Uungwana ni vitendo na uungwana huo huthibitika pale ukweli halisi unaposemwa bayana badala ya kukwepakwepa na kutafuta visingizio.
Katika misimu mitatu mfululizo, mwenendo wa Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club ya Dar es Salaam katika Ligi Kuu umekuwa si mzuri. Jambo hilo limesababisha timu hiyo kutoshiriki michuano ya kimataifa na kuwafanya wenzao Yanga kuwakejeli kwa kuwaita timu ya mchangani huku mashabiki wake wakiwa wanyonge na kukosa la kujibu.
Wekundu hao wa Msimbazi ambao kwa sasa wapo chini ya kocha Dylan Kerr, Mwingereza, imekuwa katika kipindi cha shinikizo kubwa la kufufua matumaini ya kurudia enzi zake za kushiriki michuano ya kimataifa. Pamoja na hayo, ni vyema pia kuangalia na aina ya nguvu inayowekwa na timu hiyo katika kufikia matarajio hayo.
Nasema ihojiwe nguvu inayowekwa na timu hiyo katika kufikia matarajio waliyo nayo ili kuepusha lawama zisizo za msingi kwa kocha, maana tayari ‘figisufigisu’ zimeanza ndani ya Msimbazi. Matokeo katika jambo lolote hutegemea nini umewekeza. Uwekezaji wa Simba katika usajili wa kuwafikisha wanapotaka ni hafifu sana ukilinganishwa na wa Yanga na Azam.
Mpira siyo suala la jina au historia bali ni suala la uwekezaji na ndiyo maana Yanga na Azam zinazopishana kileleni mwa msimamo wa Ligi zimefanya usajili wa maana pamoja na kuwa walikuwa na vikosi imara kabla hata ya usajili huo. Timu yenye mabeki kama Serge Pascal Wawa na Aggey Morris au mabeki kama Kelvin Yondani na Nadir Haroub Cannavaro na bado ikaingia sokoni kutafuta beki mwingine wa kimataifa, lazima timu kama Simba ijiulize mara mbili mbili kuwa inawezaje kupambana na timu kama hizo.
Uwiano wa wachezaji wa Simba na wale wa washindani wao katika Ligi ni tofauti sana na ndiyo maana ni makosa makubwa sana kuanza kumshushia lawama kocha. Kocha ni mtaalamu lakini ili mtaalamu afanye kazi yake vizuri, ni lazima apate vifaa ambavyo vitaendana na mahitaji ya kazi yake – tena kwa viwango vya ushindani. Ukweli huu ni kama Simba wanaukwepa na kutaka kumuona kama kocha ndiye anayewanyima mafanikio wanayoyahitaji (kushika nafasi ya kwanza au ya pili).
Simba wamekuwa na usajili wa kusuasua kwa misimu kadhaa sasa kutokana na ukata unaoikabili klabu hiyo kutokana na sababu mbalimbali. Unapofika wakati wa usajili Simba imekuwa ni timu inayotafuta wachezaji wa bei chee na siyo wachezaji wa ushindani. Simba wakitaka kusajili mchezaji kisha Azam au Yanga ‘wakitia mguu’ hapo wao wananywea halafu leo wanatarajia kushindana na timu hizi katika matokeo ya uwanjani, jambo ambalo haliwezekani.
Klabu kama imeshindwa kufanya usajili wa ushindani isitarajie kuleta ushindani katika Ligi ila inahitaji utulivu na kujipanga taratibu bila presha ya kushindana na wale waliofanya usajili wa gharama. Sisemi wasitafute mafanikio makubwa ila wasipeane shutuma au kujengeana hoja za uzembe pale wanaposhindwa kupambana vilivyo na wale waliotumia gharama kubwa katika usajili.
Soka ni uwekezaji kama ulivyo uwekezaji mwingine wowote na hivyo kanuni za uwekezaji lazima zizingatiwe. Ninachoelewa kama mwekezaji ana mtaji mkubwa wa pesa anaweza kuwekeza kwa kutumia pesa kwa viwango vya kutosha na kuanza kusubiri faida lakini mwekezaji mwenye mtaji mdogo atahitaji kuwekeza pesa zake na muda wa kusubiri kwa muda fulani ili uwekezaji wake ukomae na aweze kuvuna faida.
