia na ikaamuru kunyongwa kwake hadi kufa. Kumbuka Mahakama Kuu ilimwachilia huru. Ni Mahakama ya Rufaa iliyobadilisha uamuzi huu kutoka kuachiliwa huru hadi kunyongwa.
Kwanini Bageni anyongwe?
Kumbuka Mahakama Kuu ilimuachilia Bageni kwa sababu kuu mbili. Kwanza, siye aliyefyatua risasi; pili, yule aliyefyatua risasi CPL Saad hakufika mahakamani kumtaja Bageni kuwa ndiye aliyemuamrisha kupiga risasi ili wote wawe na hatia sawa.
Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Kifungu cha 22 cha Kanuni za Adhabu aliyetenda kosa kama vile CPL Saad alivyopiga risasi, na aliyeamrisha (saidia) kutendwa kosa, wote hatia yao ni moja. Kama ni kunyongwa ni wote na kama ni kifungo ni wote.
Kwa msingi huu, Mahakama Kuu haikumuona Bageni akifyatua risasi kwa sababu si yeye aliyefyatua risasi, hivyo upande huo akaondolewa, lakini pia haikumuona akiamrisha risasi kufyatuliwa, kwa sababu aliyefyatua hakuwapo mahakamani kumtaja kuwa ndiye aliyemwamrisha kufyatua, hivyo upande huo pia nako akaondolewa. Mwisho akaonekana haingii popote kwenye kosa, basi akaachiliwa huru.