Kwa hiyo, mwekezaji mwenye mtaji mdogo anahitaji muda pia mbali na pesa aliyowekeza katika uwekezaji husika mfano mtu ambaye hana pesa za kuwekeza kwa kununua uwanja mjini Kariakoo atalazimika kwenda kununua uwanja huko Mabwepande kwenye mji tarajali na hapo itabidi asubiri mpaka huko Mabwepande kuwe mji ndipo aanze kuvuna faida ya uwekezaji wake.
Simba kwa miaka kadhaa wamekuwa wakisajili chipukizi na wachezaji wakubwa kadhaa kutokana na hali ya kichumi inayowakabili. Uamuzi huo hauna ubaya wowote kama wangekubali na kuheshimu aina yao ya uwekezaji kwa kukubali kuwekeza na muda kwa maana ya kuwapa muda wachezaji hao na kocha aliyepewa timu hiyo kuinoa.
Simba hawataki kusubiri ilhali uwekezaji wao ni wa kipato kidogo na wanatamani washindane na wale waliofanya uwekezaji mkubwa. Jambo hilo ndilo linalosababisha wao kuwatimua makocha mara kwa mara kwa kuwa hawaleti matokeo kama ya Azam na Yanga. Ukiangalia uwiano wa bajeti ya usajili kati ya Simba na washindani wao wa Ligi (Azam na Yanga) utagundua kuwa Simba hawahitaji kumlaumu kocha yeyote kwa hilo.
Kwa mazingira kama haya unaposikia minong’ono eti Simba wanataka kumtimua kocha Kerr lazima ushangae kama kweli Simba wanatambua hali yao kiuchumi au wanaangalia ukongwe wao kana kwamba ukongwe ndiyo unacheza mpira. Kelele za kumuondoa Kerr zilianza baada ya kipigo walichopata kutoka kwa Prisons ya Mbeya na kelele hizo zikazimwa kupitia kipigo cha mabao 6 walichoishushia Majimaji ya Songea.
Baada ya hapo kelele zimerudi kwa mtindo mwingine kabisa kwamba kocha msaidizi wa klabu hiyo, Selemani Matola, amejiuzulu kwa madai kuwa hawezi kufanya kazi na kocha huyo Mwingereza. Upande wa pili inasikika kuwa kocha Kerr naye amekataa kufanya kazi na Matola lakini hajaandika kwa maandishi.
Kwa hiyo, hapo ni lazima mmoja kati ya Kerr au Matola aondoke na rais wa klabu hiyo amenukuliwa akisema kuwa misimamo mingine ya Kerr haitekelezeki. Kelele za kuwa Kerr anatakiwa kutimuliwa ziliposikika ilielezwa kuwa kuna viongozi hawamtaki kocha huyo na wanasubiri wakati wa mapumziko ya Ligi ndipo atimuliwe.
Kilichoibua hayo ni kipigo walichokipata kutoka kwa Prisons ya Mbeya lakini baada ya kugawa dozi nene kwa Majimaji ya Songea, hoja ile imepoteza mashiko na sasa limeibuka la kocha msaidizi kumkataa kocha mkuu kwamba hashauriki.
Maelezo ya kocha msaidizi Matola ni kuwa mwendo wa timu siyo mzuri na kwamba timu itaboronga huko inakoelekea, hivyo kwa kuwa yeye hasikilizwi ndiyo ameamua kuachia ngazi katika kipindi hiki cha mapumziko ya Ligi, ambacho kilisikika awali kuwa ndiyo kipindi cha kumuondoa kocha Kerr.
Filamu inaendelea lakini kabla Simba hawajaendeleza rekodi ya kutimua makocha ndani ya vipindi vifupi kwa kumtimua kocha wake mkuu, Dylan Kerr, ninataka kuwauliza kwani wana kiasi gani…?
Baruapepe: [email protected] Simu: 0715 36 60 10